Katika kile kinachoonekana kwamba serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais John Magufuli haitalegeza kamba linapokuja suala la
kusitisha safari holela za nje za watumishi wa umma, Idara ya Uhamiaji imesema bado inakagua uwapo wa barua ya mwajiri na kibali maalum cha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Awali, ili kusafiri nje ya nchi mtumishi wa umma alihitaji pasi ya kusafiria yenye viza na tiketi.
Akizungumza na Nipashe kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa
Uhamiaji, Sylvester Ambokile, Msemaji wa Idara hiyo Tabu Burhan, alisema
idara hiyo inaendelea kusimamia kikamilifu maelekezo ya Rais.
Katika utekelezaji wa agizo hilo, kila mtumishi wa umma
anayesafiri nje ya nchi anatakiwa kuonyesha barua ya mwajiri wake na
kibali cha Ikulu, alisema.
Burhani alisema Idara hiyo inafanya ukaguzi huo katika
vituo vya usafiri kama viwanja vya ndege na mipakani ili kubaini watu
watakaokiuka kwa makusudi agizo la Rais Magufuli.
Burhan alisema ingawa kazi ya kuwadhibiti watumishi wa umma
wanaosafiri nje ni ngumu kutokana na hati zao za kusafiria kutoonyesha
kazi wanazofanya, lakini wamejipanga vizuri kutumia mbinu mbalimbali
kuwabaini.
“Tutawabana wakija kugonga mihuri hati za kusafiria,
tukigundua ni mfanyakazi wa serikali tutamuomba atupatie barua kutoka
kwa mwajiri na kibali cha Ikulu, kama hana tunamrudisha na hataweza
kusafiri,” alisema Burhan.
Alisema zamani ilikuwa rahisi kwa kila mtumishi aliyetaka
kusafiri nje ya nchi kutambulika kazi yake kwasababu walikuwa wakitakiwa
kujaza fomu iitwayo TIF 10 na TIF 12, mfumo ambao ulisitishwa mwaka
2005 baada ya kuanza kutumika hati za kusafiria za kieletroniki.
“Tunawashauri watumishi ambao wanataka kusafiri
wajiridhishe wenyewe kwanza, itakuwa usumbufu na hasara endapo
tutawarusidisha wakiwa tayari uwanja wa ndege,” aliongeza.
Akizungumzia idadi ya watu waliozuiliwa tangu kuanza kwa
utekelezaji wake, msemaji huyo alisema mpaka sasa hakuna mtumishi
aliyenaswa mbali na wafanyakazi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) ambao tayari wamesimamishwa kazi.
Watumishi hao ni Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha.
Agizo la kuwazuia watumishi kusafiri nje lilitolewa na Rais
Magufuli siku moja baada ya kuapishwa kwa lengo la kubana matumizi ya
serikali na hadi sasa ameshaokoa mabilioni ya fedha.
Akilihutubia Bunge la 11 na kulizindua mwishoni mwa mwaka
jana, Rais Magufuli aliwataka watanzania na wabunge waunge mkono uamuzi
wake wa kupiga marufuku safari za nje ambapo fedha nyingi zitaokolewa na
kutumika kwenye huduma za jamii kama barabara, afya na elimu.
Alitoa mfano kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2013 na
nusu ya 2014/2015 pekee, safari za vigogo nje ya nchi ziligharimu Sh.
bilioni 356.3 fedha ambazo alisema zingeweza kujenga barabara yenye
urefu wa Kilomita 400 au kutimiza miradi mbalimbali ya jamii.
Alisema tiketi za ndege pekee ziligharimu Sh. bilioni
183.160, mafunzo ya nje ya nchi Sh. bilioni 68.612 na posho za kujikimu
Sh. bilioni 104.552.
Novemba mwaka jana, Ikulu ilisambaza mwongozo unaoweka
masharti ambayo watumishi wa umma wanaotaka kusafiri nje ya nchi
watatakiwa kuyatimiza ili wapewe kibali cha kusafiri.
Sharti la kwanza ni kuomba kibali kwa Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue na maombi yawasilishwe kwa Msajili wa Hazina kabla
ya kwenda kwa Sefue ili aweze kujenga hoja kwa kuzingatia umuhimu wa
safari hiyo na tija itakayopatikana kutokana na safari hiyo.
Sharti lingine linamtaka Mtendaji Mkuu wa Shirika ama
taasisi apime kama safari hiyo ni muhimu kuombewa kibali kwa Katibu Mkuu
Kiongozi, kabla ya kuwasilishwa Hazina na aeleze manufaa ambayo nchi
itapata kutokana na safari hiyo.
Pia sharti lingine linataka mhusika aeleze umuhimu wa
safari hiyo na isipofanyika itaathiri vipi nchi. Mwombaji aanatakiwa
aeleze manufaa ya safari hiyo kwa taasisi na taifa; kama imewahi
kufanyika huko nyuma ilisaidia nini.
Ofisi za Umma zilipokea barua kutoka kwa Msajili wa Hazina
Novemba 12 mwaka jana ikieleza kuwa Rais Magufuli ametoa zuio la jumla
kwa safari za nje ya nchi katika utumishi wote wa umma na mihimili yake.
Barua hiyo ya Hazina ilisema zuio hilo litadumu hadi pale
itakavyoelekezwa vinginevyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment