19 October 2013

INASIKITISHA...MAMA NA WATOTO WAKE WATATU NA MFANYAKAZI WA NDANI WA FAMILIA MOJA WAFA KWA PAMOJA ...

MKOA wa Morogoro na vitongoji vyake kwa sasa umegubikwa na simanzi kubwa baada ya watu watano wa familia moja kufariki kwa mpigo katika ajali ya gari.
Happiness Mwakyami.
Ajali hiyo iliyohusisha gari ndogo aina ya Toyota Cardina, yenye namba za usajili T 180 AWT na Fuso namba T324 AWL lililokuwa likiendeshwa na John Mombozi likitokea Dar es Salaam, ilitokea Oktoba 13, 2013, eneo la Visiga, Kibaha mkoani Pwani.
Jeneza la Happiness Mwakyami.
NI MHADHIRI WA SUA
Watu waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) aitwaye Mwaitulo Suma Andalwisye aliyekuwa dereva wa gari ndogo na wanawe watatu; Gamalieli Mwakyami, Happiness Mwakyami na Jeremy Mwakyani pamoja na mtumishi wao wa ndani, Elita Mpagama.
Simanzi imeivaa familia hiyo ambayo kwa sasa imebaki na baba tu aitwaye Jimmy Wilson Mwakyami, mwajiriwa wa Kiwanda cha Sukari Kilombero, Morogoro ambaye ni Injinia.

Elita Mpagama.
IDD YA BALAA
Habari zilizopatikana eneo la msiba zinasema kwamba, Bi. Mwaitulo (36) alikuwa akielekea jijini Dar es Salaam ambapo angeiacha familia yake nyumbani kwa mama yake mdogo, Sister Mwakatogo ili wale Sikukuu ya Idd wakati yeye akiwa safarini Kampala, Uganda kikazi.


Ilielezwa kuwa, kwa sababu mumewe alikuwa kazini Kilombero, walikubaliana aichukue familia hadi Dar kwa bibi yao ili aiche hapo halafu yeye aendelee na safari yake ya Uganda.
“Huyu dada jamani ananiuma sana...unajua alipata safari ya kikazi kwenda Kampala, sasa akaona si busara kuwaacha watoto peke yao nyumbani, baada ya kushauriana na mumewe ndiyo akaamua kuwachukua akawaache kwa bibi yao, akirudi awapitie - kumbe Mungu alishapanga yake.

Suma Mwakyami.
“Inauma sana. Mimi namuonea huruma zaidi huyo mumewe. Inahuzunisha sana. Kuondokewa na familia nzima siyo jambo dogo. Mungu atamwekea wepesi na kumpa moyo wa ustahimilivu,” alisema jirani mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina lake  kwa kuwa si msemaji wa familia.
Jeneza la Suma Mwakyami.
SIMULIZI YA MAJONZI
Kati ya mambo yaliyozidisha majonzi katika ibada ya kuwaombea marehemu hao, Oktoba 15, mwaka huu nyumbani kwao, Sua mjini hapa ni namna ndoto za watoto waliofariki pamoja na mama yao zilivyozimika kama mshumaa kwenye upepo mkali.
Mtoto wa kwanza katika familia hiyo, Gamalieli (8) alikuwa anasoma darasa la nne katika Shule ya St. Marry’s mjini hapa, Happiness (5) alikuwa chekechea na Jimmy akiwa na umri wa miaka miwili tu wakati mtumishi wao wa ndani akiwa na miaka 18.

KIU YA ELIMU
Mhadhiri huyo alikuwa mama bora wa kuigwa katika familia za Kitanzania kwa kuwa alikuwa akipigania sana elimu. Kabla hajaanza kazi chuoni hapo, alipata elimu yake hapohapo, pia hadi mauti yanamkuta alikuwa akiendelea kusoma.
Mwaka 1999 alijiunga chuoni hapo akitokea Shule ya Sekondari Loleza, Mbeya ambapo alihitimu Shahada ya Kwanza katika Kilimo cha Bustani ‘Bachelor of Science in Horticulture’ mwaka 2003 na kuajiriwa hapohapo  kama Mhadhiri Mkufunzi.
Katika kujiendeleza zaidi mwaka 2007 alianza masomo ya Shahada ya Uzamili katika Mimea na Vipando ‘Master of Science in Crop Science’ ambapo alihitimu mwaka 2009 – akapandishwa cheo na kuwa Mhadhiri kamili.
Mpaka mauti yanamkuta alikuwa akisaka Shahada ya Uzamivu ‘Doctor of Philosophy – PhD’ chuoni hapo.

BABA ASHINDWA KUZUNGUMZA
mume wa marehemu Mwaitulo, Jimmy (mwenye shati ya michirizi) ambaye ajitihadi kujikaza na kupita mbele ya majeneza yote huku  machozi yakimbubujika.
Ijumaa lilitaka kuzungumza naye mawili matatu kuhusiana na namna alivyoupokea msiba huo, lakini hakuweza kutokana na kuzidiwa na huzuni.

SAFARI YA MBEYA
Kaimu Mkuu wa SUA, Utawala na Fedha, Profesa Jayro Matovelo alisema chuo kimepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa na kwamba marehemu alikuwa mchakapazi sana.
Baada ya ibada na kutoa heshima za mwisho kwa marehemu hao, msafara wa kuelekea nyumbani kwao, Kyela, Mbeya ulianza mishale ya saa 9 alasiri

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname