13 August 2015

HAWA NDO WABUNGE WALIOKATWA DODOMA KUTOKANA NA KASHFA ZA RUSHWA


Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), imepitisha majina ya wagombea ubunge wa majimbo pamoja na viti maalumu, huku baadhi ya wabunge wakongwe wakijikuta wakitupwa nje.Katika kikao hichokilichoanza juzi na kumalizika jana mjini hapa, chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, waliokatwa ni Mbunge wa Babati Mjini anayemaliza muda wake,Kisyeri Chambiri na mwenzake wa Babati Vijijini, Virajilal Jituson.
Wengine walioangukiwa na rungu la Kamati Kuu ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu ambaye alishinda katika kundi la mashirika yasiyo ya kiserikali, Rita Mlaki na Mbunge wa Sikonge anayemaliza muda wake, Said Nkumba.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kilisema kuwa hatua ya kufikiwa kwa uamuzi huo ni kutokana na wagombea hao kuhusishwa na tuhuma za rushwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, pamoja na baadhi yao kushinda na hata kukatiwa rufaa, lakini bado walionekana kuwa na makosa ya wazi ikiwamo ya kuhonga wajumbe kwa kuwashawishi ili wachaguliwe katika nafasi hiyo.
Katika mchakato huo, Jituson wa Babati Vijijini alipata kura 8,523 kati ya 32,073 zilizopigwa na aliyemfuatia alikuwa Daniel Sillo aliyepata kura 6, 222.
“Hali imekuwa tete kwa baadhi ya wabunge, hasa wa Babati Mjini na Vijiji ambao wote wameondolewa katika uteuzi na Kamati Kuu, unajua Chambiri ana tuhuma za rushwa na ripoti ya Takukuru ilisaidia sana kummaliza katika vikao hivi vya uteuzi.
“Ila mwenzake wa vijijini, Jituson yeye alilalamikiwa na wagombea wenzake na hata kumuhusisha na tuhuma za rushwa hali ambayo pia vilipatikana baadhi ya vielelezo dhidi yake.
“Ila kwa Rita Mlaki ni wazi hapa unaweza kusema kama kuna uonevu wa wazi kwani alishinda kura za maoni kupitia UWT kundi la NGO’s, lakini CC ikatumia hoja ya uwiano bara na Zanzibar.
“Badala yake wamemwondoa yeye aliyeshinda na kuteuliwa Mjumbe wa Kamati Kuu,Hadija Abood ambaye yeye katika kundi hili sasa amepangwa na Mchungaji Getrude Lwakatare, hoja hii ya uzanzibari imetumika katika kundi hili tu haikugusa kundi la wafanyakazi wala walemavu,” alisema mtoa habari huyo ambaye aliomba ahifadhiwe jina lake.
Katika kura za maoni zilizofanyika Agosti mosi mwaka huu, Chambiri alishinda dhidi ya makada wengine saba wa chama hicho ambao walipinga matokeo hayo.
Katika mchakato huo wa kura za maoni, Chambiri alipachikwa jina la ‘ATM inayotembea’ kutokana na madai ya kugawa fedha kwa wapiga kura, madai ambayo hata hivyo aliyakanusha mara kwa mara.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa Chambiri alikamatwa mchana na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) akiwa ndani ya ofisi za CCM Wilaya ya Babati Mjini.
Habari zaidi kutoka ofisi za Takukuru zinaeleza kuwa hatua ya kumtia mbaroni mbunge huyo ilitokana na kutafutwa kwake kwa zaidi ya siku tano baada ya kudaiwa kushiriki vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa kampeni kuelekea kura za maoni.
Inadaiwa Chambiri alinusurika kukamatwa na maofisa wa taasisi hiyo katika Kijiji cha Kiongozi ambapo wapambe wake wawili walikamatwa wakiwashawishi wapiga kura kwa kuwapa fedha na kukutwa na kitita cha Sh milioni 12.5.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname