11 February 2016

CHUO CHA GE OIL & GAS CHASAIDIA KUTOA ELIMU KWA WAHANDISI WA KITANZANIA NCHINI ITALIA




Wahandisi watatu wamekamilisha na kupongeza mafunzo maalum waliyopata katika kipindi cha miezi 4 kutoka chuo kikuu cha GE Oil & Gas huko Florence, nchini Italia.
Mafunzo hayo yalifanyika chini ya udhamini wa shirika la General Electric (G.E), linaloongoza katika sekta ya viwanda vya uzalishaji kwa njia za kidijitali, kwa kupitia kitengo chao cha mafuta na gesi.
Walionufaika na mafunzo haya ni Bw. Fabian Mwose (Mhandisi wa mafuta), Bi. Lilian Zambi (Mhandisi wa kemikali na michakato) pamoja na Bi. Limi Lagu (Mhandisi wa kemikali na michakato) wote kutoka shirika la maendeleo ya mafuta Tanzania (TPDC)
Taarifa rasmi kwa vyombo vya habari iliyotumwa na GE Oil & Gas wiki hii ilisema kuwa wahandisi hao watatu walijiunga na washiriki wengine kutoka mataifa mbalimbali kwa kipindi cha muda wa miezi 4. Mafunzo yaliyotolewa yanatoa mbinu kamili ili kuendeleza elimu na kozi zinazotolewa zinajikita katika maeneo manne ya Uongozi, Nishati, Michakato ya mafuta na gesi na Mashine za mafuta na gesi, ambazo ni kozi zaidi ya 40, zinazodumu kwa takriban miezi minne.
Chuo cha GE Oil & Gas kilifungua milango yake rasmi mnamo mwaka 2006 na kuanza kusaidia wanaofanya kazi katika sekta ya mafuta na gesi kutoka pande zote za dunia kupata nafasi ya mafunzo juu ya masuala ya menejimenti pamoja na kukuza ujuzi wao wa kiufundi na hivyo kujidhatiti vizuri zaidi katika sekta ya mafuta na gesi. Chuo kinatoa kozi zinazotambulika kwa mashirika yanayoongoza katika sekta ya mafuta na gesi kote duniani, ambao kila mwaka hupeleka wafanyakazi wao chuoni hapo kupata mafunzo.
Mpaka kufikia mwaka huu, chuo hicho kimepokea wafanyakazi kutoka kampuni zisizopungua 87 kutoka ndani na nje ya Italia. Chuo pia kimefanikiwa kushuhudia wahitimu 507 kutoka nchi 30, ambapo 212 ni waliofanya kozi za nchini Italia na 295 zikiwa kozi maalum kulingana na nchi walizotokea.
Wakizungumzia juu ya mafunzo hayo wahandisi hao walisema wamefurahia mafunzo waliyopata chuoni hapo kwani ni ya kisasa na yamesaidia kuwaboresha kiufundi. Walisema mafunzo hayo yamesaidia kuongeza thamani katika maarifa yao na yatasaidia kuongeza ufanisi wao kazini kwa ujumla.
“Tunaamini kuwa mafunzo haya yatalisaidia Shirika zima la maendeleo ya mafuta Tanzania (TPDC) na taifa kwa ujumla katika kujenga kundi la wafanyakazi wenye ufanisi na uwezo mkubwa katika sekta hii” walisema kwa pamoja.
Kwa upande wake Bi. Limi Lagu alisema ; “Kozi iliyokuwa na manufaa sana kwangu mimi ilikuwa kozi ya michakato ya kutumia na kuendesha mashine na vifaa, ambapo ilinibidi nijifunze kwa undani zaidi teknolojia ya kila kifaa na mashine inayotumika katika upatikanaji na uuzaji wa mafuta na gesi, kuanzia uchimbaji hadi matumizi.”
Bi. Limi alizungumzia pia suala la wataalamu wa mafuta na gesi nchini Tanzania na kuwaomba wadau wa sekta hii pamoja na serikali kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanapata nafasi ya kupitia mafunzo  haya ili kuhakikisha taifa linakuwa na wataalamu wa kutosha kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya mafuta na gesi nchini.
Naye Bw. Fabian Mwose aliongeza kuwa kwa upande wake kozi iliyokuwa na manufaa zaidi ilikuwa ni ziara nzima ya kiwanda cha mafuta na gesi na kusema kuwa kozi hiyo ilijumuisha karibia kila kipengele cha mzunguko wa mafuta na gesi na hivyo kumpatia picha kubwa ya sekta nzima ya mafuta na gesi kwa upana zaidi.
Taarifa hiyo ilisema kuwa GE Oil & Gas imeahidi kuendelea kuchangia kuboresha ujuzi wa wafanyakazi kutoka upande wa wateja wao pamoja na washirika wao, yote hii ili kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi nchini.
“Tunatazamia kuboresha ushirikiano wetu na Tanzania, lengo kuu likiwa ni kutoa mafunzo zaidi kwa wananchi ili kupata wahandisi wenye uwezo mzuri katika sekta hii”
Ikiwa ni sehemu ya kuboresha ushirikiano na Tanzania, GE Oil & Gas ilialika wadau kadhaa katika mkutano wake mkuu wa 16 wa kila mwaka uliofanyika jijini Florence, nchini Italia. Mkutano huo uliofanyika Februari mwaka 2015, na kuwakutanisha kwa pamoja wadau wakubwa wa sekta ya mafuta na gesi kutoka pande zote za dunia huku Mhe. George Simbachawene, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Tanzania pamoja na Dk. James Mataragio, Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, wakialikwa kama wageni wa kuhutubia.
Katika hafla hiyo, waliwashirikisha wasikilizaji katika fursa na changamoto zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi nchini Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya petroli Tanzania (TPDC), pia alihudhuria katika ufunguzi wa sherehe hizo za chuo cha GE Oil & Gas mwaka jana
General Electric ilizinduliwa mwaka 1892 na inaongoza duniani kwa sekta ya viwanda kidigitali, ikiibadili sekta hiyo kwa mashine zinazoendeshwa na programu na suluhu zinazounganisha, zinazoonesha majibu na uingizaji.
GE Oil & Gas ndio shirika linaloongoza duniani kwa huduma na teknolojia ya vifaa vya mafuta na gesi, kuanzia shughuli za uchunguzi hadi za uchimbaji na matumizi ya mafuta na gesi.
General Electric imedhamiria kuunga mkono juhudi za kupata maendeleo yenye kuboresha hali nchini kwa kutumia teknolojia ya miundombinu, huduma na ufumbuzi. Tawi hili lilianza shughuli zake nchini mnamo mwaka 2013 na kupitia mradi wake wa umeme na maji, wamekuwa wakitoa vifaa muhimu katika uzalishaji wa umeme hii ikiwa ni pamoja na miradi ya Kinyerezi 1, Songas 1, 2 & 3, Symbion Ubungo na Tanesco Ubungo, inayochangia takriban asilimia 60 ya umeme unaosambazwa Tanzania.
GE Oil & Gas ilianza operesheni zaidi ya miaka 100 iliyopita katika nchi za kusini mwa sahara. Hata hivyo mwaka 2011, GE Oil & Gas ilivumbua njia mpya za kufikia malengo yao ya sasa na ya baadae barani Afrika. Hivi sasa GE Oil & Gas inatambulika kwa kuwa na wafanyakazi 2,350, mapato zaidi ya bilioni 3.2 ya dola za kimarekani na operesheni katika nchi 25.
Operesheni kuu za GE Oil &Gas  kusini mwa Sahara zipo Nigeria, Afrika Kusini, Angola, Ghana, Msumbiji na Kenya ambapo ndipo yalipo makao makuu. GE Oil & Gas inasonga mbele, ikitoa huduma ya umeme na kuponya bara kwa kutumia njia za kisasa na endelevu ambazo zimelenga kufikia kipekee mahitaji ya kila nchi wanayohudumia ndani ya kanda na katika biashara tofauti-anga, afya, mafuta na gesi, umeme na maji na usafiri/uchukuzi.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname