02 November 2015

VIGOGO WASHINDA KWA WAGANGA ....ILI WATEULIWE KUWA MAWAZIRI ..TAZAMA HII KATUNI

NUSU ya Mawaziri wa
Serikali ya awamu nne
waliokuwa kwenye Baraza
la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete,
wamo hatarini kukosa nafasi ya
kuchaguliwa kwenye baraza jipya
la mawaziri wa Serikali ya awamu
ya tano chini ya Rais Dk.John
Magufuli.
Dk.Magufuli ambaye ameibuka
mshindi kwenye uchaguzi mkuu
uliofanyika Oktoba 25, mwaka
huu, anatarajia kuapishwa katikati
ya wiki hii ili kuanza kazi ya
kuwatumikia Watanzania katika
kuleta maendeleo na kutatua
changamoto mbalimbali ambazo
zinawakabili kwa muda mrefu.
Wakati Dk.Magufuli akijiandaa
kuapishwa ili kuanza kazi, moja
ya mambo ambayo yanamuumiza
kichwa kwa sasa baada ya
kutangazwa kuwa, ndiye mshindi,
itakuwa ni kwenye kuunda
baraza lake la mawaziri ambalo
Watanzania wanasubiri kwa hamu
kuona majina gani mapya yataingia
na majina gani yatatoka kulingana
na mahitaji yake.
Pamoja na hayo, tayari mawaziri
waliopo kwenye Serikali ya awamu
ya nne wameanza kuingia hofu ya
kuona kabisa hawana nafasi kwenye
baraza la mawaziri la Dk.Magufuli.
Zipo sababu nyingi ambazo baadhi
ya mawaziri waliopo sasa kuona
nafasi yao ni ndogo, ikiwemo ya kasi
ambayo Serikali ya awamu ya tano
itakwenda nayo ili kuwaridhisha
Watanzania.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa
masuala ya siasa nchini wamekuwa
na maoni mbalimbali na kutabiri
baraza la mawaziri ambalo
Dk.Magufuli, anatakiwa kufanya
nalo kazi, huku wengi wakiamini
kuwa, kwa namna ambayo rais huyo
mpya alivyo, kuna mawaziri wenye
majina makubwa hawatakuwepo.
Wachambuzi hao waliliambia
gazeti hili kwa nyakati tofauti
kuwa, Dk.Magufuli ni mkali hasa
pale anapoona jambo ambalo
analisimamia haliendi vizuri na
kwa kuwa, amekuwamo kwenye
baraza la mawaziri wa Serikali ya
awamu ya nne, atakuwa akiwajua
vizuri mawaziri waliopo sasa na
hiyo itampa nafasi ya kuamua nani
awe kwenye baraza lake na nani
amuweke kando.
Kwa upande wake mchambuzi
wa masuala ya kisiasa nchini,
ambaye pia ni Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Dk.Benson Bana alisema kuwa,
anatambua ugumu wa rais kuunda
baraza la mawaziri, lakini ana
matumaini na Dk.Magufuli kuwa,
kabla ya kutangaza baraza lake la
mawaziri atashauriana na Waziri
Mkuu wake ambaye atamteua hivi
karibuni.
Alisema kuwa, kiasili
Dk.Magufuli ni kiongozi mwenye
kasi ya utendaji na mfuatiliaji wa
mambo, hivyo baraza ambalo
anatakiwa kuliteua ni lile ambalo
litakwenda na kasi yake na wakati
huo huo, kufanya maamuzi yenye
tija kwa taifa, huku akielezea
baadhi ya mawaziri waliokuwamo
kwenye Serikali ya awamu ya nne
ataweza kuwachukua kutokana
na uwezo waliouonesha kwenye
baraza la sasa.
Dk.Banna alisema wapo
mawaziri wazuri ambao ataweza
kuwachukua kwa ajili ya kumsaidia
kwenye Serikali yake, huku akitoa
angalizo wale mawaziri ambao
wamekuwa wakilalamikiwa na
Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Abdulrahman
Kinana, ni vema wakawekwa kando
na kuingizwa sura mpya kwa ajili
ya kuleta ufanisi kwenye Serikali ya
awamu ya tano.
“Nimekuwa nikimfuatili
Dk.Magufuli kwa muda mrefu
kabla ya kuomba nafasi ya kuwania
urais, nieleze tu, Dk.Magufuli ni
mchapakazi na wote tunafahamu.
Kwa mazingira ya aina hiyo
tunasubiri kuona baraza lake
linakuwa na watu wenye maamuzi
kwa maslahi ya nchi yetu, baraza
la mawaziri ambao watafanya kazi
usiku na mchana kwa maslahi ya
taifa letu.
“Lakini kwa kutumia busara
zake, naamini atashauriana na
Waziri Mkuu wake, nani awe
wizara gani ili kufikia malengo yake
na kutekeleza ahadi ambazo alizitoa
wakati wa kampeni alipokuwa
akiomba kura,” alisema.
Pamoja na kuteua baadhi ya
mawaziri waliopo sasa, lakini
anatakiwa kuwa makini kwa
kuhakikisha anachukuwa wale
ambao wakipewa majukumu ya
kusimamia wizara, wanaweza
na wakati huo huo anaweza
kuwachukua baadhi ya watendaji
ambao si wanasiasa, lakini
akiwateua kuwapa ubunge na kisha
kuwapa wizara wamsaidie.
Dk.Banna alisema iwapo
angepata nafasi ya kumshauri
Dk.Magufuli kuhusu baraza lake
la mawaziri, angempa baadhi ya
majina ya mawaziri waliopo sasa
ambao wameonesha uwezo wao wa
kufanya kazi akiwamo Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi.
Alisema Waziri Lukuvi
ameonesha uwezo mkubwa wa
kusimamia majukumu yake katika
wizara zote alizopita, ikiwemo
aliyo nayo hivi sasa, kabla baraza la
mawaziri halijavunjwa.
Alisema Lukuvi ametatua
migogoro mingi ya ardhi maeneo
mbalimbali nchini na kwamba,
akipewa nafasi kwenye baraza la
mawaziri katika Serikali ya awamu
ya tano, atasaidia. Hata hivyo,
alisema Lukuvi pia ni mzoefu
kwenye Serikali zilizopita na hivyo
atakwenda na kasi ya Dk.Magufuli.
Pia, alisema Waziri wa Ulinzi,
Dk.Hussein Mwinyi, naye
anastahili kurudi kwenye baraza
la mawaziri katika Serikali ya
awamu ya tano kwa kueleza kuwa,
kila wizara aliyopewa kuiongoza,
alionesha uwezo mkubwa na hivyo,
anastahili kuwepo kwenye Serikali
ya awamu ya tano.
Dk.Banna alisema kuwa, anaona
nafasi ya Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Angella Kairuki, kwa madai
kwamba, alionesha uwezo mkubwa
kwenye nafasi ambazo alipewa
kwenye Serikali ya awamu ya nne,
lakini pia akiwa kwenye Bunge la
Katiba. Hivyo, anatamani kuona
akipewa nafasi kwenye Serikali ya
Magufuli.
Aliongeza kuwa, Profesa Sospeter
Muhongo naye ana nafasi kubwa
kwenye baraza la mawaziri katika
Serikali ya Magufuli na kueleza
kuwa, sababu zipo nyingi, lakini
kubwa akiwa Waziri wa Nishati na
Madini alionesha namna ambavyo
anaweza kusimamia watendaji
wa Serikali kutimiza wajibu wao,
pia alikuwa na maamuzi yenye
tija na kusimamia kwenye kile
anachokiamini.
Kwa upande mwingine, alisema
anaona haja kwa Dk.Magufuli
kuingiza damu mpya kwenye
baraza lake la mawaziri ambao
kimsingi ni wale ambao kwa rekodi
zao wanaweza kufanya kazi ambayo
yeye ataitarajia kuifanya katika
kuwatumikia Watanzania, ikiwa
pamoja na kutanguliza uzalendo na
uadilifu.
Alisema kuna wanasiasa wengi
waliopata nafasi ya kuwa wabunge
na hao wanaweza kuingia kwenye
baraza hilo na hata wasipokuwa
mawaziri kamili, anaweza
kuwateua kuwa manaibu waziri
kwa kuangalia sifa zao na si
kuteua kwa urafiki, bahati nzuri
Dk.Magufuli hana urafiki zaidi ya
kuteua kwa sifa za utumishi.
Pia, alisema wamo makatibu
wakuu wastaafu ambao ni wazuri
kwenye utendaji kazi, hivyo
alishauri Dk.Magufuli kuangalia
kama anaweza kuwatumia kwenye
Serikali yake, akimtolea mfano
Patrick Rutabanzibwa, Fanuel
Lyimo na Vincent Mrisho, ambao
waliwahi kuwa makatibu wakuu
kwenye Serikali zilizopita na
waliacha historia ya utendaji
uliotukuka.
Wachambuzi wengine wa
masuala ya siasa nchini, walisema
Dk.Magufuli kwa sasa anakuna
kichwa kuhakikisha anapata
baraza la mawaziri ambalo
litafanya kazi usiku na mchana
kuwatumikia Watanzania. Hata
hivyo, walitaja baadhi ya mawaziri
ambao wanaamini wana nafasi ya
kuteuliwa tena na rais wa awamu
ya tano.
Kwa mujibu wa wachambuzi hao,
walitoa baadhi ya majina ambayo
wanaona yanaweza kupenya
kwenye baraza hilo, ambao ni
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba, Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu, Waziri
Dk.Mary Nagu, Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya Salum na Mbunge
wa Ulanga Mashariki, Dk.Hajji
Mponda.
Wengine waoatajwa kuwamo
kwenye baraza la mawaziri
katika Serikali ya Dk.Magufuli
ni Waziri wa Afrika Mashariki,
Dk.Harson Mwakyembe, Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, January Makamba
na Janeth Mbene ambaye aliwahi
kuwa, Naibu Waziri wa Fedha.
Wachambuzi hao pia walisema
Dk.Magufuli anayo nafasi ya kuteua
baadhi ya watu kutoka makundi
maalumu, ambapo walitumia nafasi
hiyo kumpendekeza aliyekuwa
mjumbe wa Bunge la Katiba, Amon
Mpanju, ambaye alionesha uwezo
mkubwa wa kuelezea mambo yenye
maslahi mapana kwa nchi.
Pamoja na yote hayo, bado
inaelezwa kuwa, kuunda baraza
la mawaziri hasa kipindi hiki
ambacho Watanzania wanafahamu
haki zao na wajibu wa Serikali
katika kuwatumikia, Dk.Magufuli
anatakiwa kuumiza kichwa
kupata safu makini ambayo
haitamwangusha na kurejesha
matumaini ya Serikali kwa
wananchi.
Wakati hayo yakiendelea,
Dk.Magufuli mara kadhaa
amekuwa akieleza wazi kuwa,
mawaziri ambao atawateua,
kabla ya kuwaapisha ataingia nao
makubaliano na ambaye hataweza
ni bora akasema mapema kabla ya
kumwapisha.
Dk.Magufuli amekuwa akielezea
namna ambavyo hatakuwa na
mchezo na mawaziri ambao
atawateua, lazima wafanye
kazi usiku na mchana katika
kuwatumikia Watanzania na wale
ambao wamekuwa wakifanya kazi
kwa mazoea, kwake hawana nafasi.
Pia, akiwa kwenye mikutano
yake ya kampeni, Dk.Magufuli
hakusita kueleza kuwa, hataki
kuwa na baraza la mawaziri lenye
watu wengi, hivyo ataunda baraza
la mawaziri wachache, ambalo
litafanya kazi kubwa ya kiutumishi,
ikiwa pamoja kumtanguliza
Mungu.
“Hao mawaziri ambao nitawateua
wajiandae maana nataka tufanye
kazi usiku na mchana. Nataka
mawaziri ambao watawajibika
kwa wananchi bila kuchoka.
Hivyo, kabla ya kumuapisha huyo
nitakayemteua, lazima niingia naye
makubaliano na asaini.
“Kama hawezi ni bora aseme
mapema, lakini akikubali
kuapishwa ajue anatakiwa
kufanya kazi,” alikuwa akieleza
Dk.Magufuli kwa nyakati tofauti,
wakati akiomba kura kwa
Watanzania na sasa amefanikiwa
kushinda urais, kazi iliyopo mbele
yake ni kutimiza ahadi yake kuteua
mawaziri watakaofanya kazi.
Pamoja na hayo, ni wazi kuna
kundi kubwa la mawaziri waliopo
kwenye Serikali ya awamu ya tatu
na ya nne hawatakuwepo kwenye
Serikali ya awamu ya tano, kwani
baadhi yao walianguka kwenye
kinyang’anyiro cha kuomba ridhaa
ya ubunge kwenye majimbo yao
na hivyo, labda kama Dk.Magufuli
ataamua kuwateua na kisha kuwapa
wizara.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname