Dar/Arusha. Siku moja
baada ya kifo cha rubani Rodgers Gower (37) aliyekuwa anaendesha
helikopta inayomilikiwa na Mwiba Holdings, baadhi vyombo vya habari vya
kimataifa vimeripoti kuwa huenda bunduki iliyomuua ni ile iliyokuwa
inatumika kuulia tembo.
Miongoni mwa vyombo
hivyo ni magazeti ya Uingereza ya Daily Mail, The Guardian, The Sun, The
Telegram, The Independent, Shirika la Habari la Ufaransa AFP na Shirika
la Utangazaji la Marekani CNN.
Mbali na vyombo hivyo,
jana asubuhi mwili huo ulifanyiwa uchunguzi ambao ulionyesha matundu
manne ya risasi, moja kwenye mguu, mawili begani na jingine kwenye paji
la uso ambako risasi iliingilia kichwani na haikuwa imetoka.
Chanzo cha habari katika
Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, ulikopelekwa mwili huo
kilisema walipewa maagizo kuhakikisha hauondolewi hadi risasi iliyopo
kichwani imeondolewa.
“Unajua huyu aliyefariki
ni Mzungu, hata kama amefanyiwa postmoterm hapa anaweza kufanyiwa
nyingine Aga Khan, Dar es Salaam na akifikishwa kwao Uingereza
anafanyiwa tena, ndivyo walivyo wenzetu,” alisema.
Ijumaa iliyopita, Gower
aliuawa kwa risasi wakati akiendesha helikopta hiyo kwenye doria dhidi
ya majangili katika pori la Akiba la Maswa, mkoani Simiyu akiwa pamoja
na raia wa Afrika Kusini, Nicky Bester ambaye alinusurika kifo.
Serikali kupitia Waziri
wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe imesema inaendelea na
uchunguzi ili kuwabaini majangili waliohusika.
Alivyouawa
Daily Mail lilisema jana
kuwa inawezekana hata bunduki iliyomuua Gower ni ile waliyokuwa
wanatumia majangili hao kuua tembo. Lilieleza kuwa wakati Gower akiwa
katika doria, aliona mabaki ya tembo wawili chini.
Gazeti hilo lilimnukuu
Pratik Patel, mmoja wa marafiki wa karibu marehemu, akisema wakati
anaendelea na doria aliona tembo mwingine ambaye hakuwa ameuawa muda
mrefu.
“Baada ya kuona hivyo,
akataka ageuze ili wakamwangalie yule tembo, huku akijaribu kuona kama
kuna majangili, ndipo mwanamume mmoja alitokea akiwa na bunduki na
kupiga kwenye uvungu wa helikopta,” alisema Patel ambaye pia ni
mfanyakazi mwenzake.
“Ile risasi ilitoboa
uvungu wa helikopta na kupenya ndani, ikampiga rubani kwenye mguu na
sehemu ya bega na uso kisha kutoboa paa la helikopta na kutoka nje
…kutokana na uzito wa silaha iliyotumika kumuua, pengine ndiyo ileile
ambayo majangili walitumia kuua tembo.”
Lakini gazeti la The Telegram, lilieleza kuwa bunduki iliyotumika kumuua Gower ni AK47.
“Alipokuwa anamkaribia
tembo mmoja aliyeuawa, ndipo akapigwa risasi na kufariki kabla ya timu
ya waokoaji kufika katika eneo hilo,” ilisema sehemu ya habari hiyo.
Mwanzilishi wa Mfuko wa
Hifadhi wa Friedkin (FCF) aliyetoa taarifa kwa vyombo vya habari, Dan
Friedkin ambaye aliwahi kufanya kazi na Gower alisema ni jambo la
kusikitisha kuona rubani huyo, aliyekuwa katika operesheni ya kusaidia
Tanzania kupambana na majangili ameuawa na haohao majangili.
The Guardian liliripoti
kuwa jukumu kubwa la marehemu ambaye pia alikuwa mhasibu kitaaluma,
lilikuwa kusafirisha watalii kwenye kambi mbalimbali za hifadhi.
Gower ambaye pia
alihitimu masomo ya urubani wa helikopta mwaka 2004 London, Uingereza
amekuwa akifanya doria kwa kushirikiana na wahifadhi kwa ajili ya
kupambana na majangili kwenye hifadhi.
Akizungumzia mipango ya mazishi, Patel alisema jana kuwa suala hilo bado linajadiliwa na familia ya marehemu.
Hata hivyo, taarifa nyingine zilieleza kuwa mwili huo unatarajiwa kusafirishwa kwenda Uingereza kwa mazishi.
Chanzo cha kuaminika
katika Mount Meru kilisema muda mfupi baada ya mwili huo kufikishwa,
wakala wa kusafirisha miili ya raia wa kigeni alifika na kuzungumza na
baadhi ya wafanyakazi wa Mwiba Holdings, iliyokuwa inamiliki helikopta
hiyo.
No comments:
Post a Comment