28 May 2015

RAMADHANI SINGANO: SIUTAMBUI MKATABA ULIOPO SIMBA NA TFF


MESSI 6
Singano akiwa nyumbani kwao jana wakati wa mahijiano maalumu na mtandao huu
STORI kubwa ya michezo nchini kwasasa ni sakata la mkataba wa kiungo mshambuliaji, Ramadhan Singano ‘Messi’ na klabu yake ya Simba.
Kuna sintofahamu kubwa kwasababu Singano anadai amemaliza mkataba, wakati Simba na TFF wana mkataba unaoonesha ana mwaka mmoja zaidi katika mkataba wa miaka mitatu aliosaini  mei 1 mwaka 2013.
Singano yeye anadai alisaini mkataba wa miaka miwili mei 1 mwaka 2013 na unatakiwa kumalizika Julai 1 mwaka 2015, lakini Simba wao wanadai mkataba wake utaisha  Julai 1 mwaka 2016.
Kuna sakala la ku-foji mkataba baina ya Singano na klabu yake ya Simba, nani kahusika?, fuatilia sinema hii.
MAELEZO YA RAMADHANI SINGANO ‘MESSI’
Singano anasema: “Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili mwaka 2013, wiki mbili baadaye nilichukua nakala ya  mkataba wangu na kwenda nayo nyumbani.
Baada ya mwaka kuisha tangu nisaini mkataba, nikaitwa timu ya taifa, lakini mwezi wa saba (2013), nikapewa taarifa kwamba kuna mkataba wa miaka mitatu TFF, nikafuatilia na kupata nakala yake na nilipoangalia nikakuta kweli kuna miaka mitatu.
Tukirudi nyuma kidogo kwenye mkataba wa kwanza wa miaka miwili,  kuna vipengele ambavyo zikutimiziwa, ikabidi niandike  barua tarehe 13 mwezi wa pili 2013 kwenda kwa uongozi (utawala wa Aden Rage) kuwaeleza kuwa kuna stahiki zangu sijapata,  lakini sikupewa majibu yoyote,  nikaendelea kufanya kazi bila kuingia kwenye vyombo vya habari.
Baada ya uongozi kuondoka, nikakutana na uongozi wa Rais  Aveva (Aveva), nikaongea na makamu wa Rais  (Geofrey Nyange Kaburu) kuhusu madai yangu, akaniambia haina shida watalifanyia kazi.
 Baada ya ligi kusimama mwezi wa 12 mwaka jana tulikuwa tupo Gym, nikamwambia Kaburu  kuhusu barua niliyoandika kudai stahiki zangu. Alichonijibu hata mimi nilishangaa, aliniambia mchezaji mzawa huwezi kulipwa kodi ya nyumba, nikasema hakuna shida, lakini kubwa likawa ni mkataba wa miaka mitatu, nikamwambia, hili mbona silifahamu?  Nipe ufafanuzi kwasababu mimi nina mkataba wa miaka miwili.
Kikubwa alichoniambia ni kwamba subiri ligi imalizike tutaongea juu ya hilo. Baada ya ligi kuanza mzunguko wa pili ikabidi nipeleke vielelezo kwanza na nikaandika barua kuwapa taarifa.
 Niliandika barua ya kwanza mwezi wa tatu (2015) ambayo niliwaambia kuhusu malalamiko yangu ya mkataba wa miaka mitatu wakati mimi nina mkataba wa miaka miwili, nilimuandikia Rais Aveva.
Nikajibiwa barua ya hiyo  na katibu mkuu wa klabu (Stephen Ally) akithibitisha kupokea barua yangu ya malalamiko na akanitaka nimpelekee nakala ya mkataba ili alinganishe na ile waliyokabidhiwa,  baada ya hapo aondoe sintofahamu iliyopo upande wangu.
Baada ya kupokea barua hii kutoka kwake nikaisoma na kuandika barua nyingine tarehe 31 mwezi wa tatu 2015 na kuambatanisha nyuma nakala ya mkataba wangu na kumpekelea kama alivyonitaka kwenye barua yake ya nyuma ambayo ilisema tutamaliza kwa muda mfupi sintofahamu yangu, lakini wakakaa kimya  mapaka leo hii tunavyoongea (jana).
Kabla ya ligi kuisha nikaitwa tena ofsini tarehe 13 mwezi wa tano mwaka huu (jumatano), nikaonana na makamu wa Rais Nyange Kaburu. kwanza kabla ya yote tukaongelea mkataba, alikiri na mwenyezi mungu ni shahidi, akasema mkataba wao wa kwanza una makosa. Alivyodai ni kwamba karatasi yao ya kwanza inaonesha ni 2015 na ya pili 2016. Nikamwambia hilo la 2016 silifahamu, nimekuja hapa kuongelea mkataba mpya kwasababu nimeshamaliza mkataba wangu.
 Wakaleta mkataba mpya bila hata ya kujibu barua yangu. kubwa sio kama watu wanavyofikirIa, watu wanadanganywa kwamba mimi nina tamaa ya hela,  kwanza ni kumalizana kuhusu mkataba huu wa miaka mitatu, wakati mimi ninaujua wa miaka miwili”.
MESSI 2
MAPUNGUFU YA MKATABA MPYA KWA MUJIBU WA MENEJA NA KAKA YAKE RAMADHANI SINGANO, HAMIS RAMADHANI
Hamis Ramadhani ambaye  pia ni kaka yake wa damu wa Singano (Mama mmoja, baba tofauti), anafunguka: 
“Kitu anacholalamikia Ramadhani, bila kujali kama Simba watamsajili au hapana,  wala hafungi milango kwa Simba ni mkataba. Simba wanatakiwa watambue kwamba, mkataba mpya walioleta una mapungufu mengi.
Kwa mfano Simba wanasema Ramadhani ana miaka mitatu, lakini mkataba huu mpya unasema utaanza tarehe 1 mwezi wa sita 2015. Kama kweli Ramadhani  ana mkataba wa miaka mitatu basi unatakiwa kuisha mwakani (2016).  Sasa inakuwaje kama mkataba wa kwanza unaisha mwakani (2016), mkataba mpya uanze tena mwezi wa sita mwaka huu (2016) na kumalizika 2017?
Mkataba huu mpya unaonesha ni wa miaka miwili na utaisha mwaka 2017.  kama kweli Ramadhani ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi na Simba, mkataba mpya wa miaka miwili utaishaje mwaka 2017 badala ya 2018?
Yaani kama bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba,  sahizi akaongeza mkataba wa miaka miwili, basi mkataba wake wote utaisha mwaka 2018 na si 2017.
Chapili ; kuna kipengele ambacho kinaonesha jinsi gani mchezaji atakavyokuwa katika timu na kocha atavyokuwa na mapendekezo juu maslahi yake. Hili pia tumeona ni tatizo kwa Ramadhani. Yeye kama mchezaji anatakiwa kujua kwamba Simba watakapokuja kukatisha mkataba wake, maslahi yake yako  vipi?.
Simba wanasema mchezaji atakapokatishwa mkataba atalipwa kwa kipindi cha mwezi mmoja, swali linakuja, mwezi mmoja atalipwa kiasi gani cha fedha?.  Ukishaisha msimu wa kwanza,  anabakisha mwaka mzima, eti unakuja kumlipa mshahara wa mwezi mmoja mtu aliyebakiza miezi 12, inakuwaje hapo?
Pia kuna kipengele kingine ambacho kinaonesha kwamba kina mapungufu katika mkataba huu, hasa sehemu ya kuvunja mkataba.
Wakati mchezaji atalipwa mshahara wa mwezi mmoja tu akivunjiwa mkataba na klabu, yeye akivunja mkataba na klabu anatakiwa kulipa dola laki sita. Yaani klabu ikivunja mkataba wa mchezaji, analipwa mshahara wa mwezi mmoja, lakini mchezaji akivunja mkataba na klabu, yeye anatakiwa kulipa dola laki sita.  Kipengele hiki tumeona ni kigumu kwa Ramadhani kusaini mkataba huu mpya.
 Lakini  kwanza tunataka kujua mkataba wa kwanza wa miaka miwili una mapungufu gani ili tuyaweke  sawa, tuangalie stahiki zake zipoje na amelipwa au hajalipwa?
MESSI 1
JICHO LA TATU LA MTANDAO HUU
Ukisoma maelezo ya Ramadhani Singano na Meneja wake Hamis Said kuna mkanganyiko wa wazi unaonekana na kuna mtu ame-foji mkataba.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu umebaini kuwa mkataba wa miaka miwili aliosaini Singano ulianza mei 1 mwaka 2013 na unatakiwa kumalizika Julai 1,  2015, lakini ukiwa na kipengele cha kuongeza kutegemeana na namna Simba watavyomuona mchezaji.
Katika mkataba huo wa miaka miwili, kuna stahiki ambazo Singano hajapata mpaka umemalizika kisheria. Kwa mfano kipengele kimoja cha mkataba kinasema mchezaji atapewa shilingi laki sita (600,000) ikiwa pango la nyumba ‘House Allowance’ , lakini haijaelezwa kama itatolewa kwa mwezi au mwaka.
 Hata hivyo Singano hajawahi kupewa pesa hiyo mpaka mkataba wake unaisha. Kumbuka katika maelezo yake alisema kwamba alimwambia Kaburu kuhusu hilo, lakini alimjibu kuwa mchezaji mzawa hawezi kupewa kodi ya nyumbani.  Kama ni hivyo kwanini kipengele hicho kiwepo kwenye mkataba?
Ukiachana na hilo, mkataba wa miaka miwili wa Singano unaeleza kuwa;  kama mchezaji ataitwa mara nyingi timu ya Taifa ataongezewa 25% ya mshahara na imefafanuliwa kuwa klabu itaanza kumtathimini mchezaji  miezi sita tokeo asaini mkataba.
Ukiangalia toka Singano asaini mkataba 1/5/2013 ameitwa mara nyingi timu ya Taifa, lakini anasema mashahara wake haujawahi kupanda kwa 25%. Kiufupi kuna mapungufu mengi katika mkataba huo na mchezaji hajapata baadhi ya stahiki zake muhimu.
TURUDI KWENYE  UTATA WA MKATABA WA MIAKA MIWILI NA MKATABA WA MIAKA MITATU
Singano baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili 2015, inatakiwa tarehe 1/7/2015 umalizike, lakini kikanuni mpaka sasa ni mchezaji huru kwasababu FIFA wanasema mchezaji akibakiza miezi sita kwenye mkataba wake anaruhusiwa kuongea na timu nyingine.
Utata mkubwa  unaonekana katika mkataba wa miaka mitatu uliopo Simba na TFF. Singano amefafanua vizuri kwamba alienda TFF kufuatilia baada ya kuambiwa kuna mkataba wa miaka mitatu. Kweli akapewa nakala yake na uchunguzi wetu umebaini kuwa mkataba huo wa miaka mitatu unaonesha ulisainiwa siku moja na mkataba wa miaka miwili alionao Singano.
Nimesema hapo juu, mkataba wa miaka miwili ambao Singano anadai ni sahihi ulisainiwa 1/5/2013 na unaisha 1/7/2015. Mkataba wa miaka mitatu walionao Simba na TFF ulisainiwa 1/5/2013 na utaisha 1/7/2016.
Mikataba  yote miwili inaonesha sahihi ya Singano na kiongozi mmoja wa Simba. Vipengele vya mikataba hiyo miwili vinafanana kabisa, utofauti ni idadi ya miaka? Swali ni je, huu mkataba wa miaka mitatu uliopo Simba na TFF umeandikwa na nani? Je, Simba wamefoji? Au Singano amefoji? Hapo ndipo utata upo na lazima upatikane kwenye vyombo vya sheria.
MESSI 4
MALALAMIKO YA SINGANO KUTOTIMIZIWA STAHIKI ZAKE KATIKA MKATABA WA MIAKA MIWILI
Mtandao huu umebaini kuwa mkataba wa miaka miwili aliosaini Singano una mapungufu  mengi na ni dhahiri mchezaji hajatimiziwa stahiki zake kwa mujibu wa mkataba huo.
Mchezaji hakukaa kimya kudai haki zake kwani februari 13, 2014 aliandika barua kwenda kwa katibu mkuu wa Simba, akieleza kwamba ni zaidi ya nusu mwaka tangu aingie mkataba na klabu hiyo, lakini hajatimiziwa haki zake za kimsingi zilizoainishwa kwenye mkataba.  Kuna mambo ya msingi alieleza mfano kadi ya Bima ambayo aliahidiwa kupewa kabla ya kuanza kazi. Pia kodi ya nyumba ambayo hakupatiwa tangu wakubaliane , lakini cha kushangaza hakujibiwa barua hiyo.
Lilipofika suala la mkataba wa miaka mitatu ambao Singano hautambui, alichukua hatua za haraka kufuatilia na akapewa nakala ya mkataba huo na TFF.
Machi 10 mwaka 2015 mtandao huu umegundua kuwa Singano aliandika barua kwenda kwa Rais Evans Aveva akitaka ufafanuzi juu ya mkataba wa miaka mitatu uliowasilishwa TFF. Singano alifafanua katika barua yake kuwa mkakaba huo wa miaka mitatu hajausaini na ameshindwa kujua tafsiri halisi ya kitendo hicho.
Katibu  mkuu wa Simba, Stephen Ally alimjibu Singano kwa barua ya Tarehe 13-3-2015, KUM: SSC/12/03/2015/KM . Kikubwa katibu mkuu huyo alithibitisha kupokea barua yake ya malalamiko kwa Rais Aveva kuhusu ualakini kwenye mkataba uliopelekwa TFF na ule ambao alisaini.
Ally alimwambia Singano kwamba suala hilo lilipelekwa kwake kwa ajili ya utekelezaji na akamfahamisha kuwa wakati uongozi mpya unaingia madarakani ulikabidhiwa nyaraka zote za klabu ikiwemo mkataba wa Singano.
Katibu mkuu akasema kinyume na madai ya Singano, mkataba wake waliokabidhiwa ni ule unaoonesha amesaini kuitumikia Simba kwa muda wa miaka mitatu, lakini Singano alikuwa na mkataba wa miaka miwili,  Ally akamtaka kuwasilisha nakala ya mkataba huo ili wamalize mapema tatizo lake.
Haraka sana Singano alikaa chini na kuandika barua machi 31, 2014 akijibu barua ya katibu mkuu, Stephen Ally ya tarehe 13/3/2015 yenye KUM: SSC/12/02/2015/KM ambayo ilimtaka kuwasilisha nakala ya mkataba wake na klabu ya Simba.
Katika barua yake Singano aliambatanisha mkataba wa miaka miwili anaoutambua akitarajia kupata ufumbuzi, lakini tofauti na matarajio yake, hakupata majibu mpaka jana alipokuwa anaongea na mtandao huu.
Cha kushangaza jana hiyo hiyo amepokea barua kutoka Simba yenye KUM 18/05/2015/RL/05 iliyoandikwa na Rais Aveva tarehe 18/05/2015. Barua hiyo ambayo Singano amepokea ni majibu ya barua yake ya 31/03/2015 aliyotuma pamoja na nakala ya mkataba wake wa miaka miwili.
Rais Aveva katika barua hiyo amemueleza Singano kwamba kwa mujibu wa kumbukumbu za klabu pamoja na nakala ya mkataba uliowasilishwa TFF, mkataba wake na klabu ya Simba utamalizika tarehe 1 julai 2016. Hii ni tofauti na nakala ya mkataba aliyoambatanisha Singano kwenye barua yake inayoonesha mkataba wake unaisha Julai mosi, 2015.
BOMU LINGINE KATIKA SAKATA HILO LA MKATABA
Wakati hayo yote yakiendelea, mtandao huu umegundua kuwa klabu ya Kuhnsdorf-Klopeiner See ya Austria ilituma mwaliko Simba ikiomba Ramadhani Singano akafanye majaribio. Barua hiyo ya mwaliko iliandikwa 29.04.2015
Kuhnsdorf katika mwaliko wao walisema majaribio hayo yataanza mei 15, 2015 mpaka angalau juni 30 mwaka huu. Walifafanua kuwa gharama za usafiri wa ndege na kuishi kule, matibabu yote watagharamikia wao wenyewe na wakatumaini kwamba mpaka mei 15 mwaka huu Singano atakuwa amewasili klabuni kwao.
Katibu mkuu wa Simba, Stephen Ally baada ya kupokea barua hiyo ya mwaliko aliandika barua yenye KUMB: SSC/22/2015/05/GS kwenda ubalozi wa Austria Tanzania akieleza kupokea maombi ya klabu ya SK Kuhnsdorf kumtaka Singano akafanye majaribio kwao.
Simba katika barua yao hiyo walieleza kuwa Ramadhan Singano ana mkataba na amealikwa kwenda kufanya majaribio katika klabu hiyo iliyopo maeneo ya Viebba,  Austria, hivyo wanauomba ubalozi wa nchi hiyo hapa Tanzania kumruhusu kusafiri kwenda nchini mwao.
MESSI 3
UTATA MWINGINE HUU HAPA…….
Simba katika barua waliyoandika kwenda ubalozi wa Austria inaeleza kwamba Singano ana mkataba ambao ndio ule wa miaka mitatu unaoisha 2016, lakini ukiangalia kwa jicho lingine, mei 12 mwaka huu 2015, siku mbili kabla ya mchezaji kwenda Austria  kufanya majaribio, walitengeneza mkataba mpya na kumtaka Singano asaini haraka.
Kwa maana hiyo wakati anakwenda Austria walitaka awe na mkataba wa miaka miwili. Katika maelezo ya mkataba huo mpya wa miaka miwili, Simba wameeleza kuwa utaanza rasmi Juni 1 mwaka huu hadi mei 30 mwaka 2017, lakini kuna kipengele cha kuongeza kutegemea na muelekeo wa klabu.
Swali linalotatiza ni kwamba, kama kweli Singano bado amebakiza mkataba wa mwaka mmoja, kwanini Simba walimharakisha kusaini mwingine kabla ya kwenda Austria? Ingawa kisheria unaruhusiwa kuongeza mkataba wakati wowote.
Hata angeenda bila kusaini mkataba  mpya, bado klabu ya SK Kuhnsdorf ingelazimika kuzungumza na Simba ili imsajili kwasababu ana mkataba wa mwaka mmoja zaidi kama wanavyodai.
Kumbuka mkataba wa miaka miwili anaoujua Singano unatakiwa kuisha kabisa 1/7/2015, lakini kikanuni umeshaisha na mchezaji yuko huru. Maana yake kama Singano angeenda Austria na kufuzu majaribio angesajiliwa bure kabisa, Simba wasingepata chochote.
Kwa mazingira haya, unashawishika kusema Simba walijua Singano amemaliza mkataba, hivyo wakalazimika kumtengeneza mkataba mpya haraka ili akienda Austria na kufuzu, wafaidike na biashara hiyo.
Nani aliyefoji mkataba kati ya Singano na Simba?
Endelea kusoma mtandao huu…yapo mengi kuhusu sinema hii…kesho tutakuletea majibu ya  Simba kuhusu sakata hili.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname