MATOKEO
ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yaliyotangazwa mwanzoni mwa
juma, yanaendelea kutawala mijadala mbalimbali kila kona.
Katika
matokeo hayo karibu shule zote za umma zimefanya vibaya, zile za kata
zikiongoza katika kufelisha, huku ile ya Mibuyuni iliyopo Kilwa mkoani
Lindi ikiwa ya mwisho kabisa katika kundi la shule zenye zaidi ya
wanafunzi 40.
Mkuu
msaidizi wa shule hiyo Robart Mzumbi, alisema kuwa matokeo hayo
yalitarajiwa kwa kuwa tangu wanafunzi hao walipoandikishwa kidato cha
kwanza, hawakuwa wamefaulu.
Alibainisha
kuwa, matokeo ya kidato cha pili ya wanafunzi hao walipofanya mtihani
wa taifa mwaka 2010, yalikuwa kiashiria kingine kwamba, hata kwenye
matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wanafunzi hao hawatafanya vizuri.
Pamoja
na hayo, Mzumbi anaeleza kwamba kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni
kuhakikisha wanafundisha watoto hao na mwisho wafanye vyema, matokeo
hayo yamewasikitisha kwa kiasi kikubwa.
Alitaja
upungufu wa walimu na umaskini wa kipato kwa jamii inayozunguka shule
hiyo kuwa ni moja ya sababu kubwa zilizosababisha matokeo hayo mabaya.
Mwalimu
huyo alibainisha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika shule
hiyo hujishughulisha zaidi na biashara ndogo ndogo, badala ya kusoma.
Aliweka
wazi kuwa, shule hiyo ilikuwa ya mwisho kati ya shule 3,392 zenye
watahiniwa 40 na kuendelea, wakati watahiniwa hao wa mwaka 2012
walipochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2009, ambapo walikuwa na
alama za chini.
Aliongeza
kuwa wanafunzi hao walichaguliwa kuanza kidato cha kwanza wakati tayari
wengi wao walishaanza kufanya biashara ndogondogo, hivyo walikusanywa
kutoka huko mitaani na kupelekwa shule.
“Ndugu
yangu shule yetu huwa inafanya vizuri kidogo, angalia matokeo ya kidato
cha pili mwaka huu Sekondari ya Mibuyuni imekuwa ya 115 kati ya shule
242 za Kanda ya Kusini, wanafunzi wanane wamefaulu kati ya 25 waliofanya
mtihani. Lakini kwa matokeo ya kidato cha nne, kwa kweli wanafunzi
waliochaguliwa mwaka 2009, hawakuwa na sifa bali waliokotwa tu ili
kujaza darasa,” alisema na kuongeza:
“Hata mtihani wa kidato cha pili mwaka 2010, walifanya vibaya sana na shule hii ilikuwa ya pili kutoka mwisho.”
Mzumbi
alisema kwamba shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo
kukosa maabara, upungufu wa walimu wa sayansi, usafiri na umeme wa
uhakika.
Pia
ina ukosefu wa maji, nyumba za walimu, mabweni kwa ajili ya watoto wa
kike, pamoja na shule kujengwa mbali na makazi ya wananchi.
Alieleza
kuwa wanafunzi wengi wanaosoma katika shule mbalimbali za Mkoa wa
Lindi, hulazimika kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni.
source:mwananchi.co.tz