Imebainika kwamba sababu ya shambulizi
la risasi lililotokea Ilala Bungoni, Dar es Salaam Jumanne iliyopita na
kusababisha vifo vya watu watatu, ni wivu wa mapenzi uliopindukia.
Akizungumza nyumbani kwao Ilala Bungoni
jana, mmoja wa majeruhi ambaye ndiye aliyekuwa kiini cha shambulizi
hilo, Christine Newa alisema si kweli kwamba sababu ya mchumba wake,
Gabriel Munisi kuwashambulia na kuwajeruhi kwa risasi yeye na mama yake
mzazi, Ellen Eliezer na kumuua mdogo wake wa kike, Alpha Newa ni
kutokana na kusaliti uchumba wao.
Awali, ilidaiwa kwamba sababu ya
shambulizi hilo ni Christine kumkataa Munisi, (ambaye pia alijiua baada
ya kufanya mauaji hayo) na kuchumbiwa na rubani wa ndege, marehemu
Francis Shumila ambaye pia alifariki katika tukio hilo... “Kwanza
Shumila hakuwa mchumba wangu kama ilivyoelezwa. Alikuwa shemeji yangu,
mume wa dada yangu Caroline Newa. Pia hakuwa rubani wa ndege, bali
nahodha wa meli.”
Alisema amekuwa katika uhusiano wa
kimapenzi na Munisi katika kipindi kisichofikia mwaka mmoja lakini
sehemu kubwa ya maisha yao ikitawaliwa na misuguano iliyowafikisha
polisi mara kadhaa.
Alisema katika kipindi cha uhusiano wao
marehemu Munisi alikuwa akimpiga, akimkataza kufanya kazi, kusoma na
alikuwa na wivu uliopindukia.
Christine kuona hivyo, aliamua kufanya
mipango ya kwenda kusoma katika Visiwa vya Cyprus kimyakimya pasi na
kumuaga, jambo ambalo alisema lilimkera mchumba wake huyo na kuweka
kisasi.
“Nikiwa huko, Munisi alitafuta
mawasiliano hadi akayapata na tukawasiliana na siku niliporejea alikuja
kunipokea uwanja wa ndege lakini cha ajabu, alinikataza kwenda nyumbani
na badala yake akanipeleka moja kwa moja hadi Mwanza eneo la Kitangiri,”
alisema na kuongeza: “Tukiwa njiani kuelekea Mwanza, katika maeneo ya
Singida, alisimamisha gari akaniambia nishuke, akatoa bastola na
kuniuliza kwa nini niliondoka bila ya kumuaga. Je, nataka kumuacha?”
Alisema alimwomba msamaha na kuendelea
na safari yao. Anasimulia kwamba baada ya kufika Mwanza, alimpora simu
zake zote na kumfungia ndani kwa zaidi ya wiki mbili hadi alipopanda
kwenye dirisha na kuomba msaada kwa majirani na kuwapa namba za simu za
ndugu zake ili wamsaidie kuwapa taarifa.
Ndugu zake walianza mchakato wa
kuwasiliana na polisi hatua iliyofanikisha msichana huyo kurudishwa Dar
es Salaam... “Hata hivyo niliondoka na khanga na fulana tu. Vitu vyote
niliviacha huko.”
Baada ya kurudi Dar es Salaam, anasema
Munisi naye aliamua kumfuata lakini safari hii alifikia katika Hoteli ya
MM iliyotenganishwa na ukuta wa nyumba yao na akawa anafuatilia nyendo
za familia hiyo.
“Alikuwa ananitumia meseji kwamba
amemuona dada Caro, mama na Alpha na wakati mwingine anasema ameniona
mimi mpaka nguo tulizovaa, tukaanza kupata na wasiwasi,” alisema.
Wasiwasi huo ulitokana na historia ya
maisha yao ya Mwanza na pia tishio ambalo anadai kwamba Munisi aliwahi
kulitoa kwamba atahakikisha anaiteketeza familia yote kuanzia Goba
anakoishi mama yake (Ellen), Zanzibar anakoishi mdogo wake (marehemu
Alpha) na hapo Ilala.
Anasema walikwenda polisi lakini walielezwa kwamba hayo ni masuala madogo ya mapenzi na kwamba yatamalizwa kifamilia.
Siku ya tukio Christine alikuwa akitoka
kwenda uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kurudi shuleni Cyprus ndipo
Munisi alipotokea na kuanza kumrushia Shumila risasi na baadaye Alpha
kisha mama na yeye kabla ya kujiua.
Akizungumzia tukio hilo, Caroline
alisema mumewe alitabiri kifo chake kabla kwani baada ya kusikia vitisho
vya Munisi, alimtoa shaka Christine akimwambia kwamba atamlinda hata
ikibidi kupoteza maisha yake, jambo ambalo lilidhihiri.
Alisema mama yake amepata nafuu na
ameruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa
amelazwa na mazishi ya mdogo wake, Alpha ambaye ameacha mtoto mwenye
umri wa miezi minane, yamepangwa kufanyika Jumamosi Goba, Dar es Salaam.
Alisema mipango ya mazishi ya mumewe inafanywa huku akidokeza kwamba huenda akasafirishwa kwenda Mombasa.

No comments:
Post a Comment