17 February 2015

Magaidi wa Tanga' Watiwa Mbaroni.....Mwili wa Mwanajeshi wa JWTZ Aliyeuawa katika Mapigano hayo Waagwa


Serikali imetoa taarifa rasmi kuhusu uhalifu uliotikisa mkoani Tanga, ikisema hali ni shwari na umma wa Watanzania upuuze taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikitia hofu.

Aidha, imesema  watu kadhaa wanashikiliwa wakihusishwa na uhalifu huo.
 
“Tunawashikilia ila mpaka sasa siwezi kukueleza idadi yao na kwamba ni wa kikundi cha ugaidi au la. Hao watu tunafanya nao mahojiano ili kuweza kuelewa kama wanahusika kwenye tukio hilo,”  alisema Kaimu Kamanda wa Polisi  wa Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki.
 
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Ndaki alisema hali katika kitongoji cha Majimoto, Amboni na mkoa wa Tanga kwa ujumla iko shwari. “Tunaendelea kufanya uchunguzi kubaini hao wahalifu pamoja na silaha zilizoibwa,” alisema.
 
“Tunaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano wao hasa wanapoona watu wenye majeraha au wanaowahisi kwamba ni wahalifu ili nasi tuweze kuwachunguza kama wanahusika kwenye tukio hili”, alisema.
 
Ingawa Kamanda hakuelezea mazingira ya kukamatwa kwa watuhumiwa, waandishi wa habari waliozuru eneo la Amboni  yalikotokea mapigano, waliarifiwa kwamba baadhi ya wavuvi kwenye Mto Zigi, walimkamata mtu wakimtuhumu kukutwa akifua nguo zenye damu.
 
Katika mapigano hayo baina ya askari na wahalifu, yalisababisha kifo cha askari wa JWTZ,  Sajenti Said Kajembe na wengine kujeruhiwa.
 
“Asubuhi wavuvi kadhaa walikuwa hapo mtoni ghafla walikutana na mtu pembeni ya mto akiwa anafua kanzu pamoja na vifaa fulani kama nguo za kufunika uso ..’maski’ ikabidi wawapigie haraka polisi simu lakini hawakuweza kupatikana na ndipo wakawapigia askari wa JWTZ ambao walifika haraka eneo la tukio na kumkamata mhusika”, alisema mkazi mmojawapo.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga,  Magalula Said Magalula aliwataka wakazi wa Tanga na vitongoji vyake, kuondoa hofu kwa kuhakikisha wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji kwa sababu ulinzi umeimarishwa na hali ya usalama ni  shwari.
 
Pia, aliwataka wananchi na wageni wenye mpango wa kutembelea eneo la kihistoria la Mapango ya Amboni, kuendelea na ratiba zao kwa sababu eneo hilo liko salama na tangu awali halikuhusika kwenye vurugu hizo.
 
Magalula ambaye pia alikutana na waandishi wa habari, alisema “Hali ni nzuri ulinzi na usalama uko imara… naomba wananchi waondoe hofu, wawe na amani na waendelee na shughuli zao za uzalishaji… hakuna tatizo kabisa usalama umedhibitiwa vizuri.”
 
Mkuu huyo wa mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alisisitiza  “Naomba Watanzania wenzangu muelewe kwamba eneo lilipofanyika tukio la mapigano na wahalifu si pale yalipo mapango ya Amboni ... maeneo hayo yapo mbali na nitoe mwito kwa wageni wenye mpango wa kutembelea hapo wawe huru kufanya hivyo mahali hapo ni salama.”
 
“Naomba Watanzania nchini kote kwa ujumla wawe na amani kwa sababu Tanga iko shwari hakuna tena hizo vurugu za wahalifu… naomba wasiamini sana taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii… sisi tuko shwari na shughuli za kijamii zinaendelea kama kawaida ikiwemo Amboni,” alisema.
 
Akizungumzia mapigano hayo yaliyotokea  Februari 14,  alisema licha ya majibizano ya kurushiana risasi yaliyofanywa na askari wa Polisi kwa kushirikiana na wa JWTZ , uchunguzi unaendelea  kuwapata wahusika.
 
“Vikosi vya usalama vinaendelea na juhudi za kuwasaka pamoja na kutafuta silaha zetu lakini hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa … zipo simulizi mbalimbali zinazoendelezwa kwenye mitandao ya kijamii ila sisi serikali ya mkoa bado hatujathibitisha kwamba watu hao ni wa kikundi gani ila ninachokifahamu hao watu ni wahalifu”, alisisitiza.
 
Kuhusu kuongezeka kwa matukio  katika maeneo mbalimbali mkoani humo,  alisema kila tukio linachukuliwa kwa uzito mkubwa na linashughulikiwa kwa namna linavyotokea.
 
Aidha, amewataka wakazi wa Tanga hususan wanaoishi eneo la Amboni na vitongoji vyake kuhakikisha wanaendelea kutoa habari sahihi kuhusu watu mbalimbali wanaowatilia shaka . Alisema taarifa hizo zina umuhimu wa kipekee kwa askari katika kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao.
 
Kutokana na maswali mengi ya wanahabari na wananchi, kudai kutoridhishwa na mwenendo  wa utoaji taarifa kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Mkoa aliruhusu watembelee eneo la tukio  kuthibitisha kama hali ni shwari katika eneo husika.
 
Timu ya wanahabri takribani 10 kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakiwa chini ya ulinzi wa askari walipelekwa eneo la tukio, ambalo liko umbali wa takribani kilometa tano kutoka yaliko Mapango ya kihistoria ya Amboni.
 
Eneo hilo limetawaliwa na miamba ya mawe makubwa yenye mapango, ambayo hayatumiki kwa shughuli za kihistoria, kama ilivyo katika kitongoji cha Kiomoni yalipo mapango ya kihistoria ya Amboni.
 
Shughuli zinazoonekana kufanyika jirani na eneo hilo, ni ulipuaji wa miamba kwa kutumia baruti ambao hufanywa na wachimbaji wadogo kisha kuvunja kokoto  kwa ajili ya viwanda vya kutengeneza chokaa pamoja na mawe kwa shughuli za ujenzi mjini hapa.
 
Eneo wanakodaiwa kuishi wahalifu hao,  liko umbali wa meta 300 kutoka upande wa pili zinapofanyika shughuli za upasuaji  kokoto zinazoendeshwa na wakazi wa kitongoji cha Majimoto na Mafuriko huko Amboni.
 
Katika eneo hilo,  kulikuwa na ukimya kutokana na kutokuwapo shughuli yoyote hususani uvunjaji kokoto iliyozoeleka kutokana na wananchi kusimamishwa kutokana na tukio hilo.
 
Waandishi wa habari walilazimika kufuata maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na wanausalama waliokuwa wakiwaongoza  kufika ndani ya pango husika.
 
Mwonekano wa eneo hilo, ulidhihirisha ni la hatari kutokana na mapango kufunikwa na vichaka. Ndani ya pango hilo, upo uwazi mkubwa unaoashiria uwepo wa shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikiendelea.
 
Ndani ya pango hilo, zilikutwa nguo; hususan suruali, madumu ya kuhifadhia maji, vikombe kadhaa vya plastiki, chupa za maji ya kunywa zilizotumika hatua ambayo imedhihirisha kuwapo binadamu waliokuwa wakikaa humo licha ya kwamba, kufika kwake ni kwa shida.
 
Wakazi wazungumza
Wakizungumza na waandishi, baadhi ya wakazi wa maeneo jirani na eneo hilo, walisema hawajaruhusiwa kufika eneo hilo kwa kuwa linaendelea kulindwa  na askari wa Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU)  kwa kushirikiana na JWTZ.
 
“Muda mfupi tu kabla ya ninyi kwenda huko, askari wa FFU walitoka huko , ninyi mnaelezwa kwamba pako shwari lakini sisi bado hatujaruhusiwa kufika kule kwa sababu panalindwa muda wote na askari… ,” alisema mkazi  aliyejitambulisha kwa jina moja la Mrisho.
 
Katika hatua nyingine, askari wa JWTZ aliyefariki wakati akitibiwa kwenye Hospitali ya Bombo baada ya kujeruhiwa kwenye mapigano hayo ya mwishoni mwa wiki,  mwili wake uliagwa jana mjini hapa kabla ya kusafirishwa kuelekea wilayani Korogwe kwa maziko yaliyofanyika katika kijiji cha Bungu.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname