Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe amefunguka na kuonesha masikitiko
yake kwa kitendo cha serikali kushindwa kuleta Bungeni mpango wake wa
maendeleo wa miaka mitano.
Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa Facebook ameweka wazi jambo ambalo
serikali inapaswa kufanya baada ya uchaguzi na kusema ni kuwasilisha
mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
"Shughuli ya kwanza ya serikali baada ya uchaguzi ni kuwasilisha
mpango wa maendeleo wa miaka mitano ( kutafsiri ilani yake kwenda kwenye
mpango wa utekelezaji) . Bunge linapaswa kujadili na kuidhinisha Mpango
wa Maendeleo wa miaka 5 na kisha Mpango wa mwaka mmoja kuanza
kutekeleza Mpango huo wa miaka 5. Kwa mujibu wa Katiba ya JMT Ibara ya
63(3)(c), Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 hutungiwa sheria kwa ajili ya
utekelezaji." Alisema Zitto Kabwe
"Leo Serikali ya Rais John Magufuli ilipangiwa kuwasilisha Mpango
huo wa Maendeleo wa miaka 5. Imeshindwa. Imeleta mwelekeo wa Mpango.
Haikuleta sheria na Kamati ya Bajeti Imeleta maelezo yake kuhusu Mpango
wa Maendeleo wa mwaka mmoja ilhali hakuna Mpango wa Miaka 5.
"Mwenyekiti Chenge alitaka wabunge wajadili kwa mujibu wa kanuni
ya 94 ambayo kimsingi ni Kanuni inayohusu Mpango wa mwaka mmoja.
Serikali imejichanganya. Uongozi wa Bunge umechanganyikiwa." Aliongeza Zitto Kabwe
Zitto Kabwe alimaliza kwa kusema kuwa ni aibu kubwa kwa serikali inayojinasibu kwa kauli ya "Hapa kazi tu"
"Bunge linapaswa kuagiza Serikali ikalete Mpango wa Maendeleo wa
miaka 5 ili uidhinishwe na utungiwe Sheria kabla ya kuanza kujadili
mipango ya mwaka mmoja mmoja.
"Ni aibu kubwa kwa Serikali ya #HapaKaziTu kushindwa kuleta
Bungeni Mpango wake wa Maendeleo wa miaka 5 na hata ule wa mwaka wake wa
kwanza. Itapangaje bajeti zake? Itatekeleza vipi ilani yake? Kuongoza
nchi sio kutumbua majipu tu, ni kuendesha nchi." Alimaliza Zitto Kabwe.
No comments:
Post a Comment