Dodoma/Dar.
Mpambano rasmi wa CCM na Ukawa katika Bunge la Kumi na Moja unaanza
kesho huku mambo 10 yakielezwa yataibuliwa na kuchangamsha mjadala
unaotarajiwa kuwa wa aina yake katika kipindi cha siku 11 cha bunge
hilo.
Katika
mambo hayo kumi yanayotajwa kuwa yataibua mjadala mkali bungeni,
inaonekana mambo manne yapo dhahiri kutokana na vyama vinavyounda Ukawa
kukutana zaidi ya mara tatu kuyajadili.
Mkutano
huo wa pili wa Bunge la Kumi na Moja utakuwa wa wiki mbili, lakini
uliojaa matukio makubwa kama mabishano ya muundo wa Kamati za Bunge,
uchaguzi wa marudio Zanzibar, upinzani kuzuiwa kufanya mikutano ya
kuwashukuru wananchi na kuahirishwa kwa Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar
es Salaam.
Mambo
hayo ni mbali na zile hoja sita, ukiondoa moja ya Zanzibar,
zilizoelezwa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa katika gazeti hili wiki
iliyopita, ikiwa ni matarajio yao kuhusu yatakayojitokeza katika Bunge
linaloanza kesho.
Mambo
mengine yaliyotajwa na wachambuzi wiki iliyopita ni sakata la Akaunti
ya Tegeta Escrow, Hotuba ya Rais John Magufuli, bomoabomoa, Sera ya
elimu bure, uchaguzi wa Zanzibar, Katiba mpya na maagizo mbalimbali ya
mawaziri.
Kufutwa
kwa uchaguzi Zanzibar ndiyo linaonekana suala kubwa baada ya Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuitangaza Machi 20 kuwa siku ya marudio ya
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Kurudiwa kwa uchaguzi huo kunapingwa na CUF na vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.
Wabunge
wa Ukawa walipiga kelele wakitaja jina la mgombea urais wa CUF, Maalim
Seif Sharif Hamad wakati mpinzani wake, Rais Ali Mohamed Shein akiingia
kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kusikiliza hotuba ya Rais John
Magufuli Novemba 20, mwaka jana.
Zanzibar
Suala
la Zanzibar linakolezwa zaidi na kikao kati ya Maalim Seif na aliyekuwa
mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa waliotarajiwa kufanya
kikao na wabunge wa Ukawa katika ukumbi wa African Dream jana jioni
mjini Dodoma.
Jana
kwa nyakati tofauti wabunge wa Ukawa walisita kuzungumzia suala hilo,
huku wakishauri watafutwe viongozi wakuu ili kutoa ufafanuzi, hali
iliyoashiria kuwa wanasubiri maazimio ya pamoja ya Ukawa ambayo
yametajwa kuwa ndiyo utakuwa msimamo wao wa mwisho kuhusu suala hilo.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliliambia gazeti hili
kuwa msimamo wa vyama vinavyounda umoja huo ni kutoshiriki uchaguzi wa
marudio.
Alisema
kitakachoikumba Zanzibar kwa kulazimisha uchaguzi huo kitamfikisha Rais
wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif
Ali Idd na mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha mahakamani.
CUF
ambayo inapinga kurudiwa kwa uchaguzi huo, imepanga kufanya vikao vyake
vya juu mapema wiki hii kuweka msimamo wake kuhusu tangazo la tarehe ya
uchaguzi. Vikao hivyo vitaanza Jumatano.
Muundo Kamati za Bunge
Suala
jingine ambalo linaonekana litaibua mjadala katika bunge hilo ni jinsi
Ukawa inavyopinga wajumbe wa kamati mbalimbali za bunge walivyoteuliwa
na hata kusababisha wasusie uchaguzi wa viongozi wa kamati hizo.
“Wasemaji
wote wamepelekwa kamati ndogo. Serikali inataka kuliendesha Bunge.
Hatuhukumu watu lakini unapowaweka katika kamati moja wabunge waliokuwa
vinara katika kamati za Bunge lililopita ni ishara ya kutaka kuficha
mambo fulani,” alisema Halima Mdee, mbunge wa Kawe kwa tiketi ya
Chadema.
Mdee
alisema wabunge makini, wenye tabia ya kuibua mijadala na hoja kubwa
wamepelekwa katika kamati ambazo hazijadili masuala makubwa ya kitaifa.
Siku
tatu zilizopita Bunge lilitangaza wajumbe wa kamati za Bunge, huku
likiunda kamati mpya mbili, kubadilishwa majina na nyingine kuunganishwa
baada ya Rais Magufuli kupunguza idadi ya wizara kwa kuziunganisha.
Uteuzi
huo wa wajumbe wa kamati uliofanywa na Spika wa Bunge, Job Ndugai
ulilalamikiwa na wabunge mbalimbali, huku wale wa Ukawa wakisusia
uchaguzi wa viongozi wa kamati hizo, zikiwamo za Hesabu za Serikali
(PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), ambazo wenyeviti wake
lazima watoke upinzani.
Licha
ya kamati zote kupata viongozi wake, kamati ya PAC na Laac ambazo
lazima ziongozwe na upinzani, hazijapata wenyeviti baada ya wabunge wa
Ukawa kususia uchaguzi.
Moja
ya kamati zilizowahi kutikisa nchi ni ya PAC ambayo ilifichua ufisadi
mkubwa serikalini kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali na Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Unapowapeleka
watu hawa (wabunge wadadisi) katika kamati ambazo zitawafanya wakose
hoja kubwa za kuchambua na kudadisi kinachoendelea ndani ya nchi ni kama
kulifanya Bunge kuwa kibogoyo,” alisema Mdee.
“Serikali
imeingilia kwa kiasi kikubwa kupanga majina ya wajumbe wa kamati.
Tunajua lilikuwa ni agizo nani akae wapi na nani awekwe wapi. Hili
tutalisema maana hata Spika (Ndugai) hakuweza kufanya lolote, ‘list’
nzima alipelekewa, alichokifanya ni kuitangaza,” alidai Mdee.
Hata
hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe
aliwashutumu wabunge wa Ukawa na kusisitiza kuwa kamati zote zipo sawa
na hakuna kamati iliyo bora zaidi.
“Twendeni
kwenye hizi hizi kamati tulizopangiwa kuwafanyia kazi Watanzania,
twendeni tukaonyeshe kuwa Bunge litabaki kuwa Bunge tu. Wabunge
tusikubali Bunge Kibogoyo, ni lazima Bunge lidhibiti Serikali hata
Serikali hiyo ikiwa inaongozwa na Malaika,” alisema Zitto.
Upinzani kuzuiwa mikutano
Mbunge
wa Kibamba (Chadema), John Mnyika alisema kitendo cha Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa kuzuia mikutano ya hadhara ni kinyume na Katiba ya nchi
inayompa mwananchi uhuru wa kukusanyika na ni kinyume na sheria ya vyama
vya siasa.
Desemba
25, mwaka jana, Majaliwa alisema wanasiasa walioshindwa kwenye Uchaguzi
Mkuu hawaruhusiwi kuitisha mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuwashukuru
wananchi kwa kuwa wanaweza kuvuruga shughuli za maendeleo.
Alisema
wakati wa siasa umekwisha na sasa ni wakati wa kufanya kazi za
maendeleo, hivyo Serikali haitaki tena kuona wanaibuka watu kuvuruga na
kwamba mikutano ya shukurani itafanywa na wale tu walioshinda kwenye
maeneo yao.
“Lazima
tumbane bungeni, kwanza kwa kauli yake kama waziri mkuu, lakini pili
kama kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni. Lazima tumbane atueleze
kuhusu suala hili kwa kina ili tujue alikuwa akilenga nini,” alisema
Mnyika.
Alisema
kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, chama chochote cha siasa
kufanya mikutano ni sehemu ya kazi yake, hivyo kukizuia kufanya hivyo ni
kukizuia kufanya shughuli zake zilizopo kisheria.
Uchaguzi wa meya Dar
Mdee
alisema Ukawa watatumia mjadala wa hotuba ya Rais Magufuli kuhoji
uhalali wa kuahirishwa kwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
uliokuwa umepangwa kufanyika Jumamosi iliyopita.
“Wizara
ya Tamisemi ipo chini ya ofisi ya rais na kimsingi kuahirishwa kwa
uchaguzi huu ni lazima rais atakuwa anajua kinachoendelea. Hili
linafanyika wakati sheria zipo wazi na zinaeleza kila kitu juu ya
masuala ya kufuatwa,” alisema Mdee.
Wakati
madiwani wa Ukawa wakijipanga kwa uchaguzi huo, Halmashauri ya Jiji
ilitoa taarifa ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo bila kueleza sababu za
kufanya hivyo, zaidi ya kusema tu utafanyika katika siku itakayotangazwa
baadaye.
“Kunapokuwa
na dhamira ya kutaka kuchelewesha uchaguzi huu na ukirejea mbinu chafu
walizofanya katika uchaguzi wa meya wa halmashauri ya Ilala na
Kinondoni, utabaini kuwa kuna mchezo unachezwa,” alisema Mdee.
Alibainisha
kuwa uchaguzi huo umekumbwa na ‘figisufigisu’ kwa sababu CCM wanaogopa
Ukawa kufumua madudu ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) na huduma
ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka (Uda RT).
“Miradi
ya Uda na Dart ipo chini ya Jiji na sisi tukiingia ni lazima kuna vitu
lazima vijulikane kiini chake na uhalali wa mchakato wake. Naona kuna
hofu kuna uchafu uliofanywa Jiji lilipokuwa chini ya CCM unawapa tabu.
Wanajua ikipata nafasi itafumua mikataba yote ya Uda,” alisema.
Alisema
nyuma ya pazia ya miradi hiyo kuna vigogo wa CCM na watoto wao na ndio
sababu ya kufanyika kwa mizengwe. “Ndiyo maana hawatoi sababu za msingi.
Ninachokiona hapa ni Rais Magufuli kuogopa aibu ya Serikali yake.
Hatuwezi kukwepa kulizungumza jambo hili,”alisema. Hata hivyo,
Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Simon Group, Robert Kisena mwishoni
mwa wiki alisema hakuna kigogo au familia ya kigogo wa serikali au CCM
mwenye ubia katika umiliki wa Uda.
Mwenyekiti
huyo alisema nje ya familia yake, mtu mwingine mwenye hisa tano ni
waziri wa zamani, Profesa Juma Kapuya na akasisitiza kuwa kampuni yake
ya Uda RT ndiyo itakayoendesha mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini
Dar es Salaam.
Tayari
wabunge wa CCM na Ukawa wapo bungeni na wamekuwa wakifanya vikao
mbalimbali vya ndani kwa lengo la kuwekana sawa kabla ya kuanza kwa
bunge hilo kesho.
Kauli za wasomi
Mhadhiri
wa UDSM, Richard Mbunda alisema jambo ambalo lina uzito wa kujadiliwa
bungeni ni lile la Majaliwa kukataza vyama vya siasa kufanya mikutano ya
kuwashukuru wananchi baada ya uchaguzi na mengine ni ya kawaida.
“Suala hilo ni muhimu kwa sababu linakandamiza demokrasia hasa kwa vyama vya upinzani,”alisema Mbunda.
Pia,
aligusia muundo wa kamati za Bunge kuwa hiyo ni ishara kuwa Serikali
imejipanga kutengeneza mazingira ya kutaka sera zake zipite bila
vikwazo.
“Hata
kwenye mchakato wa naibu spika tuliona…ila kama ni kwa nia njema basi
yale yatakayopitishwa na kamati yatakuwa mazuri kinyume na hapo wananchi
wataumia,”alisema Mbunda.
Kwa
upande wake, Makamu Mkuu mstaafu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine
(Saut), Dk Charles Kitima alisema kwa kuwa Bunge linaongozwa na sheria,
linapokwenda kujadili masuala hayo lazima lizingatie hilo.
“Tunategemea masuala yatakayokwenda kujadiliwa yatazingatia utawala wa sheria,”alisema Dk Kitima.
Alisema
Tanzania imekuwa ikifanya maamuzi yake bila kuwagawa wananchi, hivyo
hata Bunge katika maamuzi yake kuhusu masuala hayo lazima lizingatie
yale ya kuwaunganisha wananchi.
Mbali
na hilo, alisema mijadala mingine pia inatakiwa kujikita katika
changamoto mbalimbali zilizopo kama ajira na kukuza uchumi wa Taifa.
“Tunafahamu
hapa Tanzania, utaifa kwanza na mengine baadaye. Wakajadili mambo yenye
manufaa kwa wananchi waliowapa dhamana ya kuwawakilisha bungeni,”
alisema.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alianza kwa
kuzungumzia muundo wa kamati za Bunge na kusema kuwa kujadili suala hilo
ni kupoteza muda wa kujadili mambo muhimu.
Dk Bana alisema anaamini uchaguzi huo uliofanywa chini ya Spika ulizingatia kanuni, hivyo jambo hilo si la kujadiliwa.
Kuhusa
suala za Zanzibar, alisema hilo bado lina ukakasi na utata, lakini
kinachotakiwa ni kuendelea kwa mazungumzo baina ya viongozi wa visiwani
humo huku uchaguzi ukisubiriwa.
No comments:
Post a Comment