Mshambuliaji mpya wa Yanga, Geilson Santos ‘Jaja’.
Na Mwandishi Wetu
MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Geilson Santos ‘Jaja’, amempiku kwa
mara nyingine mshambuliaji mpya wa Simba, Emmanuel Okwi, safari hii
ikiwa ni katika mshahara wa mwezi.Siku chache zilizopita, Jaja amekuwa
ndiye mchezaji gumzo zaidi hasa baada ya kufunga mabao mawili wakati
Yanga ilipoivaa Azam FC na kuitwanga kwa mabao 3-0 kwenye mechi ya Ngao
ya Jamii.
Umaarufu huo wa Jaja ulifanya amfunike Okwi huku mashabiki wa Yanga
wakiona wamepata mbadala wa kuwapoza baada ya Okwi kurejea Simba,
ghafla.
Kwa mara nyingine, Jaja amezidi kung’ara baada ya mshahara wake
anaochota kwa mwezi Yanga kuwa unazidi ule wa Okwi kwa dola 100 (Sh
168,000).
Simba inamlipa Okwi dola 2,500 (Sh milioni 4.2) na imeelezwa inaweza kumuongeza wakati wa kuingia mkataba mpya.Yanga inatoa dola 2,600 (Sh milioni 4.4) kwa Jaja ambaye mshahara wake unaendana na ule wa Andrey Coutinho.
Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ndiye mchezaji anayeongoza kwa mshahara
‘rundo’ kwa wachezaji wote wa Yanga na Simba kwa kuwa kwa mwezi analamba
dola 3,000 (Sh milioni 5).
Wageni wengine ni Hamis Kiiza anayechukua dola 2,500, sawa na Mbuyu Twite, mwenye uraia wa Rwanda lakini akiwa na asili ya DR Congo.
Wageni wengine ni Hamis Kiiza anayechukua dola 2,500, sawa na Mbuyu Twite, mwenye uraia wa Rwanda lakini akiwa na asili ya DR Congo.
Kwa upande wa Simba, Okwi ndiye anaongoza kwa mshahara huo wa dola
2,500 akifuatiwa na nahodha Joseph Owino anayepokea dola 2,000 (Sh
milioni 3.4), anafuatiwa na Paul Kiongera (dola 1,500), halafu Amissi
Tambwe na Pierre Kwizera wote raia wa Burundi ambao kila mmoja analamba
dola 1,000 (Sh milioni 1.7).
Mishahara ya wachezaji wa Yanga imeonekana kuwa juu zaidi kuliko wale
wa Simba na inaonekana Simba ambayo imepata uongozi mpya, inaanza
kujipanga.
Kabla ya kuingia kwa uongozi mpya, wachezaji wa Simba walikuwa
wakipokea mishahara ya chini zaidi lakini tayari wameanza
kujitutumua.Yanga walianza kuboresha mishahara ya wachezaji wao mapema
na wamekuwa wakisisitiza wataendelea kufanya hivyo.
Timu hizo kongwe mbili na Azam FC ndizo zinaonekana kuwa na mishahara
mikubwa kwa wachezaji wake wa kigeni na angalau wale wa nyumbani.
No comments:
Post a Comment