HABARI
ya Mwenyekiti wa Klabu ya Bongo Movie Unity, Steven Mengere ‘Steve
Nyerere’ kujiuzulu wadhifa wake siyo mpya lakini Ijumaa Wikienda
linakudadavulia sababu zilizochochea bosi huyo abwage manyanga.
Kwa mujibu wa chanzo makini, bosi huyo alitakiwa ajiuzulu mwenyewe
katika mkutano wa wanachama uliofanyika Ijumaa iliyopita katika Viwanja
vya Leaders Club, kutokana na tuhuma mbalimbali huku wanaodaiwa
kutangaza nia ya kugombea urais 2015, Edward Lowassa na Bernard Membe
wakitajwa.
Mapaparazi wetu waliokuwepo eneo la tukio, walishuhudia wasanii mbalimbali wakiendesha ajenda ya kumng’oa Steve Nyerere.
Wanachama hao walidai kwenye uongozi wa Steve kumekuwepo na ufisadi,
kutumia madaraka vibaya na ubadhirifu mkubwa hivyo bora ajiengue. Steve
alionesha kukasirishwa na tuhuma hizo ambazo alidai hazikuwa na ukweli
wowote lakini hadi mwisho wa kikao, wanachama waliendelea kushikilia
msimamo wao kwamba ajiuzulu.
Punde tu baada ya kikao hicho kilichokosa muafaka kumalizika, Steve
Nyerere alitangaza kupitia mtandao wa Instagram kwamba amejiuzulu
wadhifa wake.Mapaparazi wetu walipomtafuta Steve alifunguka kuwa aliamua
kujiachia ngazi ili kulinda heshima yake.
Hata hivyo, madai ya Steve Nyerere kujiuzulu yalipingwa vikali na
wanachama wenzake wa Bongo Muvi waliodai kuwa amejikosha lakini ukweli
ni kwamba wamemng’oa.Uongozi wa Steve Nyerere ulioteuliwa mwaka jana,
umekuwa ukikumbwa na kashfa kibao za uchakuchuaji wa fedha zikiwemo za
rambirambi na mambo mengine yahusuyo klabu.
Hata hivyo, kuna tetesi kwamba wanasiasa wanaotajwa kuwania urais
2015, Lowassa na Membe ndiyo waliosababisha mtafaruku huo kwa kuwagawa
wasanii hao, kila mmoja akimshabikia mwanasiasa anayemtaka.
No comments:
Post a Comment