TAIFA liko katika mkao wa kusubiri kuapishwa kwa Rais Mteule wa Awamu ya
Tano, Dk. John Pombe Magufuli ambaye Alhamisi iliyopita alitangazwa
kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha urais dhidi ya wenzake saba lakini
tayari Wabongo wanaumiza vichwa kuhusu Baraza Jipya la Mawaziri la
Magufuli.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (Nec), ilimtangaza Dk. Magufuli kuwa
mshindi mbele ya wagombea wengine ambao ni Anna Elisha Mghwira
(ACT-Wazalendo), Hashim Rungwe Spunda (Chaumma), John Pombe Magufuli
(CCM) na Edward Nyoyai Lowassa (Chadema akiungwa mkono na Umoja wa
Katiba ya Wananchi, Ukawa ambao ni Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD).
Wengine ni Macmillan Lyimo Elifatio (TLP), Chief Lutasola Yemba (ADC),
Malick Jankin Kasambala (NRA) na Fahim Dovutwa Nassoro (UPDP).
WIKIENDA LAINGIA MTAANI
Mwishoni mwa wiki iliyopita, gazeti hili lilizunguka katika Jiji la Dar
kwa lengo la kuzungumza na wasomaji wake kuhusu mitazamo yao ya wana-CCM
waliopata nafasi ya ubunge ambao wanaweza kuitwa kwenye baraza la
mawaziri la Dk. Magufuli ambaye ataapishwa Alhamisi wiki hii.
Kila msomaji alikuwa na mawazo yake, lakini wengi mawazo yao yaliangukia
sehemu moja kwa kuzingatia mikoa, kanda na imani za kidini na hivyo
kutoa picha ya baraza hilo.
“Kwanza kabisa ijulikane kwamba, Magufuli hataweza kufanya kazi na
mawaziri wazembe. Yeye ni mchapa kazi, lazima atachagua wenye uwezo
lakini pia uteuzi wake lazima ataangalia haki, kila mkoa atatoa waziri,
pia ataangalia kanda na kubalansi dini.
“Hii inanipa picha kwamba, pia anaweza kuwateua wabunge kupitia zile
nafasi zake kumi kama ataona kuna mtu anamtaka afanye naye kazi lakini
hakuupata ubunge. Si unajua katiba inasema ili uwe waziri lazima uwe
mbunge,” alisema msomaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Fime, mkazi
wa Mwananyama A,
WAZIRI MKUU
Kwa mujibu wa wasomaji hao, nafasi ya uwaziri mkuu wengi wameipeleka kwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Vangimembe
Lukuvi (Mkoa wa Iringa).
“Huyu bwana ni mwenye subira, mstahimilivu, mvumilivu na mtulivu lakini
pia ni mchapa kazi. Tumeona alivyoinyoosha wizara yake ya ardhi. Hata
alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar, alifanya vizuri. Anaweza kumsaidia rais
katika ubora wake,” alisema msomaji mwingine akisema anaitwa Bakar Omar,
mkazi wa Tabata Matumbi.
NISHATI NA MADINI
“Mimi naamini Wizara ya Nishati na Madini atarudishwa Sospeter Augustino
Muhongo (Mkoa wa Mara). Huyu alijiuzulu uwaziri kwa kashfa ya Akaunti
ya Tegeta Escrow, lakini baadaye alisafishwa kwamba hakuhusika. Akiwa
kwenye wizara ile aliiweza kwa kipindi kifupi tuliona mabadiliko.
Msaidizi wake awe Charles Mwijage (Mkoa wa Kagera),” alisema mama
Mapunda, mkazi wa Kigogo Luhanga.
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
“Mimi mawazo yangu lazima Magufuli atamrejesha Benard Kamilius Membe
(Mkoa wa Lindi) au atamuweka mama Asha-rose Mtengeti Migiro (atamteua)
kwa sababu, Magufuli kimataifa hajulikani sana. Kwa hiyo ili mambo yake
yaende vizuri, lazima atawategemea hawa kwa vile wana uzoefu na nje kwa
muda mrefu.
“Migiro alishakaa Umoja wa Mataifa akimsaidia Katibu Mkuu, Ban Ki-moon.
Membe yeye alikuwa waziri wa wizara hiyo kwa miaka kumi,” alisema Celina
Samson, mkazi wa Ilala Boma.
WIZARA YA AFYA
“Naamini Hussein Ally Mwinyi (Zanzibar) anaiweza. Arudishwe pale kwani
hata alipokuwa awali aliiweza. Lakini naibu wake anafaa sana kuwa Mbunge
wa Kigamboni, Faustine Ndungulile (Mkoa wa Dar es Salaam). Huyu jamaa
kwenye afya ni mkali,” alisema Joseph Hamisi, mkazi wa Temeke Sokota.
WIZARA YA UJENZI
“Hii wizara ndiyo ya Magufuli mwenyewe. Kwanza naamini ataipeleka kwenye
ofisi yake. Waziri wake ataitwa waziri wa nchi ofisi ya rais, ujenzi,
uchukuzi na miundombinu. Atampa Harrison Mwakyembe (Mkoa wa Mbeya).
Asaidiwe na Gerson Lwenge ( mpya Mkoa wa Njombe), hawa jamaa wataiweza
kwani na wao ni mchakachaka kama Magufuli mwenyewe,” alisema Kidawa
Halfan, mkazi wa Kigamboni, Tungi, Dar.
MAWASILIANO SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mzee Salimu Jenda, mkazi wa Mikocheni: “January Makamba (Mkoa wa Tanga),
naamini atarudi kuwa waziri kabisa. Lakini huyu anatakiwa kusaidiana na
Hamis Kigwangala (Mkoa wa Tabora). Hii timu ikiwa pamoja mambo
yataiva.”
WIZARA YA FEDHA
“Kwanza hii wizara naamini itaunganishwa na Mipango. Mwigulu Lameck
Nchemba (Mkoa wa Singida) ni sahihi kwake kuwa waziri kamili badala ya
unaibu kama alivyokuwa mwanzo. Asaidiwe na yule mama Angelina Mabula
(mpya Mkoa wa Mwanza) ni mzuri sana. Ni mchumi na mbobezi wa mambo ya
uhasibu. Wataiweza hii wizara ikiwa moja,” alisema Maua Jumanne, mkazi
wa Kibamba.
WIZARA YA ULINZI
Sakina Ngalawa, mkazi wa Vingunguti: “Kwanza hii wizara iungwe na wizara
ya mambo ya ndani, iwe moja tu. Magufuli alishasema ataunda baraza
dogo. Anayeimudu ni Kangi Lugola (mpya Mkoa wa Mara) ni mpiganaji mzuri
sana. awe waziri kamili akisaidiwa na Injinia Stella Manyanya (Mkoa wa
Ruvuma)
WIZARA YA SHERIA
“Anayefaa ni Job Ndugai (mpya Mkoa wa Dodoma). Unajua yule bwana yupo
vizuri sana kwenye sheria na ana misimamo. Wanasheria wote wako vile,”
alisema Roman Joseph, mkazi wa Mbagala Kuu.
OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA NA URATIBU WA BUNGE
“Jamani mimi naona Nape Nnauye (mpya Mkoa wa Lindi) ndiyo anaiweza.
Tumeona alivyopigania chama chake mpaka kubaki madarakani. Ni mzuri
kwenye kuratibu na kusimamia sera,” alisema Anna Mmakonde, mkazi wa
Msasani.
WIZARA YA ELIMU
“Jenista Joachim Mhagama (Mkoa wa Ruvuma), angetolewa kwenye sera na
uratibu wa bunge awe waziri kamili wa elimu. Huyu mama ataiweza, ni
mpiga kazi mzuri sana,” alisema Saimen Kimari, mkazi wa Buguruni.
Hata hivyo, haya yanabaki kuwa maoni na mtazamo wa wasomaji wetu, nafasi
hizo za utumishi, zinabaki kuwa maamuzi ya rais mwenyewe kulingana na
sifa zao.
Source: Global Publishers

No comments:
Post a Comment