KWELI huu ni unyama wa wanaume hata kama si wote! Wanawake wawili
wakazi wa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, wamepoteza maisha
kufuatia madai ya kuuawa na waume zao. Inauma sana na Uwazi ndilo lenye
mkasa mzima!
Matukio yote mawili yametokea jijini Dar es Salaam na
kuacha vilio kwa ndugu na jamaa wakiwa hawaamini kilichowakumba wapendwa
wao.
WALIOTENDWA
Wanawake waliojulikana kwa majina ya Mwanahamisi na
mwenzake Waisiko Robert Mtundi ndiyo waliodaiwa kuuawa na waume zao,
kisa kikubwa kikidaiwa ni hofu ya wanaume hao kusalitiwa katika mapenzi.
WANAODAIWA KUTENDA
Juma Shaban, mkazi wa Manzese Kwamfuga Mbwa na
Samuel Gesire Mlimi, mwenye makazi yake Msongola, maeneo yote hayo yapo
Dar ndiyo wanaodaiwa kutekeleza ukatili huo wenye kutoa machozi mpaka
basi.
MWANAHAMISI ALIVYOUAWA
Ilikuwa saa tatu usiku, Septemba 21, mwaka
huu, kila familia ya eneo la Kwamfuga Mbwa ilikuwa ndani kwa chakula cha
usiku au maandalizi ya kulala, ndipo waliposikia zogo kutoka ndani ya
chumba cha kwa wanandoa hao.
ZOGO NA MANENO
Kwa mujibu wa majirani hao waliozungumza na gazeti
hili baada ya tukio, zogo hilo liliambatana na maneno ya shutuma kutoka
kwa Juma kwamba mkewe huyo si mwaminifu ndani ya uhusiano wao.
Majirani walisema shutuma za Juma ziliambatana na kelele za Mwanahamisi kuomba msaada akisema ‘nauawa jamani! Nauawa mwenzenu!’
Wakasema
baada ya kama saa moja ya mzozo ulipita ukimya, ndipo kila jirani
alitoka nje na kuulizana nini kinaendelea ndani ya chumba cha
Mwanahamisi na mumewe!
“Baada ya dakika kumi, tulimwona Juma akitoka
chumbani kwake huku akiwa anabofyabofya simu yake ya mkononi na
kutokomea kusikojulikana,” alisema jirani mmoja huku macho yakiwa
yamevimba kwa sababu ya kumlilia Mwanahamisi ambaye wakati huo alikuwa
chini ameshakata roho.
Akaendelea: “Baada ya Juma kuondoka tulipatwa
na wasiwasi, tukaenda kumwangalia Mwanahamisi chumbani na kumkuta
hajitambui, amelala kifudifudi, ana majeraha sehemu mbalimbali za mwili
huku akiwa ametapakaa damu. Alikuwa akipumua kwa mbali.
“Alikuwa
hawezi kuongea vizuri, mimi nilimsikia akisema hana uhai tena, tumwombee
mtoto wake. Ndani ya chumba tuliona viroba vya pombe kali na kisu
kikiwa kimelowa damu, nahisi ndicho alichotumia Juma kufanyia ukatili
wake.
“Tuliamua kumwahisha hospitali Mwanahamisi lakini kutokana na
hali yake tuliona ni vizuri kuwasiliana na polisi ambao walifika baada
ya muda.
“Lakini siku yake Mwanahamisi ilitimia kwani wakati polisi wakijiandaa kumchukua kumkimbiza hospitali aliaga dunia.”
KUMBE NI MWEZI MMOJA BAADA YA KUHAMIA
Wengine waliozungumza na
gazeti hili siku ya tukio huku wakitoa machozi, walisema Juma ambaye
alitoroka baada ya ukatili huo, alihamia kwenye nyumba hiyo mwezi mmoja
nyuma lakini walipata umaarufu mtaani hapo kutokana na tabia yao ya
kupigana mara kwa mara.
MJUMBE WA MTAA NAYE ANENA
Akizungumza na gazeti hili katika eneo
la tukio, Mjumbe wa Nyumba Kumi, Techla Tesha aliwalaumu majirani na
wapangaji wa nyumba hiyo kwa kushindwa kumpelekea taarifa mapema huku
wakijua mtuhumiwa alikuwa na tabia ya kumpiga mkewe mara kwa mara.
WAISIKO ALIVYOUAWA
Awali ya yote, inadaiwa Waisiko ni mke mkubwa, mke mdogo jina lake halikupatikana mara moja.
Siku
ya tukio, saa tatu usiku inadaiwa Samuel alikwenda nyumbani kwa Waisiko
ambapo si mbali sana na nyumbani kwa mke mdogo na kuangusha timbwili
zito.
“Samuel aliingia ndani na kuanza kumpiga mkewe mkubwa huku akionya majirani kuwa asiwepo mtu wa kwenda kuamua ugomvi wao.
“Sisi kama majirani tuliogopa kwa sababu Samuel alikuwa akitishia kuwa atakayeingia atamchoma kisu.
“Licha
ya vitisho hivyo, tulisimama nje ya chumba chao huku vitisho
vikiongezeka lakini namna ya kutoa msaada tulishindwa. Hatukujua chanzo
cha ugomvi wao.
“Kauli za mwanamke kila wakati ziliashiria alichokuwa
akitendwa kwa wakati huo, mfano kuna wakati tulimsikia akisema
anavunjwa mgongo, akasema anang’olewa kucha. Pia kuna muda alilalamikia
kuvunjwa mkono. Jamani, marehemu aliteswa sana kabla ya kufariki dunia,”
alisema shuhuda mmoja.
NI MATESO YA USIKU KUCHA!!
Shuhuda
huyo aliongeza: “Mateso ya mwanamke huyo huenda yalikuwa ya usiku kucha
kwani nakumbuka mpaka alfajiri ndipo tukasikia sauti ya mwisho ya
Waisiko akisema Samuel umeshaniua, nimalizie kabisa basi. Baada ya hapo
hatukusikia tena sauti wala vurugu.
SERIKALI YA MTAA YAZUNGUMZA
Makamu
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msongola, Juma Chacha alipohojiwa
kuhusiana na mauaji hayo, alisema ana taarifa lakini mtuhumiwa alikimbia
baada ya kutenda unyama huo na anatafutwa na polisi.
UWAZI LABAINI KISA
Uchunguzi
wa gazeti hili ulibaini kuwa chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa mapenzi
kwani ilidaiwa kuwa Samuel alikuwa akimhisi mkewe huyo kutoka nje ya
ndoa.
Chanzo chetu kilisema siku ya tukio, Samuel aliwachukua baadhi
ya marafiki zake na kwenda nao baa ambako aliwaambia kuwa anahisi mkewe
huyo ana jambo kwani akimuuliza kitu anamjibu jeuri.
Mtoa habari wetu alisema Samuel akiwaambia marafiki hao kwamba siku hiyo akirudi nyumbani, mwanamke huyo atamtambua.
POLISI WALIVYOIKUTA MAITI
Polisi
walipofika na kuichunguza maiti waliikuta imevunjwa mkono wa kushoto na
kung’olewa kucha za miguu huku uti wa mgongo nao ukiwa umevunjika.
Habari
zinasema mara baada ya mtuhumiwa kufanya mauaji hayo, alikwenda kwa
mkewe mdogo na kumtaka akamuone mke mwenzie, alipokwenda yeye nyuma
akatoroka.
Polisi Mkoa wa Ilala tayari wamemfungulia jalada mtuhumiwa huyo lenye namba STK/RB/10058/2013 MAUAJI.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Marietha Minangi amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment