Shughuli
mbalimbali jijini Arusha jana zilisimama kwa muda wakati umati wa watu
ulipofurika kumlaki Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyewasili
mkoani hapa kwa ajili ya kuendesha harambee ya ujenzi wa Msikiti wa
Patandi ulioko wilayani Arumeru.
Lowassa, ambaye jana
aliweka bayana kuwa atatangaza rasmi nia yake ya kuwania urais kwa
tiketi ya CCM, alienda kuendesha harambee kwenye msikiti huo baada ya
kutumwa kumwakilisha Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal.
Katika shughuli hiyo ya
harambee, Lowassa alifanikiwa kuchangisha Sh235 milioni, ikiwa ni zaidi
ya makisio ya msikiti huo ya kukusanya Sh200 milioni.
Harambee zimekuwa
zikichukuliwa kama uwanja wa kampeni wa makada wanaowania urais kupitia
chama tawala cha CCM na tangu apewe adhabu na wanachama wengine watano,
Lowassa hakuwahi kuonekana kwenye uchangishaji fedha hadi wiki mbili
zilizopita alipoalikwa na wagombea wengine wa urais wa CCM kwenye hafla
iliyofanyika Zanzibar.
Jana, mbunge huyo wa
Monduli alipokelewa kwa mbwembwe kwenye Uwanja wa Ndege wa Arusha ambako
alilakiwa na umati wa watu, wakiwepo waendesha pikipiki ambao
waliongoza msafara hadi viwanja vya msikiti mkuu wa Arusha.
Lowassa alifanya kazi
hiyo ya harambee ya kuchangia mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa tano
la msikiti huo litakalokuwa na shule ya sekondari, msikiti na kituo cha
watoto yatima.
Barabara ya Uhuru,
ambayo msafara huo ulipita ukiongozwa na pikipiki za polisi, ilifungwa
na wafuasi wa Lowassa, ambao magari yao yalikuwa na nembo za ‘Team
Lowassa’ na ‘Lowassa FU’ huku, wengine wakiwa na magari binafsi na
waendesha pikipiki.
Lowassa alitua uwanja
mdogo wa Arusha saa 7:30 mchana na alifika viwanja vya msikiti mkuu, saa
8:35 mchana na kulifanyika harambee ya kuchangia kituo cha elimu cha
kiislam na msikiti wa Patandi na kupokelewa na umati huku wakiimba
“rais, rais, rais” na kupokelewa na sheikh wa mkoa wa Arusha, Sheikh
Shaaban Juma.
Katika msafara huo,
Lowassa aliambatana na kaimu mkuu wa mkoa, Christopha Kangoye, mkuu wa
wilaya ya Arumeru, Hasna Mwilima, mbunge wa Kigoma Mjini, Peter
Serukamba na mbunge wa viti maalum (CCM) mkoa wa Arusha, Namelock
Sokoine.
Pia walikuwepo baadhi ya
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) wa wilaya, wafanyabiashara
wakubwa wa mkoa wa Arusha, Mwanza na Kilimanjaro, sambamba na watu
kadhaa wanaotarajiwa kugombea ubunge katika majimbo ya Arusha mjini,
Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi, Monduli, Londigo na Ngorongoro.
Amshukuru Dk Bilal
Akizungumza katika
harambee hiyo, Lowassa alisema si jambo dogo kupewa fursa kumwakilisha
makamu wa Rais Dk Bilal katika hafla hiyo.
“Baada ya Makamu wa Rais
kuniomba kuja kumwakilisha hapa, nilisita kidogo kwanza kutokana na
kuwa hapa ni nyumbani, pia bado nipo kifungoni na pia nimekuwa
nikialikwa katika harambee kadhaa za misikiti mkoani hapa na kushindwa
kufika,” alisema ambaye amefungiwa kujihusiaha na shughuli za uchaguzi
pamoja na makada wengine watano.
Alisema hata hivyo,
baadaye alikubali kwa kutambua jambo ambalo anamwakilisha Makamu wa Rais
ni la maendeleo kwa wananchi wa mkoa mzima wa Arusha na Taifa.
Avunja ukimya
Lowassa akizungumza na
mamia ya watu waliohudhuria katika hafla hiyo, alisema amekuja Arusha
akiwa na taarifa njema kuwa, Mei 24 atazungumza neno kwenye Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid.
Aliwataka wakazi wa Arusha kumuunga mkono, siku hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kumsikiliza.
“Mei 24 nitatoa neno
siku hiyo na mtu akikuuliza unakwenda wapi mjibu nakwenda kwenye safari
ya matumaini,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati wa watu.
Lowassa alipongeza
wakazi wa Arusha kwa umoja wao, wanaoendelea kuuonyesha bila kujali
itikadi zao, dini wala rangi, kutokana na kuhudhuria kwa wingi katika
harambee hiyo.
“Hii ndio Arusha
ninayoijua mimi, tumeishi kwa upendo na amani miaka mingi, tusikubali
kugawanywa kwani sote ni binadamu tulio sawa,” alisema
Achangisha 235 milioni
Katika harambee hiyo,
zaidi ya Sh235 milioni zilichangwa, wakati Lowassa, Makamu wa Rais na
marafiki zake, walichanga Sh105 milioni.
Lowassa alikabidhi Sh50
milioni taslimu kwa sheikh wa mkoa wa Arusha, ikiwa ni mchango wake,
makamu wa Rais na marafiki zake huku na kuahidi Sh50500 milioni.
Katika harambee, hiyo
Sheikh wa mkoa, alijisahau na kumuita Lowassa ‘Mh Rais’, na kusababisha
umati wa watu kushangilia. Fedha nyingine Sh130 milioni zilichangwa.
Baadhi ya wachangiaji
walikuwa ni marafiki wa Lowassa walioongozwa na Mathias Manga, ambaye ni
mjumbe wa NEC wa wilaya ya Arumeru, ambao walitoa Sh20milioni, Hussein
Gonga Sh7 milioni na Mkandarasi Jeremiah Ayo alitoa Sh5milioni.
Mgombea watarajiwa wa
ubunge, Mustapha Panju alitoa Sh6 milioni, Sioyi Sumari (Sh7 milioni),
Kim Fute (Sh3 milioni), Philemon Mollel (Sh5 milioni), mbunge Peter
Serukamba (Sh3 milioni) na mjumbe wa NEC kutoka jimbo la Busega, Dk
Raphael Chegeni alichanga Sh1 milioni sawa na mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema na Namelock Sokoine.
Gharama
Awali akizungumza kabla
ya kuanza kwa harambee hiyo, katibu wa Bakwata mkoani Arusha, Juma
Masoud alisema kuwa mradi wa ujenzi wa msikiti huo unatarajiwa kugharimu
Sh1 bilioni hadi kukamilika.
Alisema kuwa mradi huo
ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo wanatarajia kuitekeleza na kwamba
ujenzi utahusisha ghorofa tano na ndani yake kutakuwa na kituo cha
watoto yatima.
“Waumini katika msikiti
huu kwa sasa wanakbiliwa na changamoto ya sehemu ya kufanyia ibada hivyo
kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuokoa tatizo hilo,” alisema.
Alisisitzia kuwa awamu
ya kwanza ya mradi huo unataraji kugharimu jumla ya kiasi cha Sh200
milioni na alimpongeza Lowassa kwa kujitoa katika juhudi za kusaidia
maendeleo ndani ya jamii.
Naye Sheikh Shaaban
alisema harambee hiyo inahusu wakazi wote wa Arusha kwani sekondari
itakayojengwa haitakuwa ya dini moja hivyo, aliwashukuru wote
waliochangia na mungu atawalipa
No comments:
Post a Comment