Chama cha
Mapinduzi (CCM) kimempitisha Dk John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais
wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika
Oktoba 25, mwaka huu.
Kwanza
kabisa napenda kumpongeza sana Magufuli kwa hatua aliyofikia na kumtakia
kila la heri. Naomba kukiri kwa uwazi kwamba katika uchaguzi
unaohusisha vyama vya siasa ni lazima mshindi atapatikana na kwa
Tanzania ni lazima mshindi huyo atoke kwenye chama cha siasa.
Tanzania
ina vyama 22 vilivyosajiliwa na vinavyofanya kazi sasa, tutake tusitake
ni lazima rais wa nchi atatoka katika chama kimojawapo, na kwa sababu
CCM imeshapitisha mgombea wake na yeye ana fursa ya kushinda uchaguzi
kama ambavyo fursa hiyo ilivyo kwenye vyama vingine. Natumia nafasi hii
kufanya uchambuzi wa dhati juu ya taswira ya serikali ya Magufuli ikiwa
atafanikiwa kushinda uchaguzi wa mwaka huu. Taswira ya namna hii pia
nitaifanya kwa wagombea wengine wa vyama ambavyo vitaamua kuweka
wagombea urais.
Katika
kulifanya jukumu hili nitachambua masuala 10 ambayo nafikiri kwamba
yanaweza kujenga utawala wa Magufuli, ikiwa atachaguliwa na Watanzania
kuwa rais wa awamu ijayo.
Mambo
matano kati ya hayo nayatazama kama taswira bora na mengine matano
yanaweza kuwa taswira hasi. Katika uchambuzi wa leo nitaanza na mambo
matano ambayo ni taswira bora.
Usimamizi bora
Taswira
ya kwanza ambayo Magufuli anaweza kuirejesha bila wasiwasi ni usimamizi
thabiti wa serikali na nidhamu ya utendaji ndani ya serikali. Naamini
kuwa serikali ya Magufuli itakuwa ya kiusimamizi na yeye mwenyewe
anaweza kulifanya jambo hilo bila kusita. Katika nyadhifa nyingi
alizopitia hadi sasa ameijenga taswira hii kila alikopita na bado
inambeba hata ikitokea anachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano.
Tukumbuke
kuwa moja ya mambo ambayo yameanguka kabisa nchini hivi ni utendaji
ndani ya serikali. Tunafahamu kuwa wafanyakazi ndani ya serikali
ukiachilia mbali matatizo waliyonayo kwa maana ya vipato, hata mambo
madogo ambayo wangeweza kuyasimamia ndani ya dakika au saa chache
huchukua wiki kadhaa na hata miezi kadhaa. Utaratibu wa utoaji huduma
umekwama sana na nadhani kama akiwa na uwezo huo atafanikiwa kutatua
changamoto kubwa na ya siku nyingi. Ikiwa utendaji wa serikali
unaimarika na huduma zinatolewa kwa wakati, tutaweza kujenga taifa
linalokwenda mbele bila kujali chama gani kiko madarakani.
Msimamo imara
Taswira
bora ya pili ya serikali ya Magufuli inaweza kuwa ni misimamo katika
masuala ya msingi na kutoyumba sana. Magufuli muda wote ambao amekuwa
kiongozi ameonyesha jambo hilo. Kila mara amekuwa na misimamo hata kama
siyo sahihi. Kwa tafsiri nyingine hii huwa ni njia bora ya uongozi wa
nchi japokuwa misimamo ya serikali au kiongozi mkuu wa serikali huwa
haipaswi kuwa juu ya haki na matakwa ya wananchi.
Moja ya
mambo ambayo serikali iliyopita ilikosa, ni pamoja na kukosa misimamo na
kuwa na “double standard”. Mfano mdogo tu ni kwenye mchakato wa katiba
mpya ambapo Rais anayeondoka alisimamia uanzishwaji bora wa mchakato
huo, akaunga mkono katika hatua zote na rasimu zote, lakini akaja
kuwageuka wajumbe wa tume hiyo na rasimu yao ya pili alipolihutubia
Bunge Maalumu la Katiba. Naamini Magufuli si mtu wa kugeuka na kuna
masuala mengi anaweza kuyasimamia kwa dhati na kila mmoja wetu akakubali
kuwa, naam! Hapa kuna kiongozi anasimamia masuala haya.
No comments:
Post a Comment