04 March 2015

Collabo 5 za hawa wasanii ambapo mashabiki wa muziki Bongo wanatamani kuzisikia

Miaka kadhaa nyuma kila mtu alikuwa na hamu ya kusikia collabo za mahasimu wawili kwenye Bongo Flava kwa wakati ule. Walikuwa ni washkaji wazuri kutoka Temeke ila baadaye wakaja kuwa maadui wazuri mno.


Mzee wa Busara remix ya Juma Nature aliyempa collabo adui yake Inspector Haroun, ilikuja kubadili vitu vingi mno kwenye Bongo Flava. Ilikuwa ni collabo ambayo watu wengi waliiomba na ikaja bila kutegemewa.

Kila mtu anatamani collabo za aina ile zitokee tena na tena.
Orodha hii inakuletea collabo tano kubwa ambazo mashabiki wengi wanazisubiri kwa hamu mno kwenye Bongo Flava.

Alikiba na Diamond

Zamani walikuwa ni washkaji hivi na usingeweza kushangaa ukisikia Alikiba ndio alimpa ruhusa Bob Junior amsaini Diamond kwenye studio ya Sharobaro records mwaka ule, ni kitu ambacho kilifungua njia nyingi mno kwa Naseeb Abdul pengine bila ‘huruma’ ya Alikiba tungechelewa mno kumjua Diamond.

Ilikuwa habari kubwa wakati fulani pale ilipovuja kuwa Diamond alifuta sauti ya Alikiba kwenye wimbo wake wa Lala Salama huku Alikiba pia akifuta sauti ya Diamond kwenye wimbo wake wa Single Boy.
King Kiba na Chibu Dangote wametengeneza ligi moja kubwa mno kwenye Bongo Flava kuanzia redioni, kwenye runinga mpaka kwenye social network. Ni wasanii wenye fanbase kubwa mno kwenye Bongo Flava ambao mara zote wamekuwa wakiwaunga mkono kwenye kila wanachofanya.

Unadhani ni kitu gani kikubwa zaidi kwenye Bongo Flava zaidi ya hiki!
Leo muziki ni biashara naona kabisa ‘wamanyema hawa wa Ujiji, Kigoma wakiingiza hela nyingi mno kama wakiamua kusahau yaliopita na kufanya collabo moja babkubwaaa ambayo mashabiki wote wanaisubiri kwa hamu na I am sure ita-break the internet zaidi ya picha za utupu za Kim Kardashian!

Joh Makini na Fid Q

Kwa miaka zaidi ya 10 wamekuwa wakicheza ligi ya peke yao kwenye Bongo Hip Hop. Wakati fulani ingeonekana John Simon ndio mkali wa Hip Hop na wakati mwingine ingeonekana Fareed Kubanda ndio mkali kwa upande huo. Kila mtu anaamini mmoja kati yao ndio anastahili crown hiyo, hawajawahi kushuka toka walipopanda mahali walipo.

Joh Makini akitokea Arusha huku Fid Q akitokea Mwanza hatujui kama watakuja kufanya collabo ila ni kitu kinachosubiriwa kwa hamu kubwa mno na mashabiki wao.

Juma Nature na Crazy GK

Hawapo hot kama ilivyokuwa miaka iliyopita, wote wamekuwa wasanii wa kawaida mno. Unakumbuka wakati ule wa East Coast Team vs TMK Wanaume? Walikamata Bongo Flava na kuifanya walivyotaka wao.
Leo GK yupo kwenye headline kwa maisha yake binafsi ya kimapenzi na mtangazaji wa Clouds FM, Diva na sio kimuziki kama ilivyokuwa miaka michache nyuma.

Gwamaka Kaihula anamhitaji mno Juma wasaidiane kutoka shimoni walipojichimbia na kuja kuiteka tena Bongo Flava kama ilivyokuwa kawaida yao. Na ipo wazi collabo moja tu watakayofanya itabadili kila kitu kwenye maisha yao na kuwarudisha kule juu walipokuwa.
Bila shaka collabo hii italeta kitu kipya haiwezi kuwa ni sawa na kumrudisha samaki aliyekufa baharini ili afufuke.

Lady Jaydee na Mwana FA

Alikufa kwa Ngoma, Hawajui, Msiache Kuongea, ni baadhi ya ngoma nyingi mno ambazo walifanya pamoja washkaji hawa wa zamani na kuiteka Bongo Flava kama wanalia vile.

Miaka imepita na ule ushkaji wao haupo tena kama zamani, Unaweza kuwaita maadui au mafahari wawili. Je wanaweza kuamua kuishi kwenye zizi moja na kufuta uadui wao huku wakitengeneza pesa? Tusubiri tuone ila niamini mimi hiki ni kitu kikubwa mno kinachosubiriwa na wote kwenye Bongo Flava.

Nay wa Mitego na Nikki Mbishi

Nikki Mbishi alisusa kwa hasira na kuamua kuacha kabisa muziki baada ya kuona anatumia akili nyingi mno kuandika nyimbo kali ambazo raia wema wameshindwa kumuelewa huku media pia zikishindwa kumpa nafasi eti kwa sababu anaandika mistari migumu mno kueleweka kwa mashabiki, kifupi nyimbo zake zilionekana hazipo kibiashara yaani hazifai kwa mainstream.

Kwa watu wengine, Nay wa Mitego kutoka Manzese anaonekana ni mwana hip hop wa kawaida mno kuwa na mafanikio aliyonayo. Lakini bila uoga, unaweza kumweka Nay wa Mitego kuwa msanii wa hip hop mwenye mafanikio zaidi kwa wakati huu kuanzia kimaisha mpaka kimuziki.

Umegundua kitu chochote kutoka hapo juu? Kama bado ngoja nikusaidie tena. Nikki ni mwana hip hop wa ukweli ukimlinganisha na Nay. Nay Ni mfanyabiashara mzuri ukimlinganisha na Nikki, vipi ushanielewa?

Kama Nikki alitaka kuacha muziki kwa sababu hapati maslahi yoyote basi huu ni wakati wake mzuri mno wa kufuta bifu lake na ‘Neema wa Mitego’ kama anavyomwita na kufanya ngoma moja ambayo itabadili mambo mengi mno kwenye muziki wake. Hiki kitakwenda kuwa kitu kikubwa mno kwa mashabiki wa pande zote za hip hop.

Imeandikwa na Heri Athumani (Twitter @heribest. Twitter @mimiheri na kuhaririwa na Fredrick Bundala

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname