27 December 2015

SIMANZI;HIVI NDIVYO MLINZI ALIVYOFIA GESTI,SOMA HAPA KUJUA KISA

 Polisi akiupiga picha mwili wa marehemu.
SIMANZI! Ramadhan Mohamed Duku (52), mkazi wa Mji Mpya mjini hapa amekutwa akiwa amekufa kwenye nyumba ya kulala wageni (gesti) aliyokuwa akiilinda hivyo kuibua taharuki kubwa kwa wateja waliolazimika kutoka nduki na kuwaacha michepuko waliokuwa nao vyumbani.

Tukio hilo lililoibua utata juu ya kifo hicho, lilijiri wiki iliyopita katika Gesti ya Uswaa iliyopo maeneo hayo ya Mji Mpya ambapo mwanaume huyo huwa ni mlinzi wa kujitegemea aliyekuwa akilinda gesti mbili tofauti.
 Wafiwa wakilia kwa huzuni kubwa.

Ilielezwa kwamba, mchana alikuwa akilinda gesti iitwayo Simtu Baba iliyopo Stendi ya Daladala ya Mji Mpya na usiku alikuwa akilinda Gesti ya Uswaa iliyopo maeneo hayohayo jirani na soko ambako ndiko alikokutwa na umauti.

Akiwa kwenye misele ya kutimiza majukumu yake ya kikazi, majira ya saa 2:00 usiku, mwanahabari wetu alifika kwenye gesti upande wa baa na kuzungumza na jamaa huyo aliyeonekana kuwa na afya njema akifuatilia taarifa ya habari ya runingani kuhusu Rais John Pombe Magufuli anavyowanyoosha watumishi wabovu serikalini.

Katika hali ya mshangao, asubuhi yake, mwandishi wetu alipigwa na butwaa alipopigiwa simu na mmoja wa wahudumu wa gesti hiyo akimjulisha kutokea kwa kifo hicho.

 Mwili wa marehemu ukitolewa ndani ya gest hiyo.

Mwandishi wetu alifika eneo la tukio na kushuhudia umati ukiwa nje ya gesti hiyo huku geti likiwa limefungwa na funguo alikuwa nazo marehemu hivyo wageni kushindwa kutoka na wengine kuruka ukuta wakidaiwa kuikimbia michepuko yao na kuogopa kutoa ushirikiano kwa polisi.

Muda mfupi baadaye, polisi walifika eneo la tukio na kuruka ukuta kisha kumkagua marehemu ambapo walifanikiwa kumkuta na funguo mfukoni ndipo wakafungua geti na kuwataka wateja wote waliokuwa ndani ya gesti hiyo kwenda kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo huku ndugu wa marehemu waliofika eneo hilo wakiangua vilio na kugaragara chini.

 Watu wakiwa nje ya gesti alimofia.

Baadaye polisi waliwaachia wateja hao ambapo waliuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro huku uchunguzi wa kifo hicho cha ghafla ukiendelea kubaini chanzo chake.

Akizungumza na gazeti hili, mmiliki wa gesti hiyo, Alnod Ndossi alithibitisha mlinzi wake kufa ghafla akiwa kazini huku akiacha mke na watoto watatu.

Mmoja wa wateja waliokuwa kwenye gesti hiyo waliozungumza na mwandishi wetu juu ya tukio hilo, Ally Shomari alikuwa na haya ya kusema:

Mwili wa marehemu ukipakizwa kwenye gari.

“Nilipofika kwenye gesti hii majira ya saa 4:00 usiku nilimkuta jamaa akiendelea na majukumu yake ndipo nikaingia kulala. Nilishtuka kusikia watu wakiruka ukuta na nilipotoka nikakuta jamaa amekata roho akiwa amekaa kwenye kiti pembeni mwa mlango wa vyumbani.”

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname