SAKATA la mawaziri kuandamwa kwa kutowajibika limezidi kushika kasi ambapo safari hii, Rais Jakaya Kikwete ametakiwa kumfukuza kazi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa madai ya kuwa mchawi wa maendeleo ya nchi na mzigo namba moja.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Hawa Ghasia naye anadaiwa kuwa mzigo mwingine kwa taifa kutokana
na kubariki ufisadi katika wizara yake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM)
alipokuwa akichangia katika hoja mbalimbali kuhusu kamati tatu za Bunge
zilizowasilishwa bungeni juzi.
Kamati zilizowasilisha hoja zao ni ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Kamati ya Bajeti na Kamati ya Hesabu za Serikali.
Lugola alisema kama Rais Kikwete asipowafukuza kazi Pinda na Ghasia,
CCM itakuwa shakani kurejea madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
“Mimi nawashangaa wabunge wenzangu mnaosimama hapa na kutumia nguvu
zenu nyingi kuishauri serikali… hii serikali inayoongozwa na chama
changu haishauriki, kwa kipindi kirefu ina watu wasiojua majukumu yao.
“Ni ngumu kuishauri serikali kutokana na kuwa na mawaziri wasiojua
majukumu yao, kwa kutojua wanachokifanya wameamua kutohudhuria vikao
muhimu vya kujadili taarifa za kamati,” alisema.
Lugola alisema katika kikao cha jana, mawaziri sita na manaibu wawili
ndio waliohudhuria, hivyo waliobaki kukosa fursa ya kusikiliza michango
mbalimbali inayotolewa na wabunge.
“Mimi ni mbunge wa CCM, na pengine haya ninayotaka kuyasema yanaweza
yasiwapendeze wabunge wenzangu wa CCM, lakini ndivyo nilivyo, ndivyo
Mungu alivyoniumba, naomba wanisamehe. Nchi nyingine katika Bunge
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anapowasilisha
taarifa, ndiyo wakati nchi nzima masikio ya watu yanakuwa bungeni,
lakini kwetu ni tofauti,” alisema.
Wakati Lugola akichangia bungeni, walikuwepo mawaziri wanne tu na manaibu wawili, huku nafasi za mawaziri zikiwa wazi.
Waliokuwepo bungeni ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, Hawa
Ghasia, Sofia Simba, Shamsi Vuai Nahodha, Mhandisi Charles Kitwanga na
Janet Mbene.
“Lakini cha kushangaza kuanzia jana Waziri Mkuu ameenda kuhudhuria
mahafali wakati jambo muhimu kama hili linazungumzwa bungeni. Hata hivyo
pamoja na kuwa mheshimiwa spika jana (Juzi ) uliwatetea mawaziri kuwa
walikuomba ruhusa, lakini mimi hainiingii akilini kuwa waliomba ruhusa
mawaziri wote na kubaki mawaziri wanne na manaibu wawili,” alisema
Lugola.
Alibainisha kuwa kwa busara za kawaida spika asingekubali kuwaruhusu
mawaziri hao wakati kuna jambo la muhimu linajadiliwa kwa mustakabali
wa taifa na watu wake.
Lugola alisema TAMISEMI ina mtandao mkubwa wa utumiaji wa fedha ambao
hauwezi kuwatenganisha Waziri Mkuu na Waziri Ghasia ambapo asilimia 70
ya fedha za bajeti hupelekwa huko.
Alisema kuwa licha ya wizara hiyo kutengewa fedha nyingi, bado
serikali imekuwa ikisuasua kushughulikia masuala mbalimbali ya wananchi
wa kipato cha chini.
Lugola aliwataka wabunge wasiendelee kuwasaliti Watanzania kwa
kubariki ufisadi unaofanywa na viongozi wa TAMISEMI inayoongozwa na
Waziri Mkuu, Pinda.
Alibainisha kuwa kwa sasa serikali haishauriki, na jambo hilo
linaonekana wazi kwakuwa imeendelea kulipa mishahara hewa kwa
waliofariki, huku Watanzania wakiteseka kwa umaskini.
Lugola aliongeza kuwa serikali imekuwa ikibariki ununuzi usiokuwa na nyaraka jambo ambalo ni wizi, lakini unalindwa na viongozi.
“Mchawi wetu katika maendeleo serikalini, tatizo kubwa ni Waziri Mkuu
amekuwa mpole mno, hawajibiki…, matatizo yanatokea ndani ya nchi yupo
wapi? Wananchi Mwibara umaskini unakithiri, fedha zinaliwa ambazo
zingewapa madawati, watu wangepata madawati na maji, wangevua kwa uvuvi
wa kisasa, Waziri Mkuu, jamani nakulilia huko wapi uwajibikaji wako
ndani ya serikali?” alisema.
Naye Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA), alisema
serikali imeshindwa kufanya kazi, hivyo ni vema Watanzania wakafanya
uamuzi wa kuiondoa madarakani kwa kutumia sanduku la kura.
Alisema kinachoonekana kwa Serikali ya CCM ni kubariki ufisadi
kutokana na viongozi waliopo madarakani kushindwa kuwawajibisha
wanaobainika kufanya ufisadi kwa sababu ya kulindana.
Nyerere alisema aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine,
alikuwa na uwezo wa kuwawajibisha waliobainika kufanya ubadhirifu wa
mali za umma.
“Hapa serikali mnaweza kujipima kuwa hata nyinyi wenyewe
mmeishajikatia tamaa kutokana na kukosa huduma za kiafya na ndiyo maana
hata alipotokea babu wa Loliondo viongozi wote mlikimbilia huko kwenda
kupata kikombe,” alisema Nyerere.
Katika mjadala huo ambao umeibua hisia kali kwa wabunge, ambao kwa
asilimia kubwa wamekuwa wakilalama kuwa TAMISEMI kuna ufisadi mkubwa
ambao unafanyika huku serikali ikiwa imenyamaza kimya.
Katika mjadala huo wabunge walikuwa wakihoji sababu za watendaji
wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu kuhamishwa vituo vyao vya kazi badala
ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mara kwa mara wabunge na viongozi wa CCM wamekuwa wakiwalalamikia
mawaziri kwa kushindwa kuwajibika, hivyo kuisababisha serikali kuchukiwa
na wananchi.
Wiki mbili zilizopita Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alikaririwa akiwataja mawaziri wanne ambao wanatakiwa kutoa majibu ya
uwajibikaji wao kwenye Kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho
kinachotarajia kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.
Nape aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Kilimo Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza, naibu wake Adam Malima, Waziri wa Uvuvi na
Mifugo, David Mathayo na Waziri wa Maji, Jumanne Maghembe.
No comments:
Post a Comment