Moshi. Mhasibu wa
Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa kazi kwa tuhuma za
kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.
Kuvuja kwa ujumbe huo na nambari ya simu iliyotuma, kumeibua hisia
tofauti kuhusu usiri wa ofisi ya Rais katika kushughulikia malalamiko
nyeti ya wananchi na kuwaweka njiapanda watoa habari za siri.
Mhumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya na
Serikali Kuu (Tughe) Tawi la KCMC anadaiwa na Menejimenti ya KCMC kuwa
ndiye aliyetuma ujumbe huo.
Katika barua yake ya Mei 5, yenye kumbukumbu PF.4515/22, KCMC ilidai uchunguzi umebaini kuwa Mhumba ndiye mtumaji wa ujumbe huo.
“Uongozi umepokea taarifa iliyotumwa mwishoni mwa Aprili na mwanzoni mwa
Mei mwaka huu kwa njia ya ujumbe wa simu kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete,” ilidai.
KCMC imedai katika barua hiyo, taarifa hiyo ya sms ilibeba ujumbe
unaohusiana na matumizi mabaya ya fedha za hospitali hiyo unaofanywa na
baadhi ya viongozi na Shirika la Msamaria Mwema (GSF).
Mbali na tuhuma hizo, lakini pia KCMC inadai taarifa hiyo ilimweleza
Rais kuwa KCMC na GSF linalomiliki hospitali hiyo, zinajitosheleza kwa
mapato, hivyo hakuna haja kwa Serikali kuendelea kuipatia ruzuku.
Pia, menejimenti imedai taarifa hiyo ilidai wafanyakazi wa KCMC
wanatumikishwa kama watumwa, hivyo ni maombi yao (watumishi) Serikali
ilegeze masharti ili ajira zao zichukuliwe na Serikali.
“Uchunguzi umeonyesha kuwa taarifa hiyo (kwa Rais), umeituma kwa kutumia
simu ya kiganjani ambayo ulikabidhiwa kama mojawapo ya zana ya kuleta
ufanisi katika majukumu yako,” imedai.
Mei 8, KCMC ilimwandikia barua Mhumba yenye kumbukumbu PF.4515/28
iliyotiwa saini na Profesa Raimos Olomi ikimjulisha kuwa amesimamishwa
kazi kuanzia Mei 8 hadi Mei 14.
Katika barua hiyo, Profesa Olomi alidai menejimenti imepokea taarifa ya
kutofanyika kwa kikao cha kamati ya nidhamu baada ya Mhumba kumkataa
mwenyekiti kutokana na kukosa imani naye.
Pia, kikao hicho hakikufanyika baada ya Mhumba kuomba kamati hiyo
iahirishwe kwa sababu mwakilishi wake hakuwapo na kikao kingine kupangwa
Mei 15.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment