JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
SHAURI LA UKIUKAJI WA KANUNI ZA UTANGAZAJI
NAMBA 4/2015
DHIDI YA
INDEPENDENT TELEVISION (ITV)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KATIKA KAMATI YA MAUDHUI YA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
DAR ES SALAAM
SHAURI LA UKIUKAJI WA KANUNI ZA UTANGAZAJI
NAMBA 4/2015
DHIDI YA
INDEPENDENT TELEVISION (ITV)
UAMUZI
UAMUZI WA KAMATI YA MAUDHUI KUHUSU LALAMIKO LA UKIUKAJI WA
KANUNI ZA UTANGAZAJI, MWAKA 2005
1.0 Utangulizi:
Mnamo tarehe 10/08/2015, kituo cha ITV kilikiuka Kanuni za
Huduma ya Utangazaji (Maudhui), 2005 kupitia kipindi cha Habari Zilizotufikia
Hivi Punde kilichorushwa hewani kati ya saa 2.30 asubuhi hadi saa 5.30 asubuhi.
Kipindi hiki kilikiuka Kanuni za Utangazaji kwa kutoa taarifa zisizo za kweli
na za kichochezi zilizotangaza kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam limepiga marufuku maandamano ya mgombea wa CHADEMA Mheshimiwa Edward
Lowassa. Taarifa hiyo ilikuwa na maandishi yaliyosomeka kama ifuatavyo:-
1. “ Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lapiga
marufuku maandamano ya kumsindikiza kuchukua fomu mgombea Urais kupitia
CHADEMA”.
2. “ Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lakanusha
kupiga marufuku maandamano kutokea ofisi za CUF kuchukua fomu Mgombea Urais kupitia
CHADEMA.
Katika kuhitimisha taarifa hiyo mtangazaji alisikika
akisisitiza kwamba Kamishina Suleiman Kova alisema ni marufuku maandamano ya
mgombea wa CHADEMA kupitia UKAWA kwenda kuchukua fomu katika Tume ya Taifa ya
Uchaguzi. Mtangazaji alisikika akizungumza maneno yafuatayo:-
“….ni Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Suleiman
Kova akizungumza na ITV, Radio One pamoja na Capital Radio amesema ya kwamba ni
marufuku maandamano ya Mgombea wa CHADEMA kupitia UKAWA Mheshimiwa Edward
Lowassa kwenda kuchukua fomu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi… hizo
ndizo taarifa ambazo zimetufikia hivi punde”
2.0 Kanuni zilizokiukwa
Kituo cha ITV kimekiuka Kanuni zifuatazo za Huduma ya
Utangazaji (Maudhui) 2005
Na. 5(h), 6(2)(b) na 6(2)(c) ambazo zinazosomeka hivi:-
5 Every licensee shall ensure that the programme and its
presentation-
(h) does not incite or perpetuate hatred against or vilify,
any
group or persons on the basis of ethnicity, race, gender,
Religion or disability.
6(2) The licensee shall-
(b) report accurately and fairly;
6(2)(c) report news in an objective and balanced manner,
without
intentional or negligent departure from the facts, whether
by
distortion, exaggeration, misrepresentation or material
omission;
Tafsiri ya Kanuni hizi kwa mujibu wa Kamati katika shauri
hili ni kama ifuatavyo:-
5. Kila mwenye leseni ya utoaji huduma za utangazaji lazima
ahakikishe kuwa vipindi vyake vinazingatia:-
(h) havileti uchochezi wala kujenga chuki kwa mtu au kundi
la watu kwa kigezo cha kabila, rangi, jinsia, dini au ulemavu.
6(2) Kila mwenye leseni ni lazima ahakikishe-
(b) anatoa taarifa kwa usahihi na uhakika;
6 (2) (c) anaripoti habari bila upendeleo na kizingatia
mizani, bila
kukusudia au kuondoka katika ukweli, ama kwa
kuvuruga au kutoa taarifa zisizo sahihi.
3.0 Ushahidi wa Makosa
3.1 Kuangalia DVD ya kipindi cha “Habari Zilizotufikia Hivi
Punde”
Ili kujiridhisha kama maudhui ya kipindi cha Habari
Zilizotufikia Hivi Punde na uwasilishaji wake ulikiuka Kanuni za Utangazaji,
Kamati na uongozi wa ITV waliangalia sehemu ya kipindi hicho. Maudhui ya
kipindi hicho yalionyesha ukiukwaji wa Kanuni za Utangazaji.
4.0 Maelezo ya utetezi
4.1 Maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa ITV
Mkurugenzi wa ITV aliwasilisha utetezi wa maandishi wakikana
kuhusu tuhuma zote za ukiukwaji wa Kanuni uliofanywa na kituo chao. Alisema
msingi wa habari ulikuwa si wa kichochezi na ilikuwa ombi la Kamishna wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kutoa ufafanuzi wa taarifa za
upotoshaji zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
Aliendelea kusisitiza kwamba taarifa haikuwa ya kichochezi
kutokana na ukweli kwamba watu walikuwa wamekusanyika Buguruni Ofisi ya CUF kwa
lengo la kuandamana kumsindikiza Mgombea Urais wa CHADEMA jambo ambalo Kamishna
Kova alipiga marufuku. Mkurugenzi pia aliendelea kusema kuwa wakati wakirusha
hewani taarifa ya Kamishna Kova walikuwa wanabadilisha maandishi kwenye runinga
kulingana na taarifa zilizokuwa zinatolewa na Kamishna Kova.
Aliendelea kusema kwamba pamoja na kutoa taarifa
iliyolalamikiwa Kamishna Kova alirudi tena kwenye kituo cha ITV na alitoa
taarifa kwa umma kwamba Jeshi la Polisi liliafikiana na viongozi wa vyama hivyo
kwamba maandamano yaanzie ofisi za CUF zilizoko Buguruni hadi ofisi ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi na baadae kuishia Kinondoni katika ofisi za CHADEMA.
4.2 Maelezo ya Mhariri Wa Habari
Mhariri wa Habari wa ITV alitoa utetezi wake kwa kusema
kwamba nia ya ITV haikuwa kuleta uchochezi kwa kuwa habari ilikusudia kuondoa
upotoshaji wa taarifa kwamba watu waache kwenda mjini kutokana na kuwepo kwa
maandamano ya CHADEMA. Alisisitiza kwamba Mtangazaji wa taarifa hiyo hakuwa na
nia mbaya wala kusudio la kuchochea uvunjifu wa amani na dhamira yake haikuwa
kumfanya Kamishna Kova kuongea anachokitaka yeye kama mwandishi wa habari ila
kuondoa hofu kuhusiana na suala zima la maandamano.
4.3 Maelezo
Mwanasheria/Mwakilishi wa ITV alitoa utetezi wake kwa kusema
maneno yaliyoandikwa kwenye taarifa hiyo yalikuwa ni vionjo tu vya kumwezesha
mtazamaji kuvutiwa na taarifa kisha asikilize na kupata ukweli. Bwana Semvua
alitoa mfano wa magazeti yanavyotoa vionjo vya taarifa mbalimbali ambazo
humvutia mtu kuisoma habari katika tukio husika.
5.0 Kukiri Kosa
Katika majumuisho yao wawakilishi waliotoa utetezi wa ITV
moja baada ya mwingine walikiri kosa na kudai kuwa kituo chao hakina kawaida ya
kuitwa mbele ya Kamati kwa makosa na wao kama binadamu hawakuwa na dhamira ya
kusababisha vurugu nchini kwa kuwa binadamu hukosea.
Mhariri wa Habari ITV alisisitiza kwamba haikuwa nia yao
kuleta uchochezi na wala mtangazaji wa taarifa hiyo hakuwa na nia mbaya.
Mhariri wa habari alizungumza maneno yafuatayo:-
“Mwenyekiti tunakushukuru, tunaomba mtuelewe kwamba muktadha
wa tukio lote hili haukuwa na nia mbaya, kwa maana ya kwamba nia mbaya haikukusudiwa…hakukuwepo
na kusudio , hakukuepo na nia mbaya na ovu yoyote kupeleka lile tukio liwe na
tafsiri ya watu kwa jinsi walivyo lipokea…”
Mwanasheria/Mwakilishi alisema lengo halikuwa kufanya kosa
hilo kwa makusudi na naomba mtuchukulie hivyo tulifanya kosa kwa bahati mbaya,
makosa yapo kwa binadamu na tafsiri ya kimtazamo ni kawaida kukosea na ilikuwa
ni bahati mbaya watajirekebisha. Alisema maneno yafuatayo:-
“Makosa yapo ya kila mwanadamu, tulifanya hivyo tudhani
tumefanya vizuri na ndio maana tulidhani tutapongezwa, lakini mtizamo wa
wenzetu kwa kweli imeonekana na tulivyosikia…si kweli kwamba tunaonewa asilimia
mia moja.. ukiangalia ITV na Redio One siyo vituo vinanyoletwa letwa huku mara
nyingi na ikitokea mtuchukulie kwamba imetokea kwa bahati mbaya kama wanadamu
na sisi tutajirekebisha kwa haya mliyotuadvise…..”
Aidha Mkurugenzi wa Radio One alikiri kwamba lengo lilikuwa
zuri na kusudio lilikuwa kuondoa uvumi uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Bwana Deo Rweyunga alisema yafuatayo:-
“…wito wenu ni wa nia ya kutaka kujirekebisha ili tuende
vizuri pamoja, mmetuandikia tumejieleza, tumekaa pamoja na tumezungunza pamoja,
lengo lilikuwa ni zuri tujaribu kuondoa uvumi ambao ulikuwa tayari kwenye
mitandao….tukiri katika hili ambalo limeonekana kidogo ni tofauti, tutachukua
hatua kama inavyofahamika vyombo vyetu tumekuwa tunajitahidi sana na tumeteleza
kidogo tunaomba mtuwie radhi kwa hilo”
Mkurugenzi Mtendaji alisema Breaking News ya Tanzania
inavyoendeshwa ni vigumu kuipata, tunaomba radhi kwa hilo lililotokea haikuwa
dhamira yetu, tutahakikisha tunaedelea na dhamira yetu ya kutoa matangazo kwa
ubora. Kubwa lilituleta ni mwanzo na mwisho wa taarifa yenyewe na waliomba
radhi na kuhakikisha watafanya kazi kwa umakini. Alisema maneno yafuatayo:-
“…pamoja na hayo kubwa ambalo limetuleta ambalo tumeliona ni
mwanzo na mwisho…na marekebisho ambayo tuliona tukarekebishe tukiwa hewani ni
kwamba tunaomba radhi kwa hilo kwa sababu sisi tulikuwa tunaongea kwa upande
wetu jinsi tunavyofanya kazi…..tunaomba radhi kwamba limetokea hivyo
liliyotokea na hivyo lilivyopokelewa huko nje…na haijawa dhamira yetu wala nia
yetu ya kuvuruga hii nchi…”
6.0 Tathmini ya Kamati
Kamati iliridhika kwamba, kituo cha ITV katika kipindi cha
Habari Zilizotufikia Hivi Punde kilikiuka Kanuni za Utangazaji kwa kutoa
taarifa zisizo za kweli na za kichochezi zilizotangaza kwamba Jeshi la Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano ya mgombea wa
CHADEMA Mheshimiwa Edward Lowassa.
Kamati iliona upungufu katika maneno yaliyoandikwa kwenye
runinga (subtitling) wakati Kamisha Kova akihojiwa. Katika utangulizi wa Habari
Zilizotufikia Hivi Punde mtangazaji alisikika akisema kwamba Jeshi la Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam lapiga marufuku maandamano ya kumsindikiza kuchukua
fomu mgombea Urais kupitia CHADEMA. Mtangazaji alisikika akimhoji Kamishna Kova
kutoa ufafanuzi kuhusu kupiga marufuku maandamano. Kamishna Kova alisikika
akisema alichukua nafasi hiyo kuwapigia ITV na Radio One kuondoa uvumi uliokuwa
umeenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa Polisi wamepiga marufuku maandamano ya
Kumsindikiza Mheshimiwa Lowassa kuchukua fomu za kugombea Urais katika Ofisi za
Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kamishna Kova alisema Polisi ilikuwa imepanga kuwapa
ulinzi wasindikizaji wa Mgombea Urais Mheshimiwa Lowassa kupitia CHADEMA kutoka
ofisi za CHADEMA Kinondoni mpaka ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama Jeshi
la Polisi lilivyotoa ulinzi kwa wasindikizaji wa mgombea Urais Kupitia Chama
Cha Mapinduzi DKt John Magufuli. Kamisna Kova alisisitiza kuwa haikuwa jambo
jema kwa maandamano kutokea kila sehemu ya jiji kwa vile kungeweza kuleta
uvunjifu wa amani na kuathiri shughuli zingine za wananchi. Kamisna Kova
alisisitiza kuwa:-
“………ukiwazuia watu kwa kwenda tu kuchukua fomu hapo unaweza
kusababisha uvunjifu wa amani na njia tunayoisema ambayo tunaitambua ni hiyo
ambayo mimekueleza na ninachukua fursa hii kukanusha kabisa maelezo hayo siyo
ya kwetu na hata jinsi ilivyoandikwa hili tangazo siyo model yetu na namna yetu
ya kuandika taarifa…kwahiyo tunaomba pia watu wasipotoshe watu na masuala ya
Kipolisi ni nyeti mno na mtu asijaribu kutengeneza taarifa za kupotosha watu
kupitia Kiongozi wowote wa Jeshi la Polisi….”
Mwandishi katika kuhitimisha Habari Zilizotufikia Hivi Punde
alirudia na kusisitiza kwamba Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam
lapiga marufuku maandamano ya kumsindikiza kuchukua fomu mgombea Urais kupitia
CHADEMA. Hii ni kinyume na utetezi uliotolewa na uongozi wa ITV na Radio One
kwamba walikuwa na nia ya kusaidia kutoa ufafanuzi juu ya uvumi ulioneea kwenye
Mitandao kuwa Polisi walipiga marufuku maandamano.
7.0 Uamuzi wa Kamati
Kamati iliridhika kuwa kipindi cha Habari Zilizotufikia Hivi
Punde kilichorushwa hewani na kituo cha ITV tarehe 10/08/2015 kilikiuka Kanuni
za Utangazaji.
Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya
utetezi kutoka viongozi wa ITV na Radio One, Kamati ya Maudhui inaamua
yafuatayo:-
1.1 ITV inapewa onyo kali; na,
1.2 ITV inatakiwa kukanusha na kuomba radhi katika taarifa
yake ya Habari ya saa mbili usiku na asubuhi kwa siku mbili mfululizo baada ya
kusomwa kwa uamuzi huu.
Endapo ITV itakiuka tena Kanuni za Utangazaji, hatua kali
zaidi za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Uamuzi huu umetolewa na kusomwa Dar es Salaam siku hii ya
tarehe13 Mwezi wa Agosti Mwaka 2015.
Haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu iko wazi ndani ya
siku 30 tangu uamuzi unapotolewa.
Uamuzi umetolewa na:
Mhandisi Margaret T. Munyagi
Mwenyekiti
Na:
WAJUMBE WA KAMATI YA MAUDHUI
1. Bwana Walter Bgoya
2. Bwana Joseph Method Mapunda
3. Bwana Abdul Ramadhani Ngarawa
13 AUGUST 2015
No comments:
Post a Comment