Mwanafunzi mmoja wa kike kutoka Chuo cha Moi huko Eldoret, Kenya
amekutwa amefariki dunia karibu na moja ya hosteli za chuo hicho baada
ya kubakwa na kuuwawa kikatili.
Mwanafunzi huyo inasemekana kuwa ni wa mwaka wa tatu chuoni hapo akichukulia masomo ya Sanaa na Sayansi ya Jamii.
Tukio hilo la kinyama, limetokea usiku wa kuamkia jana na bado polisi
haijawatia hatiani washtakiwa ama wahusika wa tukio hilo. Habari za
mkasa huo zinazidi kuenea kila kona ya chuo, huku taharuki na hofu kubwa
ikizidi kuwapanda wanafunzi wengine wa kike ambao wameamua kupaza sauti
kuuomba uongozi wa chuo hicho kuimarisha suala zima la ulinzi kwa
usalama zaidi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi wa zamani katika chuo hicho,
wamethibitisha kuwa tangu mwaka 2006, kumekuwa na matukio ya aina hiyo
ambapo wanafunzi wengi wamekuwa wakikabwa na wengine kubakwa na watu
wasiofahamika mara moja, hivyo wanafunzi kuwabatiza jina la
‘mashoka’,kutokana na wakabaji kutumia silaha za shoka katika kutekeleza
azma yao.
Hata hivyo vitendo hivyo vilikoma kwa kipindi fulani, kuanzia mwaka
2011, hivyo tukio la jana linaashiria bado kuna kiza kinene kwa maisha
ya wanafunzi chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment