20 April 2015

KIUNGO ‘BABU KUBWA’ ANAYELIPWA MILIONI 44 KWA MWEZI TAYARI KUTUA YANGA SC

KIUNGO anayelipwa dola 25,000 za Kimarekani kwa mwezi Etoile du Sahel ya Tunisia, (zaidi ya Sh. Milioni 44 za Tanzania), Mcameroon Franck Kom amesema yuko tayari kutua Yanga SC iwapo wataweza kumlipa mshahara huo.
Kom aliwapoteza kabisa viungo wa Yanga Jumamosi katika mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam timu hizo zikienda sare ya 1-1.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY juzi mjini Dar es Salaam, kiungo huyo aliyekuwa akiichezesha vyema timu yake, alisema kwamba anaweza kuja kucheza Tanzania.

Baada ya mechi Kom alikwenda kwenye benchi la Yanga kusalimiana na wachezaji wa timu hiyo na akatumia muda zaidi kuzungumza na kiungo wa DRC, Mbuyu Twite.
Kom alionyesha kumpenda Mbuyu Twite japo ndiyo walikuwa wanakutana kwa mara ya kwanza siku hiyo na wakapeana mawasiliano.


Alipoulizwa kama anaweza kujiunga na Yanga ikimhitaji, Kom alisema; “Kwa nini hapana, ninaweza kama wataweza kunilipa kama ninavyolipwa Etoile,”alisema mchezaji huyo ambaye wakala wake ni kampuni ya Smart Sports Management inayomilikiwa na Jacques Dongmo. Aidha, Kom aliyetua Etoile mwaka 2011 akitokea Panthere du Nde inayotumia jezi kama za Yanga kijani na njano, ya kwao Cameroon aliyoanza kuichezea mwaka 2009 amesema ndoto zake kubwa ni kucheza Ulaya.
Nacheza Afrika kutafuta nafasi ya kucheza Ulaya, timu yoyote inayocheza haya mashindano ya Afrika, kama inaweza kunilipa vizuri naweza kujiunga nayo,”amesema mchezaji huyo ‘fundi’ mwenye umri wa miaka 23.
Kom ni mchezaji wa timu ya taifa ya Cameroon na alikuwepo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichocheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2010 nchini Angola walipotolewa Robo Fainali na Tunisia.
Credit.Bin Zubeiry

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname