WAMILIKI wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali wameiomba
Serikali kufuta mfumo wa GPA unaotumiwa na Baraza la Mitihani (Necta)
kupanga madaraja ya mitihani ya sekondari, kwa maelezo kuwa haufai kwa
kuwa unahalalisha watahiniwa waliofeli waonekane wamefaulu.
Akizungumza jana Dar es Salaam kuhusu matokeo ya kidato cha
pili ambayo yametangazwa na Necta hivi karibuni, Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (TAMONGSCO), Benjamin
Nkonya alisema matokeo hayo hayaeleweki kwani wameshuhudia baadhi ya
wanafunzi wanaoonekana kufanya vizuri chini ya mfumo wa GPA wakati
katika mfumo wa madaraja (division) wanaonekana wamefanya vibaya.
Kwa hali hiyo, Nkonya amemwomba Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kufuta mfumo huo hadi
pale Necta itakapokuwa tayari kujibu maswali kadhaa ya wadau wa elimu
ambao wanaona mfumo huo hauna tija katika kuboresha elimu.
Baadhi ya hoja ambazo zilihojiwa na Nkonya ni kwamba
kulikuwa na kasoro gani katika mfumo wa madaraja mpaka ukaja huo wa GPA
na akataka kujua ni nani alilalamikia mfumo wa division mpaka
ukaondolewa? Alihoji kabla ya mfumo huo kuletwa, ni wadau wapi
walishirikishwa?
Alisema TAMONGSCO ilipata taarifa za kuwepo kwa mfumo huo
wa GPA kupitia vyombo vya habari na hawakushiriki katika ngazi yoyote ya
mijadala ya kisera kama sheria inavyoelekeza.
Katibu Mkuu huyo wa TAMONGSCO alihoji, “Je, alama za
chini za gredi D, C,B na A zilibaki kama zilivyokuwa wakati wa mfumo wa
division au kuongeza gredi E na B+ ilikuwa mbinu ya kushusha alama za
ufaulu na matumizi ya GPA yakaanzishwa kwa lengo la kuficha ukweli kuwa
viwango vimeshushwa kwa kiasi kikubwa??
Nkonya pia alihoji mfumo huo una faida zipi na unasaidiaje
katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaomaliza wanakuwa na ujuzi stahiki
utakaowawezesha kuhimili changamoto za soko la ajira na utandawazi?
“Kwa hali hii bado tunaishauri Serikali isitishe matumizi ya mfumo wa GPA hadi pale hoja zetu zitakapopatiwa ufumbuzi,”alisema Nkonya.
No comments:
Post a Comment