Dar es Salaam. Mkenya Joshua Mulundi aliachiwa huru baada ya kulipa
faini ya Sh1,000 kwa kupatikana na hatia ya kuidanganya polisi kuwa
alihusika kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari
Tanzania, Dk Steven Ulimboka.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana baada ya
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka kusoma maelezo ya awali na
mshtakiwa huyo kukiri alitoa taarifa ya uongo kwa polisi kuhusu tukio
hilo.
Kabla ya hukumu hiyo, Mulundi aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwa
kuwa hilo lilikuwa kosa lake la kwanza. Pia alijitetea kuwa Juni 27,
2012 akiwa Arusha alitekwa na kupelekwa Dar es Salaam ambako alikuwa
hana mwenyeji wala hakuwahi kufika.
Alisema kutokana na kutekwa huko alichanginyikiwa hivyo kukubali
chochote alichoambiwa afanye kwa kuwa aliyemteka alikuwa na silaha na
alimwelekeza mambo ya kuzungumza.
“Mheshimiwa kwa ajili ya vitisho hivyo, nilikwenda Kawe katika Kanisa la
Ufufuo na Uzima lililoko kwenye eneo la Tanganyika Packers, mbele ya
Mchungaji Joseph Malwa Kiliba na kuungama kuwa ni miongoni mwa watu
waliomtesa Dk Ulimboka katika Msitu wa Pande,” alisema Mulundi na
kuongeza:
“Siwalaumu Serikali, upande wa mashtaka wala polisi kwa kitendo cha kuniweka gerezani kwa muda mrefu, najilaumu mimi mwenyewe.”
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Kweka aliiambia Mahakama kuwa hana
kumbukumbu za uhalifu za mshtakiwa lakini aliomba apewe adhabu kali
kutokana na mazingira ya tukio hilo.
Akitoa hukumu, Hakimu Katema alisema alifikia uamuzi huo kwa kuzingatia maombi ya mshtakiwa ya kupunguziwa adhabu.
No comments:
Post a Comment