WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwa ndio kwanza imelikabidhi
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa vyama vya siasa na wadau wengine wa
uchaguzi, ili kufanyiwa uhakiki, uchunguzi umeonesha daftari hilo ni
chafu na haliaminiki. Anaandika Charles William … (endelea).
Siri hii inafichuka siku tisa tu kabla ya Oktoba 25 ambapo Watanzania wapatao milioni 22 wanatarajiwa kujitokeza vituoni kupiga kura ya kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Wabunge na Madiwani.
Kwa Zanzibar, kutakuwa pia na uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Waakilishi na Madiwani.
Hatua hiyo inakuja siku moja tangu Tume ya Uchaguzi iruhusu vyama vya
siasa kuchukua daftari hilo ndani ya shinikizo kubwa za viongozi wakuu
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Mbele ya waandishi wa habari leo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Abdallah Safari pamoja na
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Reginald Munisi, walisema
kumebainika “madudu na upungufu mwingi kwenye daftari. Kwa hakika
haliaminiki.”
“Tumeanza kulifanyia ukaguzi daftari la Tume baada ya kulipata jana
Jumatano, na kwa tuliyoyaona, sasa tumeelewa ni kwanini walikuwa
hawataki kulitoa mapema,” amesema Prof. Safari ambaye ni wakili wa
Mahakama Kuu nchini.
“… ni wazi Tume hii ambayo si tume huru imejiandaa kuhujumu uchaguzi kwa
kuwa katika kituo kimoja tu tulichokagua tumeona majina feki mengi
yakiwa yameingizwa,” ameongeza Munisi ambaye amesema ukaguzi ulifanywa
katika jimbo la Dodoma mjini.
Dosari za msingi zilizobainika katika ukaguzi huo ni
- Majengo kuandikishwa kama wapiga kura. Katika hali ya kushangaza picha za majengo, ikiwemo migahawa zimeonekana kuwa ni sehemu ya majina ya wapigakura wa jimbo la Dodoma Mjini huku zikibeba majina ya watu na namba ya kitambulisho cha mpiga kura.
- Baadhi ya vitambulisho kuonekana vikiwa na picha mbili: kumekutwa baadhi ya vitambulisho vinachoandamana na picha ya halisi za watu wengine nyuma.
- Raia wa kigeni kuandikishwa: Kumekutwa majina ya wasiokuwa raia wa Tanzania wamejumuishwa kwenye daftari, majina mengine yakiwa yasiyoeleweka; picha za raia wanaoonekana kuwa wageni kama Wachina na Wazungu zimeonekana zikiwa sehemu ya wapigakura wa Tanzania; na majina yenyewe yana herufi tupu zisizo na irabu na hivyo kushindwa kusomeka. Kwa mfano limekutwa jina lililoandikwa LHPG SVWTN.
- Picha za pikipiki kutokeza kama majina ya wapigakura: kumekutwa picha za pikipiki zikiwa ni sehemu ya majina ya wapigakura huku majina na picha hizo yakiwa na namba za vitambulisho vya wapigakura.
- Majina yalioainishwa kuwa ni ya wanaume yana picha za wanawake: baadhi ya majina yalioneshwa kuwa ni ya kiume na kitambulisho kuonesha kuwa jinsia inayomiliki kitambulisho ni ya kiume lakini picha ni za wanawake.
- Picha za wapigakura kupigwa katika maeneo tofauti ikiwemo sehemu zenye mabati na mbao badala ya kitambaa kimoja kilichokuwa kikitumiwa kwenye vituo vya Tume:picha za baadhi ya wapigakura zimeonekana kwa mwonekano tofauti wa nyuma (background), ikiwemo kupigwa kwenye sehemu za mabati na mbao hivyo kuzua hofu kuwa huenda uandikishwaji uliendelea katika maeneo mengine baada ya muda wa uandikishaji kumalizika.
Prof. Safari amesema kufuatia uchafu wa daftari, wanaandaa barua kwenda
jumuiya za kimataifa ili kuzitahadharisha namna ambavyo serikali ya
Chama Cha Mapinduzi inavyoshirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kuvuruga uchaguzi.
“Leoleo tunaandika barua na kuzituma mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa
kivita ICC, tunaipelekea pia Jumuiya ya Madola, Umoja wa Ulaya, Umoja
wa Afrika pamoja na Umoja wa Mataifa kuwajulisha waone mbinu chafu za
CCM kutafuta ushindi wa goli la mkono… wanajiandaa kuiingiza nchi katika
machafuko,” ameeleza Prof. Safari.
Munisi amesema wanaitaka tume ya taifa ya Uchaguzi kutoa majibu juu ya
daftari hilo na kulirekebisha haraka sana kabla hawajatangaza uamuzi
mwingine watakaouchukua iwapo hawataridhishwa na hatua za NEC.
Source: Mwanahalisionline

No comments:
Post a Comment