
Maxmillian Rafael Msacky (wapili kushoto) na Patrick James Natala (wa tatu kulia) wakiwa mahakama ya kisutu jana Ijumaa.
Watu wawili, Patrick Natala
na Maxmillian Msacky wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 10 yakiwamo ya kughushi,
kutengeneza tovuti feki na mifumo ya mtandao kwa kutumia majina ya
Taasisi, viongozi na wanasiasa.
Akiwasomea hati ya mashtaka
jana Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawa akishirikiana na Wakili
Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Johannes Kalungura walidai kuwa washtakiwa hao
walitengeneza tovuti feki kwa kutumia majina ya Taasisi ya Jakaya
Kikwete Foundation (Ikulu), TCRA Foundation, Akiba Saccos Social
Company, Social Credit and Loans Company, Ridhiwani Social Company, Hisa
Tanzania, Zitto Kabwe Foundation, Vicoba Tanzania na Wekeza Fund.
Mutakyawa alidai kuwa
washtakiwa hao wametengeneza tovuti hizo feki kati ya Januari na Aprili
2014 jijini Dar es Salaam kinyume na kifungu cha 122 (b) cha sheria ya
Kielektoliniki na Mawasiliano ya Posta namba 3 ya 2010.
Mbali na mashtaka hayo,
Mshtakiwa Msacky yeye anadaiwa kuwa kati ya 2006 na 2024 kwa njia ya
udanganyifu alighushi cheti cha Sekondari namba 0421130 chenye indexi
namba S 0260-0001.
Iliendelea kudaiwa kuwa
kati ya 2005 na 2014 mshtakiwa huyo alighushi cheti kingine cha
Sekondari namba 0217951 chenye indexi namba S 0310-0532,akionyesha ni
halali na kwamba vimetolewa na Baraza la Mitihani Tanzania wakati akijua
kuwa ni uongo.
Washtakiwa hao walikana
mashtaka na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika
na washtakiwa walipelekwa rumande hadi Septemba 28, 2015 itakapotajwa.
Akizungumzia tukio hilo,
Mkurugenzi wa Sheria wa TCRA, Elizabeth Nzage alisema kati ya Aprili na
Juni katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 walipata malalamiko toka kwa
wananchi kuhusu kuwepo kwa makampuni feki yaliyokuwa yakidai kuwa
yanatoa mikopo kwa muda mfupi.
Nzage alidai kuwa wahusika
hao walitumia majina ya wanasiasa na pia kujifanya ni viongozi na
wamiliki wa taasisi hizo na kwamba makumpuni hayo yanaandaa shughuli za
kuchangisha fedha.
No comments:
Post a Comment