10 February 2016

YONA, MRAMBA WANAFUNDISHA KULIKO BABU SEYANA LUQMAN MALOTO
MAMA yupo na mwanaye Hospitali ya Palestina, Sinza, Dar es Salaam. Amempeleka kupata matibabu. Mtoto anashangazwa na wingi wa watu, anamuuliza mama yake: “Kuna nini?”
Mama anamjibu mwanaye: “Kuna watu walikuwa vigogo wa nchi, walitumia vibaya madaraka yao walipokuwa viongozi wakubwa wa serikali, walihukumiwa na mahakama kwenda jela kwa kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
“Baada ya kuhukumiwa kwenda jela, baadaye walipata punguzo la adhabu mahakamani, walipewa kifungo cha nje pamoja na kufanya usafi kwenye maeneo ya kijamii, hapa hospitali ni moja ya sehemu walizopangiwa.”
Mtoto anatikisa kichwa kuonesha kuwa ameelewa, kisha anauliza tena: “Ndiyo wale akina babu walikuja na magari mazuri? Wanafagia kwa lazima na kupiga deki makorido ya hospitali, kwani nyumbani kwao hakuna wadada wa kazi? Si wangewachukua waje kufanya kazi kwa niaba yao?”
Mama anamjibu mwanaye: “Mwanangu hiyo ni adhabu ya mahakama, inatakiwa kutekelezwa na mwenye kosa. Hapo hairuhusiwi kutumia fedha kuleta watu wa kusafisha wala kuita ndugu wawasaidie, ni wao wenyewe.”
Mtoto anaendelea: “Kama ni hivyo basi ngoja na mimi nitapike hapa ili waje wafute ili waitumikie adhabu vizuri.”
Mama kwa hisia, anamwambia mwanaye: “Usifanye mzaha mwanangu, hili jambo siyo dogo. Hawa watu unaowaona ni matajiri, wana uwezo mkubwa lakini sheria imechukua mkondo wake. Wanalipa gharama za walichokifanya wakiwa ofisini.”
Katika kumuweka sawa mtoto wake, mama anasema: “Unaziona hizi pesa? Basi kwa taarifa yako, hao watu wawili kwa nyakati tofauti tumetumia noti zenye saini zao, unadhani ni wadogo hao?”
Mtoto sasa anashtuka, anauliza: “Kumbe wenyewe ndiyo huwa wanasaini hizi pesa tunazotumia?”
Mama anajibu: “Walikuwa wanasaini, siyo sasa. Walipishana wizara ya fedha wakati Rais Benjamin Mkapa alipokuwa madarakani, kabla ja Dk. Jakaya Kikwete na Dk. John Magufuli.”
Mara mtoto anapayuka: “Mama ona yule mzee anafagia anakosea.” Mama anamshika kinywa mwanaye aache kupayuka.
Mwaka 1997 mpaka 2000, Daniel Yona alikuwa waziri wa fedha na baada ya hapo alikuwa waziri wa nishati na madini. Kati ya mwaka 2000 mpaka 2005, Basil Mramba alikuwa waziri wa fedha. Ila sasa wapo kwenye adhabu ya usafi, nyakati zimebadilika.
Yona anageuka anamwangalia mtoto aliyepayuka, anakuta mama kamziba mdomo, anashindwa kusema kitu, ila inamuuma.
Mama anapomwachia mdomo mtoto, anapayuka tena: “Kwa hiyo na wale ni mafisadi? Si wamechezea fedha za serikali na kuitia hasara?”
Mtoto aliongea harakaharaka, mama alipotaka kumuwahi mdomo, alikuta ameshamaliza. Mama anaogopa, anaona hatari hiyo maana Mramba na Yona ni watu wakubwa! Nyakati tu zimebadilika!
Mramba anafagia, kuna mkazi wa Manzese mtukutu, yupo Hospitali ya Palestina anasubiri huduma. Alikuwa amekaa, mara anainua miguu kisha anamwita: “Mzee huoni uchafu huu, pitisha hapa ufagio sisi raia wema tukae kwenye maeneo masafi.”
Wakati anafagia, mtukutu wa Manzese anazungumza kwa ukauzu: “Si ulisema bora tule nyasi ndege ya rais inunuliwe? Lipia gharama za maneno yako.” Mramba anakumbuka maneno hayo aliyoyatamka bungeni katika Bunge la 8. Roho inauma, siku haziwezi kurudi nyuma! Na nyakati zimebadilika!
Yona akiwa anaendelea kufanya usafi, teja wa Kinondoni Manyanya ambaye yupo kliniki (rehab) akitumia dawa mbadala ya methadone, anampita Yona kisha anamwambia kwa sauti ya kebehi: “Mwana hii ndiyo ‘laifu’, ona sasa hivi umekuja kudeki matapishi ya wagonjwa hapa Palestina.”
Ni maneno ambayo yanamuuma Yona, anawatazama polisi kisha anatamani kuwaamrisha wamuweke ndani yule teja, ghafla anakumbuka, jeuri hiyo hana tena, na pale yeye ni mfungwa. Wale askari wapo kwa ajili kumsimamia anavyotekeleza adhabu. Anatikisa kichwa kwa uchungu! Nyakati zimebadilika!
Nyakati hizo alikuwa akitamka kuwaambia polisi “kamata”, ilikuwa hakuna kuhoji kwa kosa gani, maafande wanakubeba msobemsobe mpaka kituoni, hutoki wala hupelekwi mahakamani mpaka aamue! Ndiyo, si vigogo wengi walikuwa wakitumia nguvu hiyo kandamizi?
Kuna mama mmoja mzuri, msafi, anaonekana wa heshima. Anatembea kumwelekea Mramba. Anamfikia na kumsalimia vizuri kisha anatoa noti mbili za shilingi 10,000 na 5,000, zile pana, kabla ya hizi ‘vipotabo’ za sasa.
Anamwambia Mramba: “Samahani, hii saini kwenye hizi pesa ni kama yako hivi, au?”
Mramba kwa unyenyekevu anajibu: “Ni kweli hiyo ni saini yangu.”
Mama anajibu kisharishari tena kichokozi: “Utajibeba baba, toka kusaini pesa mpaka kusafisha vyoo vya hospitali, mbona unalo!”
Mramba anamuangalia kwa kumshangaa, alimuona ni mtu mwenye heshima zake, kumbe hovyo kabisa, mama mgomvi! La kumjibu anakosa, anatikisa kichwa. Anakumbuka enzi zake mwanamke yule hata asingepata nafasi ya kumkaribia. Ndiyo hivyo tena, nyakati zilishabadilika!
Yona anamtazama Mramba, anamuona kama mtu aliyetahayari. Anabaini atakuwa amekwazwa na yule mwanamke. Anamnyooshea ishara kuwa awe mvumilivu wasije kuharibu adhabu. Maana mahakama haishindwi kuagiza warudi gerezani kwa sababu nje ya gereza wanagombana na raia.
Wanaendelea na usafi, mara kuna mgonjwa anamuona Yona, anamwambia: “Baba nimekukumbuka, wewe si ndiye yule mwenye lile jengo la kifahari pale Bahari Beach? Mzee upo vizuri, mjengo wote ule wako peke yako. Hii nchi watu mnafaidi jamani.”
Yona anashindwa kujibu, anaamua kumpuuza na kuendelea na usafi, yule mgonjwa anaendelea: “Ila usijali mtu mzima, hii inaitwa mchana na usiku, giza na nuru. Nyumbani kwako una wafanyakazi kibao kwenye ule mjengo wako lakini hapa umekuja kutusafishia wodi zetu. Wajibika kiongozi, ndiyo maisha hayo na pande zake mbili za shilingi.”
Mzee anatumia hekima zake za kuzaliwa kuendelea kumpuuza. Yona anaendelea na kazi yake ya usafi.
Mwingine kafika na kupanga foleni ya kuingia kwa daktari. Mara anapaza sauti: “Mzee Mramba eeeh!”
Mramba anageuka kumtazama, yule mtu anapayuka: “Nilikuwa nadhani utani, kumbe mpo hapa mnafyekeshwa nyasi. Mimi siumwi wala nini, nilikuja tu hapa mara moja kuwashuhudia kwa macho yangu na kuwaambia kuwa haya ndiyo maisha. Wazee wa Ngwasuma waliimba Dunia Kigeugeu, yaani dunia imewageukia kiukweliukweli.”
Hili pia Mramba linamsikitisha, linamuondolea ujasiri wake. Anajiona mnyonge. Anajilaumu kwa nini aliomba kifungo cha nje, maana kule gerezani angekuwa hakutani na raia. Kifua kinajaa kwa hasira na uchungu. Anaangalia hadhi yake na kazi anazotumikishwa. Ila hana jinsi, nyakati zilishabadilika!
Najaribu tu kuvuta picha! Mramba na Yona kufanyishwa usafi siyo jambo dogo. Ni mambo ambayo kwa Tanzania na Bara la Afrika hatujapata kuyazoea.
Kwa wenzetu wenye kuheshimu utawala bora, mtu kuwa kigogo wa serikali leo kisha baadaye kutupwa jela kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka ni kitu cha kawaida kabisa.
Rod Blagojevich, alikuwa Gavana wa Illinois, Marekani. Mwaka 2009 aliondolewa kazini baada ya kupoteza sifa kutokana na kashfa za rushwa. Hivi sasa yupo jela!
Jesse Jackson ni mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu, na mtetezi wa Wamarekani weusi. Alifanya kazi kubwa mwaka 2008, alipomfanyia kampeni za nguvu Rais Baraka Obama na kumuwezesha kushinda urais, hivyo kuwa rais wa kwanza mweusi kuliongoza Taifa la Marekani.
Pamoja na mchango mkubwa wa Jesse, lakini mtoto wake, Jesse Jackson, Jr, hivi sasa yupo jela, kwa makosa ya rushwa akitumikia kifungo cha miaka miwili na nusu.
Jesse, Jr, kwa mwavuli wa baba yake alifanikiwa kuwa mwanasiasa anayechanua na akawa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, akiwakilisha Chama cha Democrats, Jimbo la Illinois 2nd District. Obama hajamkinga na jela!
William Jefferson alikuwa kigogo wa kisiasa nchini Marekani. Hivi sasa yupo jela, akitumia kifungo cha miaka 13 jela, baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Mwaka 2005 akiwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Jimbo la Louisiana 2nd District, alikutwa nyumbani kwake na dola 90,000, shilingi milioni 117 kwa ‘chenji’ ya wakati huo. Fedha hizo Jefferson, maarufu kama Bill Jefferson alikuwa amezificha kwenye friji.
Unaweza kujiuliza ni wangapi leo hii wanakaa nyumbani kwao na fedha nyingi kiasi hicho hapa nchini. Kuna wanaoishi nyumbani kwao na mabilioni ya shilingi bila wasiwasi wowote. Hii ndiyo Tanzania!
Marekani, mwanasiasa mkubwa alipokutwa na shilingi milioni 117 moto ulimuwakia. Umaarufu wake ulipungua, na tangu mwaka 2012 yupo anatumikia kifungo jela.
Hapa kwetu, yupo ambaye alibainika kuhifadhi shilingi bilioni moja Jersey, Uingereza, alipoulizwa, alijibu: “Hivyo vijisenti tu!” Hajawahi kufanywa chochote tangu mwaka 2008 alipobainika na alipojibu hivyo.
Yupo ambaye amekuwa akizungumzwa kuwa alifanya hamisho kubwa la fedha kwenye akaunti za nje, tangu mwaka jana kabla ya Uchaguzi Mkuu, mpaka leo hajawahi kuitwa hata mara moja kuulizwa, uhalali wa miamala aliyofanya.
Taarifa ya Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kisha kuthibitishwa na Bunge la 10, Novemba 2014, iliezwa kuwa ipo miamala ilihamishwa kwa magunia, masandarusi, lumbesa na viroba Benki ya Stanbic.
Magunia ya fedha, wapi yalipelekwa? Kama siyo kwenye nyumba za watu? Inaelezwa mgao ulikuwa shilingi bilioni 70. Je, hakuna waliokwenda kuficha kwenye uvungu wa vitanda vyao noti za mabilioni?
Nakumbusha, Jefferson aliponzwa na shilingi milioni 117 tu, hapa kwetu, watu na mabilioni yasiyo na maelezo wala hawachukuliwi hatua.
Andrew Theophanous alikuwa kigogo katika Baraza la Wawakilishi nchini Australia. Makosa ya rushwa yalimpeleka jela miaka sita, na maisha ya kisiasa yalikoma mwaka 2002 baada ya hukumu. Wenzetu wamezoea, sisi bado sana.
Inapozungumzwa hoja kuhusu Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ni kwa sababu suala lake lake la kashfa ya Tegeta Escrow halijafungwa.
Wapo watu wanajaribu kusema kuwa Muhongo alipojiuzulu ilitosha, kweli? Mtu ambaye ndiye kitovu cha wizi mkubwa kufanyika, zaidi ya shilingi bilioni 300, zikachotwa kihuni, eti siyo jambo zito hilo.
Inavyoonekana ni kwamba Jefferson angepata kashfa hiyo akiwa Tanzania, leo hii asingekuwa jela. Hata kuziona fedha hizo, nani angethubutu kwenda kumkagua? Blagojevich kwa Tanzania asingefungwa, tena angekuwa anaendelea kuula serikalini.
Wakati James Rugemalira anaendelea kudunda, ugawaji wake wa fedha, ni zaidi ya ule wa mtu wa kati (lobbyist), Jack Abramoff, aliyetikisa Serikali ya Marekani katika kashfa ya Jack Abramoff CNMI.
Bob Ney, akiwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Jimbo la Ohio, kwa Chama cha Republican, alibainika kupewa fedha na Abramoff, papo hapo ukaibuliwa uchunguzi wenye maswali mengi, wamepeana fedha za nini?
Hakukuwa na kitu zaidi ya rushwa! Abramoff na Ney, wote walihukumiwa kwenda jela, miezi 30. Yaani miaka miwili na nusu.
Sisi huku Rugemalira aligawa fedha kama njugu, watu hawahoji. Wengine wakasema ni za mboga.
Hivi karibuni, kuna maofisa wa serikali walishinda kesi mahakamani baada ya kuonekana mashtaka dhidi yao hayana kichwa wala miguu.
Yaani unampeleka mtu mahakamani kwa tuhuma za rushwa. Mashtaka yako yanasema alipewa rushwa na Lugemalira. Jaji, anauliza sasa mbona huyo mtoa rushwa hamjamleta hapa?
Rushwa hujumuisha mtoaji na mpokeaji. Kama ambavyo Abramoff na Ney walivyofungwa. Utani wa namna hii ni rahisi kupatikana Tanzania peke yake.
Hivyo, hapa kwetu bado hakujawa na mazoea ya kuwajibishana, ndiyo maana adhabu hii ya Mramba na Yona naona ina maana kubwa, pengine kuliko walivyokuwa wanaitumikia gerezani. Nitaeleza!
Lipo kundi kubwa linalalamika kuwa adhabu ni ndogo kuliko kosa. Wanahoji iweje mfungwa wa kuku afungwe miaka 10, aliyeisababishia serikali hasara ya mabilioni apewe kifungo cha nje? Ni haki yao kutoa maoni. Nchi huru hii!
Hata hivyo, wote wenye kutoa maoni hayo hawajui maana ya adhabu wanayoitumikia Mramba na Yona kwa sasa.
Watu hawaadhibiwi kwa lengo la kukomoana tu, bali pia kupitisha mafunzo kwa jamii ili itambue kuwa kuna malipo ya gharama baada ya kutenda makosa.
Mtoto aliyewaona Mramba na Yona, anapata picha kuwa kumbe nchi inaongozwa kwa sheria. Ukifanya makosa baadaye lazima utalipia gharama kwa mujibu wa sheria za nchi. Hii inafundisha zaidi.
Watu ambao wanalingana na babu yake, wanabebeshwa mafagio, chepe na ndoo za kupigia deki kwa ajili ya kufanikisha usafi, kisha anatambua wanasota kwa sababu walifanya makosa walipokuwa na nyadhifa zao serikalini.
Huwezi kuiona adhabu ya kufagia ya Yona na Mramba ni kali kama hufikirii nje ya sanduku. Hadhi zao, mamlaka waliyokuwa nayo! Maisha yao ya jela ni wangapi wangeyaona zaidi ya wafungwa wenzao?
Wanaposhiriki usafi kwenye maeneo ya jumuiya, wanafunzi wanaona, wanaingiza kitu kichwani kwamba siku wakipewa dhamana za kuongoza nchi, wanatakiwa kuwa waadilifu, kinyume chake ni kudhalilika kama taadhira wanayokutana nayo Mramba na Yona!
Inawezekana ikawa ni adhabu ndogo kwa macho, ila utaiona ni ngumu kama utavaa uhusika wa Mramba na Yona! Binadamu tumeumbwa na aibu. Mtu wa kawaida tu kutumikishwa kazi hawezi kuona sawa, itakuwa Yona na Mramba?
Fikiria japo kidogo tu, umekuwa kiongozi, ukilindwa, ukipanga bajeti za nchi, ukisaini mikataba mikubwa kati ya serikali na wawekezaji, kila waziri anakutazama wewe apate fungu, ni wewe ndiye unamiliki hazina, benki kuu ipo chini yao. Leo unakuwa msafisha vyoo hospitali!
Wakiwa jela wanakuwa tu simulizi. Fulani na fulani wamefungwa, lakini vifungo vyao havitoi fundisho kama kuwaona kwa macho.
Hata mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, adhabu yao haifundishi chochote. Watu wanasimuliana tu, yupo jela, picha hutoa elimu kubwa kuliko simulizi.
Binafsi naona adhabu hii ya Mramba na Yona ina faida kubwa kwa jamii kuliko walipokuwa jela. Watu wengi watakuwa wakiwaona na kuelimika kuhusu umuhimu wa uadilifu. Kesi ya Babu Seya na Papii, ni ya kihistoria lakini haifundishi jamii. Watu hawawaoni, hawanyooshewi vidole. Mramba na Yona kwa sasa wananyooshewa vidole.
Ndimi Luqman Maloto

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname