MSHITAKIWA
wa kwanza, Salim Marwa katika kesi ya mauaji ya raia wa Ghana, Joseph
Opong ametoroka chini ya uangalizi akipatiwa matibabu katika Hospitali
ya Temeke, Dar es Salaam.
Mkuu wa
Magereza mkoa wa Dar es Salaam, Joel Bukuku alikiri kutokea kwa tukio
hilo Jumatatu usiku majira ya saa 6:00 huku akiwa na askari magereza
wawili. Alisema mshtakiwa huyo alikuwa akipatiwa matibabu hospitalini
hapo kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.
Lakini
hakufafanua zaidi kuhusu upasuaji wa nini wala alilazwa kwa muda gani.
Kuhusu alikotorokea mshitakiwa huyo alisema bado magereza haijafahamu
alikoelekea na kwamba tayari wametoa taarifa katika Jeshi la Polisi ili
kuweza kusaidia kupatikana kwake.
Aidha, alisema tayari wamesambaza askari kwa ajili ya kumtafuta ili kukamatwa na hatua nyingine kufuatia.
Kuhusu
askari waliokuwa wakimlinda alisema hajui kama kutoroka kwa mshtakiwa
huyo chini ya uangalizi wao ni uzembe, lakini kwa kuwa wanazo sheria zao
za Magereza watawafungulia mashtaka, kuwachunguza na kisha hatua
nyingine zitafuata.
“Mimi kwa
sasa niko nje ya ofisi, siwezi kuzungumzia zaidi kama mshtakiwa alikuwa
akisumbuliwa na nini na alilazwa hospitalini hapo kwa muda gani…na
hivyo sina details (taarifa) zaidi,” alisema Bukuku.
No comments:
Post a Comment