09 February 2016

Ulimwengu aendeleza moto wa mabao TP Mazembe ikiua 5-0

Thomas Ulimwengu ( Picha ya hisani Getty Image)
Thomas Ulimwengu ( Picha ya hisani Getty Image)
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya TP Mazembe, Thomas Ulimwengu ameendelea kung’ara katika klabu yake baada ya kufunga na kupika bao katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Lubumbashi Sport.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo, Ulimwengu alikuwa mpishi wa bao la kwanza lililowekwa kimiani na mshambuliaji kutoka Ivory Coast Roger Assale mnamo dakika ya 16.
Assale alirudisha mkono wa shukrani kwa kumtengenezea Ulimwengu bao la pili kwa mabingwa hao wa Afrika katika dakika ya 23.
TP Mazembe ilipata pigo kipindi cha pili baada ya Ulimwengu kushindwa kuendelea na mchezo na kutolewa nje kutokana na majeruhi. Nafasi yake ilichukuliwa na nyota wa Zambia, Rainford Kalaba dakika ya 63.
Mabao mawili ya haraka haraka kutoka kwa Luyindama na Adama Traore mnamo dakika ya 75 na 76 yalihakikishia TP Mazembe ushindi.
Kalaba alifunga bao la tano dakika sita kabla ya muda wa kawaida kutimia na kuifanya TP Mazembe kuondoka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya mahasimu wao wa jiji la Lubumbashi.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname