MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema hatma yake kisiasa ndani ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itajulikana katika kipindi
cha mwezi mmoja kutoka sasa.
Raia Mwema linafahamu
kwamba tangazo hilo la kisiasa linahusu mustakabali wake wa kisiasa
ndani ya Chadema, chama ambacho amekitumikia katika maisha yake yote ya
kisiasa tangu akiwa mtoto wa umri wa miaka 16.
Katika mahojiano
aliyofanya kwa njia ya mtandao na gazeti maarufu la Guardian la
Uingereza wiki iliyopita, Zitto alisema kuna kitu kikubwa atakifanya
mwishoni mwa mwezi Machi huu.
“Sijawahi kufanya
kampeni yoyote kubwa ya kisiasa kupitia mtandao wa twitter katika maisha
yangu ya kisiasa, lakini nataraji kuwa nitafanya hivyo katika muda wa
mwezi mmoja kutoka sasa. Fuatilieni tu twitter na mtaona,” alisema Zitto
pasipo kwenda kwa undani.
Gazeti hilo la Uingereza
limeanzisha utaratibu mpya wa kuhoji watu maarufu kwa kutumia mtandao
wa twitter (twit interview) na Zitto alikuwa mwanasiasa wa kwanza
kuhojiwa baada ya kubainika kuwa ndiye anayeongoza kwa kuwa na wafuasi
wengi kwenye mtandao huo hapa nchini.
Akizungumza na gazeti
hili kuhusu nini hasa anataraji kukifanya mwishoni mwa mwezi Machi kama
alivyozungumza na gazeti hilo, Zitto alisema ni mapema kwa sasa kuweka
kila kitu hadharani lakini wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi.
“Niseme kwamba kwenye
mahojiano yale nilisema hivyo kweli na nakuhakikishia kuwa kuna tukio
litatokea mwishoni mwa mwezi Machi. Ni tukio gani na linahusu nini bado
mapema kusema.
“Ila naomba kuahidi
Watanzania kuwa watafahamu kila kitu kuhusu tukio hilo wakati ukifika.
Hiyo kampeni ambayo itaendeshwa kupitia mtandao wa twitter na mingineyo,
itakuwa ya kisasa na ya uhakika kuliko yoyote ambayo imewahi kuendeshwa
katika historia ya Tanzania, “ alisema.
Zitto alikataa kusema
lolote kama tangazo hilo litahusiana moja kwa moja na kuhama kwake
kutoka Chadema kwenda ACT au chama chochote kingine cha siasa hapa
nchini zaidi ya kusema; “subirini”.
Kwa sasa, Zitto ni
Mbunge na mwanachama wa Chadema kwa sababu tu ya zuio ambalo Mahakama
Kuu kupitia Jaji John Utamwa liliweka katikati ya mwaka jana la
kufukuzwa kwake ndani ya chama hicho kutokana na kikao cha Kamati Kuu ya
chama hicho.Zitto na wenzake, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba,
walifukuzwa na Chadema kwa madai ya kupanga mapinduzi ya kumng’oa
madarakani Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mwigamba na Kitila
wamehamia katika chama kipya cha siasa cha ACT; Mwigamba akiwa Katibu
Mkuu wa muda na mwenzake mshauri na Zitto mwenyewe amekuwa akihusishwa
na chama hicho.
Akizungumzia mahojiano
hayo ya Zitto na Guardian, Dk. Kitila Mkumbo alisema aliyasoma mahojiano
hayo lakini akasema anayejua nini kitatokea mwishoni mwa Machi ni Zitto
mwenyewe.
“Mimi kama mshauri wa
ACT nasema Zitto kama mwanasiasa makini ana mawazo yake na mipango yake.
Mimi nasisitiza tu kwamba kama ataamua kuja ACT basi tunamkaribisha kwa
mikono yote miwili.
“Tunaamini kwamba yeye
ni muumini wa dhana ya Unyerere (Nyerereism) ambayo ndiyo msingi mkuu wa
sera za ACT. Kama ataamua vinginevyo, sisi pia tutamuunga mkono kwa
sababu tunajua itakuwa kwa nia njema,” alisema.
Katika mahojiano hayo na
Guardian, Zitto aliulizwa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu siasa na
Tanzania, ikiwamo changamoto za kisiasa, hifadhi za jamii na nguvu ya
mitandao ya kijamii katika siasa za hapa nchini.
Zitto alisema silaha
kubwa ya maendeleo ambayo Tanzania inayo kwa sasa ni wingi wa vijana
ambao alisema kama watawekewa mipango mizuri na kuwezeshwa kutumika kwa
kadri ya uwezo wao, Taifa litapiga hatua kubwa.
Alisema fursa hiyo ina
hatari yake nyingine kwamba chini ya asilimia 20 ya Watanzania hawana
ulinzi wowote wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii, jambo alilosema ni hatari
kwa mustakabali wa Taifa.
Alisema pia kwamba kwa
sasa Watanzania wengi wana ufahamu wa masuala ya mitandao ya kijamii,
lakini akasema idadi ya wanaoitumia ni ndogo; huku akibainisha kuwa
baadhi ya viongozi wa juu wa serikali hawako hata kwenye mitandao kama
twitter.
Zitto ana wafuasi zaidi
ya 200,000 katika mtandao wa twitter akiwa anaongoza kwa wafuasi; huku
katika nchi nyingine barani Afrika wanaoongoza wakiwa marais,
wanamichezo na wanamuziki maarufu kama Didier Drogba wa Ivory Coast na
Wiz Kid wa Nigeria.
No comments:
Post a Comment