Jana, wakati Baraza la Uongozi la CUF likifanya mkutano wake kule
Buguruni Dar es Salaam, Pemba ilisimama. Ilisimama kimya na wima
ikifuatilia kitakachojiri mkutanoni. Pemba ilikuwa ikisubiri kwa hamu
uamuzi wa CUF juu ya kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa marudio wa
Zanzibar wa hapo tarehe 20 Machi mwaka huu.
Baada ya kikao kumalizika na kupatikana kwa taarifa kuwa CUF imeamua
kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio, Pemba iliripuka kwa shangwe, mayowe
na nderemo kana kwamba Taifa Stars imeingia fainali za kombe la dunia.
Au ni kama Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kiuchumi barani Afrika. Pemba
ikazizima.
Tafisiri ya hapo ni hii. Pemba imeikataa CCM na imeikumbatia CUF. Hata
kwenye matokeo ya uchaguzi wa Oktoba yaliyofutwa, CCM ilipigwa kwa KO
huku Pemba. Pemba na CUF, CUF na Pemba. Kama ni ngome, basi hapa Pemba
ni ngome ya CUF. Linaposemwa au kufanywa jambo lolote na CUF,jambo hilo
ni la Pemba yote. Unguja ni pasu kwa pasu. Wapo wa CCM wa kutosha, CUF
na vyama vingine.
Tafsiri ya pili ya nderemo za Pemba ni kuwa Pemba imekataa uchaguzi wa marudio. Wanataka waliowachagua Oktoba mwaka jana wapewe nafasi zao na Zanzibar isonge mbele. Uchaguzi wa marudio unatakiwa Unguja na si Pemba. Uchaguzi wa marudio haupokelewi kabisa hapa Pemba.
Pemba iko tofauti!
Mzee Tupatupa wa Lumumba (kwasasa Pemba)
No comments:
Post a Comment