UTAJIRI wa komediani maarufu Bongo, Emmanuel Mgaya ‘Masanja
Mkandamizaji’ ni kufuru! Tena unatisha na sasa anaonekana kuwa miongoni
mwa wasanii wACanaomiliki fedha na mali nyingi Bongo, Risasi
Mchanganyiko linakupa zaidi.
HABARI MEZANI
Awali, habari
kuhusu utajiri wa Masanja ilitua mezani mwa gazeti hili kama kidokezo,
hapo mwandishi wetu akaingia mzigoni na kuanza kuchunguza kwa kina mali
anazomiliki msanii huyo na kugundua kuwa ni kati ya mastaa mabilionea
Bongo.
“Masanja sio yule tena. Ana mpunga (fedha) mrefu sana. Hakuna
msanii wa maigizo Bongo anayeweza kumfikia kwa sasa. Hao wengine ni
mbwembwe tu, lakini pesa imelala kwa Masanja,” kilipasha chanzo chetu.
Kikaongeza: “Kwanza ana ghorofa lipo Tabata, hapo ndipo anapoishi. Pia
ana magari kibao ya kifahari, mashamba ya mpunga na Kampuni ya OK
Security inayolinda sehemu mbalimbali zikiwemo taasisi nyeti nchini.
“Ni msanii gani mwenye kampuni kubwa kama ya Masanja? Wengi wanaishia
kudai wanatayarisha filamu ambazo hata matunda yake hayaonekani.”
RISASI MZIGONI
Mdogomdogo, Risasi Mchanganyiko likajitupa mtaani kuchimba kuhusu madai hayo ambayo awali liliyatilia shaka kama si wasiwasi.
Uchunguzi wetu ulibaini ukweli wa mali za msanii huyo na mambo mengine mengi yanayoingia kama vyanzo vya mapato yake.
MAGARI SITA
Ilibainika kuwa, Masanja anamiliki magari sita, yakiwemo ya kifahari.
Baadhi ya magari hayo ni Toyota Land Cruiser V8, Nissan Hardboad na
Toyota Verossa.
NYUMBA TATU BONGO
Pia, mkali huyo wa kuvunja mbavu, anamiliki nyumba tatu za maana jijini
Dar es Salaam, moja ni ghorofa ipo Tabata, nyingine Kigamboni na
nyingine haifahamiki eneo rasmi ilipo.
Hata hivyo, imebainika kuwa mbali na mijengo yake hiyo iliyopo jijini Dar, nyumbani kwao Mbarali, Mbeya ana mjengo wa maana.
MASHAMBA KIBAO
Msanii huyo hayupo nyuma kwenye kilimo, ana mashamba kadhaa Kigamboni
jijini Dar es Salaam lakini linalotia fora ni lile lililopo Mbarali
lenye ukubwa wa hekari 50 ambalo analima mpunga.
NI MSANII WAMAIGIZO TAJIRI ZAIDI?
Kwa utajiri huo, ipo minong’ono kuwa, nyota huyo anaweza kuwa kwenye namba za juu za wasanii wa maigizo wenye mkwanja mrefu.
Wengine wanaotajwa kwenye orodha ya waigizaji matajiri Bongo ni Husna
Posh ‘Dotnata’, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ na Amri Athumani ‘Mzee
Majuto’.
]MATAJIRI BONGO FLEVA
Katika muziki wa Bongo Fleva, wasanii wanaoaminika wana utajiri mkubwa
zaidi ni Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Joseph
Haule ‘Profesa Jay’.
Wasanii hao wanamiliki mijengo ya maana, achilia mbali magari ya kifahari na miradi kadhaa.
MASWALI KUHUSU MASANJA
Utajiri wa Masanja umeonekana kuibuka ghafla huku vyanzo vyake vya
kumwingizia kipato vikijulikana ni sanaa ya uigizaji, muziki na huduma
ya uchungaji.
Je, kwa uigizaji tu katika Kundi la Orijino Komedi ‘OK’ ndiko alikopata mkwanja huo na kuanzisha miradi hiyo mikubwa?
Kama ndiyo, kwa nini memba wenzake ndani ya kundi hilo hawana maendeleo makubwa kama yeye?
Kazi nyingine ya Masanja ni muziki wa Injili ambapo kwa sasa albamu
yake ya Hakuna Jipya iko sokoni. Je, albamu hiyo na shoo anazofanya
zinaweza kuwa chanzo cha utajiri huo?
Lakini pia Masanja ni
mchungaji ambaye anahudumu katika Kanisa la Evangelist Assemblies of God
Tanzania (EAGT) ‘Mito ya Baraka’ lilicho chini ya Askofu Bruno
Mwakiborwa. Je, mshahara anaoupata kutokana na huduma hiyo unaweza kuwa
chanzo cha mapato yake?
Risasi Mchanganyiko halikutaka kupasua
kichwa, juzi lilimsaka Masanja kwa simu na kumhoji juu ya mali zake
ambapo kwanza alithibitisha kweli anamiliki mali hizo na nyingine ambazo
hakupenda kuzitaja.
“Ni kweli nina nyumba tatu hapa mjini,
kampuni ya ulinzi na mashamba ya mpunga eka 50 nyumbani Mbarali, Mbeya.
Kuhusu magari pia ni kweli kabisa. Mimi ni mtumishi sitakiwi kusema
uongo,” alisema Masanja.
RISASI: Lakini mbona utajiri wako umekuwa wa haraka sana mtumishi, vipi vyanzo vya mapato yako?
MASANJA: Orijino Komedi ndiyo chanzo cha vyote... pale ndipo kwenye koki.
RISASI: Kuchekesha tu kaka? Au kwenye muziki wa Injili pia kunalipa?
MASANJA: Injili na uchungaji ninaotumika kanisani ni huduma kaka,
sitegemei mapato kutoka huko. Nipo kwa ajili ya kulisha kondoo wa Bwana.
RISASI: Wasanii wenzako wa Orijino Komedi wanachukuaje mafanikio yako?
MASANJA: Wanafurahia, wananiunga mkono maana ni sehemu ya mafanikio yao
pia. Sisi tunaishi kama ndugu. Kwa hiyo kuna baadhi ya aidia ni zao,
hivyo wanajivunia sana mafanikio yangu.
No comments:
Post a Comment