Wazanzibari
wanaoishi nchini Uingereza leo wamefanya maandamano wakidai haki ya
kutangazwa ushindi wa Chama Cha Wananchi (CUF) katika uchaguzi mkuu wa
Zanzibar uliofanyika Octoba 25 mwaka huu
Maandamano
hayo yameandaliwa na Jumuiya ya Zanzibar Welfare Association (ZAWA)
ambapo wazanzibari hao wametoka maeneo mbali mbali katika miji yao na
kukusanyika katika eneo Downing Street kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu wa
Uingereza, David Cameron na uongozi huo kukabidhi barua yao yenye
malalamiko kutaka suala la Zanzibar lishughulikiwe.
Maandamano
hayo yamefanyika kwa lengo la kuongeza shindikizo kwa mamlaka ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuchukua hatua za haraka ya kuhakikisha Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inakamilisha kazi ya kutangaza matokeo ya
uchaguzi huo.
Uchaguzi wa
Zanzibar umekwamishwa na uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar, Jecha Salum Jecha Octoba 28 alipotangaza kufuta uchaguzi huo
wote kwa madai kwamba umekumbwa na matatizo mbali mbali.
Uamuzi huo
wa kufuta matokeo umepigwa na Chama Cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kwa
kuwa hauna ngumu kisheria ambapo Mwenyekiti wa tume hiyo hana mamlaka ya
kufuta uchaguzi ambao tayari ulishakamilika na matokeo yake kuanza
kutangazwa.
Wakati
jecha akitoa tangazo la kufuta matokeo bila ya kushauriana na tume yake
alikuwa tayari ameshatangaza matokeo ya kura za urais za majimbo 31 kati
ya 54 ya Zanzibar pia washindi wa nafasi za uwakilishi na udiwani
katika majimbo hayo walishatangazwa na walishakabidhiwa vyeti vyao.
Barua hiyo
iliyowasilishwa na Rashid Ali ambaye kiongozi wa ZAWA wamewasilishwa
barua hiyo wakiamini kwamba suala la Zanzibar litashughulikiwa ili
wananchi wa Zanzibar waweze kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Mwakilishi
wa ZAWA, Hassan Khamis alisema wameamua kupeleka barua kwenye ofisi za
waziri Mkuu wakiamini suala hilo litashughulikiwa ikiwa pamoja na
serikali ya Tanzania kuchukua hatua madhubuti na za haraka kaika
kushughulikia suala hilo ambalo limewaweka wazanzibari roho juu.
“Sisi kama
Wazanzibari wameshachoka na hali iliyopo sasa huko nyumbani kwetu ambao
kuna jamaa zetu na wazee wetu wanahitaji kuendelea na maisha yao hivyo
kuna kila sababu ya kumalizwa mgogoro uliopo ili waendeleaa na maisha
yao sasa hivi maisha yamekuwa magumu, vitu havinunuliki khofu imetanda
majeshi yamejaa na hali ya khofu ndio imekuwa kubwa kwa wananchi hawajui
saa ngapi kutazuka nini” alisema Khamis.
Wakizungumza
kwa njia ya simu baadhi ya wanawake walioshiriki maandamano hayo
wamesema wanaiombea dua Zanzibar ili mgogoro na mkwamo wa kisiasa
umalizike ili wananchi waweze kuishi kwa amani kwani suala la kuishi kwa
khofu linawatia huzuni hasa wao ambao wapo nje ya nchi.
“Tunaumia
tukisikia ndugu zetu wa Zanzibar wana mgogoro mwengine uliotokana na
uchaguzi kwa sababu ni miaka mingi kulikuwa na hali kama hiyo miaka
mitano nyuma kukatafutwa Maridhiano lakini sasa tunarejea nyuma miaka 15
iliyopita, haipendezi na pia inatutia sisi wasiwasi ambao tupo mbali na
ndugu zetu” alisema mmoja wa wanawake walioandamana.
Khamis
alisema wamekabidhi barua na imepokewa ambapo wameahidiwa kwamba barua
yao itafanyika kazi pamoja na kuonana na baadhi ya viongozi wengine wa
serikali ili kupeleka malalamiko yao yafanyiwe kazi haraka.
Wazanzibari
hao waliovalia nguo rangi nyekundu na buluu huku wengine wakiwa
wamebeba mabango yenye maandishi mbali mbali na picha za Mgombea Urais
wa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad
wameonekana wakiwa na furaha wakati wa maandamano hayo.
Hii ni mara
ya kwanza tokea kumalizika kwa uchaguzi wa Zanzibar kufanyika kwa
maandamano kama hayo nchini Uingereza ambapo baadhi ya wananchi
wanaoishi Marekani nao wameandaa maandamano yao ambayo yanatarajiwa
kufanyika wiki ijayo.
“ tutafanya
maandamano kuitaka Serikali ya Marekani kuingilia kati na kuweka
shindikizo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili mshindi
aliyeshinda atangazwe na serikali ya umoja wa kitaifa iundwe wazanzibari
washirikiane wajenge nchi yao” alisema mmoja wa wazanzibari anayeishi
Marekani.
Chanzo: Zanzibari yetu
No comments:
Post a Comment