Agizo la Rais Dk. John Magufuli kuwabana wafanyabiashara wanaokwepa
kodi nchini, limeanza kuwa mwiba baada ya mabasi ya Kampuni ya
Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), kukamatwa kutokana na kukwepa kodi.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Richard Kayombo, jana alisema mabasi tisa ya UDA
yalikamatwa kutokana na kukiuka sheria za mlipakodi.
Mbali na UDA, Kayombo alisema TRA pia iliyakamata mabasi ya kampuni
nyingine kutokana na kushindwa kulipa kodi ambapo walitumia kampuni ya
udalali ya Majembe Auction Mart.
Kayombo alisema operesheni ya TRA kuwakamata wafanyabiashara wanaokwepa
kodi ni endelevu nchi nzima na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa kwa
wanaokaidi kutekeleza sheria.
Hata hivyo, Kayombo hakutaka kuzungumzia kwa undani kuhusu kiwango cha
kodi ambacho hakikulipwa na UDA, akidai kuwa hiyo ni siri ya mlipakodi
na mamlaka yenyewe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDA, Robert Kisena, alithibitisha
kukamatwa kwa mabasi yake ambayo alisema uzembe huo ulifanywa na idara
yake ya uhasibu.
Kisena alisema muda wa kulipia kodi ulikuwa umefika, lakini idara yake ya uhasibu haikuweza kulipa viwango vinavyotakiwa.
“Ni kweli kuna magari yetu matatu au manne yamekamatwa na tatizo
kubwa ni kodi ya magari, ambayo tulijua mtu wetu wa uhasibu amelipa,
lakini kumbe alikuwa hajalipa,” alisema Kisena huku akisisitiza kuwa
taratibu za kuyakomboa magari hayo zimefanyika ambapo wamekwishalipia
gharama zilizokuwa zinahitajika
No comments:
Post a Comment