Stori: Jelard Lucas
ASKOFU
na Nabii George David ‘Geordavie’ wa Kanisa la Geordavie Ministry
‘Ngurumo ya Upako’ lililoko jijini Arusha na Kawe, Dar hivi karibuni
alifanya mkutano mkubwa na kutikisa nchi kwa kuwa na magari ya kifahari
na ndege aina ya helikopta ‘chopa’ iliyokuwa ikirandaranda juu ya anga
kulinda usalama wake, Uwazi lina ushuhuda wa kutosha.
Katika mkutano huo uliofanyika Karatu mkoani Manyara, mwandishi wetu
alishuhudia msafara wa Geordavie ambaye hutoa huduma ya uponyaji kwa
njia za miujiza, ukiwavutia watu wengi kwa kuwa ulikuwa na ulinzi mkali
ambao haujawahi kutokea.
Mbali ya kuwa na chopa iliyokuwa ikiimarisha ulinzi ambayo ameinunua
hivi karibuni, askofu huyo alikuwa na msururu wa magari yenye thamani
kubwa yanayomfanya kutajwa kuwa tajiri kuliko maaskofu wengine wanatoa
huduma katika makanisa ya kiroho Tanzania.
Akiwa Karatu, mbali na ulinzi binafsi, Geordavie alikuwa akilindwa na
askari wa jeshi la polisi, askari kanzu, Askari wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU) na wale wa usalama barabarani.
Mbali na askari hao wa serikali ambao wamekuwa wakimlinda kila
anapofanya mikutano yake, pia Geordavie analindwa na askari wake binafsi
hali iliyowafanya baadhi ya watu kuamini kuwa ulinzi wake ni kama ule
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’.
“Sijawahi kumuona JK akilindwa na chopa lakini mtumishi wa Mungu
Geordavie analindwa na ndege katika msafara wake! Hii ni mara yangu ya
kwanza kuona,” alisema muumini mmoja ambaye hakupenda kutajwa gazetini.
Hata hivyo, baadhi ya watu walikuwa wakihoji utajiri wa askofu huyo
kutokana na fedha nyingi anazozitumia anapofanya mikutano katika sehemu
mbalimbali jijini Arusha.
“Tunajua kuwa ni tajiri, lakini anapata wapi fedha za kutumia hivi?”
alihoji muumini aliyejitambulisha kwa jina moja la Julius ambaye naye
alihudhuria mkutano wa askofu huyo anayetumia kaulimbiu ya Ngurumo ya
Upako katika kutoa huduma yake.
Pia, waumini wengine walilalamikia ugumu wanaoupata wanapotaka
kumuona mtumishi huyo wa Mungu kutokana na ulinzi mkali anaopewa.
“Kila mtu alitamani kumuona mtumishi wa Mungu lakini haikuwezekana
kutokana na ulinzi wake kuwa mkali, utajiri wake hakuna mfano, hata kule
nyumbani kwake Arusha, anaishi kama Mfalme Daud,” alisema Fred Mushi.
Gazeti hili lilimsaka Askofu na Nabii Geordavie kwa lengo la kutaka
kujua sababu ya kuwa na ulinzi mkali na kutumia magari ya kifahari
ikiwemo chopa katika mikutano anayoifanya lakini simu yake iliita bila
kupokelewa.
No comments:
Post a Comment