Mgombea Ubunge kwa tiketi
ya Chadema Jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi akiwa sambamba na dereva
wake akibishana na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi baada ya kuvamia eneo
lao la mkutano wa kampeni za Ubunge katika kata ya Ghana.
Baadhi ya viongozi wa CCM
wakimsihi Joseph Mbilinyi kutoendelea na safari yake na badala yake
ageuze lakini bado aliendelea na maamuzi yake.
Wanachama wa CCM waliokuwa kwenye mkutano wa kampeni wakilizuia gari la Joseph Mbilinyi kupita katika eneo hilo
Joseph Mbilinyi akiwasili eneo ambalo CCM wanafanyia mkutano na kukutana na umati wa wanaccm waliomzuia kupita
WATU 9 wamejeruhiwa na gari
na pikipiki kuharuibiwa vibaya kutokana na vurugu zilizotokea baina ya
wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) na Chama cha
Mapinduzi(CCM).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya, Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza
kuwa lilitokea juzi majira ya saa kumi na moja jioni eneo la Mbata –
Buchani, Kata ya Ghana jijini hapa.
Alisema tukio hilo
lilitokea wakati mgombea ubunge Jimbo la Mbeya mjini kwa tiketi ya CCM,
Sambwee Shitambala akiwa na wafuasi wake, wapenzi wa chama hicho alikuwa
akifanya mkutano wa kampeni katika eneo hilo kwa mujibu wa ratiba yake.
Alisema mgombea huyo akiwa
katika mkutano huo, mgombea ubunge jimbo la Mbeya mjini kwa tiketi ya
Chadema Joseph Mbilinyi alikuwa akipita eneo hilo akiwa na msafara wake
kuelekea maeneo ya Nsoho kwenye mkutano wa kampeni.
Kamanda Msangi alisema
kutokana na kitendo hicho wafuasi wa CCM ambao walionekana kuwa wengi
hadi eneo la barabara hivyo kupelekea msafara wa Mbilinyi kutoweza
kupita eneo hilo hali iliyopelekea kuzuka kwa vurugu zilizopelekea
kujeruhiwa kwa watu na uharibifu wa mali.
Aliwataja majeruhi wa vyama
hivyo vya siasa kuwa ni Robert Kerenge (58) Katibu wa CCM Wilaya ya
Mbeya, Salum Mwansasu (35) mkazi wa Majengo (CCM), Atupele Brown (39)
mkazi wa Ghana (CCM), Rose Nelson (30) mkazi wa Majengo (CCM),Sakina
Salum (25) mkazi wa Ghana (CCM), Malanyingi Matukuta (31) mkazi wa
Forest (CCM), Agabo Mwakatobe (44) mkazi wa Ghana (CHADEMA), Jailos
Mwaijande (23) mkazi wa Itiji (CHADEMA) na Gabriel Mwaijande, dereva wa
mgombea Ubunge (CHADEMA).
Kamanda Msangi aliongeza
kuwa katika vurugu hizo gari la mgombea ubunge jimbo la Mbeya mjini kwa
tiketi ya Chadema Joseph Mbilinyi aina ya Toyota land cruiser yenye
namba za usajili T161 CPP liliharibiwa kioo cha mbele, taa moja ya nyuma
upande wa kushoto na kioo cha upande wa dereva kwa kupigwa mawe.
Alisema pia pikipiki zenye
namba za usajili T332 CHV aina ya T-better na T383 CSE aina ya Skymark
ziliharibiwa kwa kuvunjwa side mirror za upande wa kushoto na zipo kituo
cha polisi kati.
Aliongeza kuwa kwa mujibu
wa ratiba ya kampeni za uchaguzi iliyotolewa na Halmashauri ya Jiji la
Mbeya kwa tarehe 17.09.2015, ilikuwa ikionyesha Chadema saa 4 asubuhi
hadi saa 9 alasiri walitakiwa kufanya mkutano Kata ya Nsoho na saa 9
alasiri hadi 12 jioni walitakiwa kufanya mkutano Kata ya Maendeleo
wakati Ccm kwa mujibu wa ratiba walitakiwa kufanya kampeni Kata ya
Itende saa 2 asubuhi hadi saa 7 mchana na saa 7 mchana hadi saa 12 jioni
mtaa wa Mbata, Kata ya Ghana ambapo tukio hili lilipotokea.
Alisema upelelezi
unaendelea ikiwa ni pamoja na kupeleka jalada la uchunguzi kwa
mwanasheria wa serikali ili waliohusika katika vurugu hizo wafikishwe
mahakamani.
No comments:
Post a Comment