09 January 2016

TFF YAWADHALILISHA WAZAZI WA SAMATA KATIKA MAPOKEZI YA MWANAO.....WAKAA KWENYE NGAZI WAKIMSUBIRI MWANAO

www.liboman.com
 
Na Saleh Ally
Umenisikia au kunisoma mara nyingi kuliko nikililia heshima ya soka na michezo mingine katika nchi yetu.

Kama ni mpenda soka, unajua ninavyolia na viongozi wa michezo na hasa soka walivyojazana kwenye uongozi wa klabu, vyama, mashirikisho kwa ajili ya matumbo yao.

Najua nawaudhi sana, lakini siwezi kuacha kwa kuwa ukweli ndivyo ulivyo na utaendelea kujionyesha.

Mfano mzuri ni picha hii inayomuonyesha mzazi wa mwanasoka maarufu zaidi nchini Mbwana Samatta akiwa amekaa kwenye ngazi za uwanja wa ndege kumsubiri mwanaye awasili.

Ally Samatta alikuwa na furaha ya mwanaye kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa wanaocheza Afrika. Aliwasili saa nane usiku, lakini mzee alikuwa pale.

Kila mmoja anajua juhudi binafsi za mzee huyo kumsaidia mwanaye kufikia hapo alipo. Wengi tumemjua baada yam zee huyo na familia yake kupambana tokea mwanzo, mimi ninaamini anastahili heshima kubwa ya mzazi na mlezi bora kabisa.
Hakuna kiongozi wa Fat, TFF, Simba au kwingine aliyewahi kumsaidia wakati akipambana kwa ajili ya Mbwana.

Ameleta heshima kubwa kwa taifa kupitia mwanaye, lakini leo anafikia kwenye ngazi ambazo nadiriki kusema alikaa chini uwanja wa ndege.
Hoja yangu iko hivi, kweli Mzee Samatta hasitahili kutumia sehemu ya VIP ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere? 
Nauliza tena, unawajua wangapi waliorejea nchini na kuitumia sehemu hiyo wakiwa hawana kubwa walilotoa kwa ajili ya taifa letu. Kungekuwa na ubaya gani Mzee Samatta angekaa kule wakati akimsubiri mwanaye, halafu wangeungana na watu wengine wakati akitoka nje?

Mara ya mwisho, niliona wakienda kumpokea Kocha Mart Nooij upande wa VIP ambao waliomba ili afikie wakati anawasili. Vipi Baba Samatta na familia yake waonekane hawafai na kwenda kukaa chini?

Hata kama wanatokea Uswahilini kwetu, lakini heshima yao wanastahili kupewa. Viongozi wa TFF wanaonekana hawajali, waliona ni jambo la kawaida tu.www.liboman.comNOOIJ ALIPOKELEWA VIP, HAKUWA AMEIFANYIA LOLOTE TANZANIA NA ALIONDOKA BILA YA KUFANYA LOLOTE. HAPA AKIWA NA VIONGOZI WA TFF WALIOFANYA MIPANGO AFIKIE HUKO.
 
Ninawakumbusha, hili ni kati ya mambo zaidi ya mia ninayoonyesha uozo, upuuzi, ubabaishaji na mambo ya hovyo kwenye mpira wetu.

Kama inashindikana uandaaji wa hili la kishujaa la Samatta, nani anasema tunaweza kufanya maandalizi bora ya ukuzaji wa vijana yanayohitaji miaka na uvumilivu wa juu?

TFF hawawezi kulikwepa hili, najua watasema hatukujua lolote, lakini lingekuwa suala linahusisha fedha, wangekuambia sisi ndiyo wasimamizi wa mpira.

Sasa suala la Samatta wakati wa mapokezi yalihusiana na riadha, netiboli au ngumi za kulipwa? Wao walikuwa wapi?

Halafu siku chache, utasikia TFF wameandaa hafla na kumwalika Mzee Samatta na familia yake eti kwa heshima. 

Kama hilo limeshindikana, nani anaweza kusema eti kwa viongozi hawa, tunaweza kuwa na ligi bora kabisa yenye ushindani na muonekano bora wakati inahitaji maandalizi ya juu kabisa?


Nitaendelea kusema tu, watakaoelewa nitakuwa nao, wasioelewa, nitaendelea tu… 
Chanzo: saleh jembe

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname