Juu ya
hivyo vipedo wamejiremba vijifulana vifupi visivyoficha mabega, matumbo
wazi; vitovu nje. Siyo ajabu kuona asilimia kubwa ya wakazi bara hili
miezi hii wakivalia ndala na kwenda nusu uchi; wanaume kwa wanawake.
Wasioonyesha
miili kiasi kile ni wanawake wa Kiislamu na Wayahudi wanaofuata pia
kanuni za kusitiri mwili. Kwa kanuni za Waislamu kinachoruhusiwa
kuonekana mwili wa mwanamke ni viganja vya mikono na nyuso tu.
Lakini
sivyo kwa wengi majuu, kutokana na majira nyanda za kaskazi ya dunia
kuwa baridi, mvua ya manyunyu na ukungu robo tatu ya mwaka. Ulimwengu ni
kama umekunja ndita kwa hasira.
Lakini
tangu mwezi uliopita mambo ahueni. Kwa Mzungu kuwaka jua kali ni jambo
adimu sana; lina Vitamin D inayotupa wanadamu furaha na kuijaza ngozi na
hisia.
Ukosefu
huu wa jua huwafanya wananchi wengi nchi za baridi kukosa raha hata
wakaugua. Ugonjwa huwa mkubwa kiasi cha kuwalazimu kwenda kwa daktari
kuandikiwa dawa ya furaha (anti-depressants). Ndiyo maana usishangae
kuwaona ndugu zetu weupe wanapoitembelea Afrika wakajianika (sana)
juani.
Kwa Mwafrika kukaa juani (kuliota) baada ya saa tatu asubuhi siyo kawaida, labda uwe mgonjwa wa homa.
Vilevile
wanavyolala juani ni jitihada ya kuibadili rangi ya ngozi hizi za mseto
wa weupe na wekundu hafifu walau uwe na kikahawia.
Kijiografia,
ulimwengu wetu huu wenye wanadamu bilioni moja, unaathiriwa na hali
tofauti za hewa. Wapo wanaousumbuliwa na vimbunga na matufani. Miezi hii
Visiwa vya Karibian na Marekani, wasioona mwangaza kwa siku sitini
uwanda wa kaskazini, Atikiti (Greenland, Finland, Norway, Canada, au
walio mazingira ya ukame na mchanga, Jangwa Kalahari, Gobi hata Sahara.
Sasa kina dada wamenisimamisha.
"Samahani wee mkazi eneo hili?" "Ndiyo!"
"Tumepotea kidogo. Unaweza kutuelekeza tafadhali?"
Wanatafuta kituo cha tiba ya miguu. Mmoja anachechemea. Biashara ya tiba ya miguu ni kubwa sana majuu.
Kati ya
maradhi yanayoangaliwa ni Funza wa Kuvu ("fungus")anayeishi sehemu watu
wanapotembea peku peku kama penye madimbwi ya kuogelea kitaalamu anaitwa
Virucca. Virucca akishaganda unyayoni ni kazi sana kumtoa.
Mganga
wake anaitwa Chiropodist au Podiatrist,elimu yenyewe inaitwa "Chiropody"
au "Podiatry" na hutoza Sh1 milioni au zaidi kumwondoa funza huyo, hapa
London.
Tatizo
jingine ni uvimbe unaotokea kwenye kidole gumba na kile kidogo, mguuni.
Uvimbe huu wa mfupa unaoitwa "bunion" kwa Kiingereza huwaathiri zaidi
wanawake kutokana na viatu vya kubana bana. Baadhi ya wanaume pia
huupata.
Ili kusawazisha inabidi ufanywe upasuaji unaorekebisha mfupa wa kidole na hilo huchukua siyo chini ya miezi tisa kupona kabisa.
Wakati nikiwaelekeza hawa kina dada, ninamwona mmoja akimwegemea mwenzie.
"Vipi umeumia ?"
"Ah, udhia mtupu. Miguu yangu imekwisha."
"Kwa vipi?"
"Viatu vya mchuchumio."
Wanacheka,
mchanganyiko wa dhihaka na kero. Hivi karibuni, utafiti uliofanywa hapa
Uingereza umegundua kuwa asilimia 90 ya wanawake wameshapatwa na
maumivu ya miguu, magoti au mgongo kutokana na viatu vyenye urefu wa
sentimeta 10 hadi 15, vinavyoitwa "high heels" kwa Kimombo.
Wanawake
waliohojiwa katika utafiti walikiri wanajua kama wavuta sigara walivyo,
kuwa siyo vizuri kuvaa viatu vya mchuchumio, lakini huendelea tu
kuvivaa. Utafiti huu uliotangazwa ndani ya majarida ya mavazi na urembo
ulisema, mjini New York, mathalan, viatu virefu aina ya Stilleto
vinavyovutia macho na kupendeza, vinajeruhi wanawake kutokana na siyo
urefu wake tu.
Mmoja wa
watengenezaji wa viatu hivyo alikiri hulipwa fedha nyingi kutoa madarasa
kwa wanawake husika namna ya kuvitembelea. Anasema mbali na urefu wa
viatu hivyo, tatizo ni kutojua kuvitumia.
Uchunguzi
mwingine uliofanywa Australia umetanabahi namna ajali nyingi za
kuanguka, majeruhi na maumivu zinavyowaathiri wanawake wanaofanya kazi
za umaarufu mfano utangazaji TV na ubunifu mavazi.
Uchunguzi ulibaini muda kuwa maumivu hupoanza baada saa moja na dakika saba.
"Mwanamke
husikia maumivu kiasi ambacho huamua kuviondoa na kurudi nyumbani peku
peku." Tatizo linatokana na wanawake hasa vijana, kudhani wanavutia
zaidi kihaiba kuliko wakiwa na viatu vifupi.
Miaka ile
nilipoishi Brazili kulikuwa na misemo iliyowagawanya wanawake mafungu
mawili. Mosi ni wale waliovalia mavazi ya kubana bana, wadogo wadogo,
mviringo mviringo, umbo la herufi nane. Mwanamke aliyedondokea daraja
hili aliitwa "gitaa".... ( kwa Kireno "violão").
Wa pili
uliwahusu kina dada warefu kiasi, wenye nywele ndefu waliotembea haraka
na viatu vya mchuchumio. Waliitwa "ndege abiria"- eropleni Kiswahili-
(Kireno "avião") ikiwa na maana mwanamke aliyependeza kutokana na viatu
hivi virefu.
Maelezo
ya kitaswira kama haya huathiri zaidi wanawake, maana wanapopita mitaani
hutazamwa na kuwekwa katika mafungu na matabaka; huandamwa na
mipangilio ya kuvaa, kutembea na kadhalika. Mengi yanayomwekea masharti
ya urembo na wajihi, pia ni adha kwake.
Mfano ni
mtindo ulioenea hii leo kwa wanawake weusi kuvaa nywele za bandia au
kuzichoma zilainike. Mtindo huu umehodhiwa na wanawake weusi maarufu
kama mkewe Rais Obama (Michelle), mwimbaji Beyonce na mtangazaji tajiri
wa runinga, Oprah Winfrey.
Matokeo
wanawake wanapofikisha miaka 40, siku hizi hata mapema zaidi nywele
hudondoka, wanageuka vipara kutokana na dawa zilizomo ndani ya
ghasia zinazotumika. Nyingine ni matumizi yasiyo sahihi ya sidiria.
ghasia zinazotumika. Nyingine ni matumizi yasiyo sahihi ya sidiria.
Wanawake
wangapi wanafahamu saizi inayotakiwa kwa matiti yao? Je, utumiaji
sidiria unawezaje kuathiri haiba na afya ya kiungo hicho?
Kwa nini wanawake vijana sana siku hizi tayari wanafikiwa na tatizo la "malapa" (kuanguka matiti)?
Hii ni baadhi ya mifano; lakini tatizo la viatu vya mchuchumio siyo mchezo.
Licha ya kuhatarisha miguu, mgongo na magoti, linaweza kumfanya mwanamke ashindwe kabisa kutembea anapofikia uzeeni.
Suluhisho ni kuchagua viatu vinavyopendeza, lakini havikongi au kuchakaza mwili kiasi hicho.
Uchaguzi
huo ni wa mwanamke mwenyewe kujua linalomfaa na lisilomfaa. Si vyema
haiba na afya vikakinzana. Chanzo: www.freddymacha.com
No comments:
Post a Comment