01 October 2013

MAPENZI YA JINSIA MOJA YASHAMIRI AFRIKA MASHARIKI.



MAPENZI ya jinsia moja ni moja ya biashara inayozidi kushamiri katika nchi za Afrika Mashariki na kuchangia maambukizi makubwa ya Ukimwi. Kutokana na hali hiyo, nchi za Afrika Mashariki zimetakiwa kuangalia namna ya kuokoa maisha ya mashoga, ili wasiendelee kuteketea na ugonjwa hatari wa Ukimwi badala ya kuwanyanyapaa.
Akizungumza jana katika mkutano unaojadili masuala ya afya kwa watu wanaosafiri, wahamiaji na watu wanaozunguka sehemu mbalimbali, Mratibu wa Chama cha Watu wanaofanya biashara ya ngono nchini Kenya, John Mathenge alisema jambo la hatari ni kwamba hata viongozi wakubwa serikalini wanapenda kufanya mapenzi na mashoga.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na Asasi ya Kimataifa ya Wahamiaji (IOM), Mathenge alisema pamoja na desturi za kiafrika kukataza vitendo vya ushoga na usagaji, lakini wapo watu katika jamii wanaofanya mapenzi hayo kama biashara ya kuwapatia kipato au kujifurahisha.
Alisema shirikisho la watu wanaofanya kazi za mapenzi lina wanachama wengi hapa nchini wapatao kama 40,000.
"Unajua biashara hii ya kuuza mwili ni kazi sawa na kazi zingine, mtu anaweza kuamua atumie mwili wake kuwa mkimbiaji, mwingine kuwa kahaba au shoga zote hizi ni kazi na wanaofanya kazi hiyo hawapaswi kulaumiwa na jamii bali wasaidiwe ili wasiambukizwe Ukimwi," alisema.
Alisema kwa kuwa watu hao wako katika jamii yetu na wanafanya mapenzi na viongozi na watu wa kawaida, maambukizi ya Ukimwi yanazidi kuongezeka hivyo kuna haja ya Serikali kukubali kuzungumza na mashoga na makahaba wengine ili kuangalia namna ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
"Tuache tabia ya kuwanyanyapaa, tukienda hospitali tunanyanyapaliwa tunaambiwa twende na wapenzi wetu, tutawatoa wapi wakati mtu umekutana naye kwa siku moja tu? Ukweli ni kwamba kila mtu hapa duniani anafanya biashara ya ngono ila katika mfumo tofauti.
"Wewe wakati unataka kuoa mke wako ulitoa mahari ili aje kwako, au kuna watu wana vimada wanawapelekea zawadi ili waendelee kupewa mapenzi, hawa nao wanafanya biashara ya ngono, sasa iweje sisi ambao tumejitokeza tuanze kunyanyapaliwa? Alihoji Mathenge.
Alisema hata kuongezeka kwa wahamiaji haramu kumetokana na kuwepo biashara hiyo ya ngono ambayo inafanywa na maofisa wa Serikali kama Uhamiaji ambao wanapewa ngono na wasichana na kuwaachia waingie kwenye nchi husika bila kuwa na vibali vinavyotakiwa kisheria.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Mohamed Sharrif Abdukadir, alisema urasimu uliopo kwenye mipaka katika kushughulikia nyaraka za mizigo ndizo zimekuwa zinachangia madereva wanaosafiri kwenda nchi jirani kuingia katika vitendo vya ngono.
Alitoa mfano wa mpaka wa Tunduma kuwa unaongoza kwa kuwa na urasimu kutokana na mfumo uliopo wa kushughulikia nyaraka hali inayomfanya dereva wakati mwingine akae wiki mbili eneo hilo hivyo kujikuta anafanya vitendo vya ngono.
Hata hivyo alisema asasi ya IOM kwa kushirikiana na Chama cha Madereva wa Masafa Marefu imewasaidia kuwapa ushauri wa namna ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi wakati wanapokuwa safarini.
Abdukadir alisema tayari kumejengwa vituo vijulikanavyo kama One Stop Border Posts ambavyo vinatumiwa na madereva kwenda kupata ushauri na kupima afya zao.
Alisema vituo hivyo viko chini ya IOM vinatoa semina kwa madereva na hata kama mtu anakutwa ameambukizwa anapewa dawa za kurefusha maisha. Eva Mwai ambaye ni Mratibu wa Asasi ya North Star Alliance katika ukanda wa Afrika Mashariki, anasema asasi yake imekuwa inatoa msaada wa kiafya kwa watu wanaozunguka kwa vile hawana muda wa kwenda kupimwa hospitalini.
Alisema wanafanya utafiti katika maeneo mbalimbali ambako ni hatarishi kwa madereva na wanajenga kliniki maalumu kwa ajili ya kutoa afya na ushauri kwa madereva na watu wengine ambao wana maisha ya kuzunguka.
Alisema wana vituo vya afya huko Mombasa, Tunduma, Kahama na Mwanza kwa ajili ya kufanya upimaji kwa watu wanaozunguka.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mbarak Abdulwakil aliwataka washiriki wa mkutano huo ambao wanatoka nchi mbalimbali kubadilisha uzoefu wa namna ya kushughulikia afya kwa watu wanaozunguka, wahamiaji mbalimbali hasa katika eneo hili la ukanda wa Afrika Mashariki

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname