14 June 2014

FLORA MBASHA AVAMIWA


SIKU chache baada ya tuhuma za ubakaji na mzozo wa familia ya mwimba Injili mahiri nchini, Flora Mbasha na mumewe, Emanuel Mbasha, mambo mengine yameibuka.


Mwimba Injili mahiri nchini, Flora Mbasha
Yaliyoibuka safari hii ni taarifa kwamba, juzikati, Flora alivamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake, Tabata Kimanga jijiini Dar dakika chache baada ya yeye kuingia na gari akitokea mafichoni anakoishi kwa sasa.
Kwa mujibu wa chanzo, siku ya tukio ilikuwa  saa 9.15 alasiri ambapo Flora aliingia nyumbani kwake na kufunguliwa geti kubwa kisha kuingiza gari ndani na geti kufungwa tena.
“Flora aliingia na gari akitokea hotelini anakoishi kwa sasa. Alikuwa ameshaingia na geti likafungwa. Ghafla, watu wakafika na kugonga geti hilo kwa nguvu huku wakisema watalibomoa geti kama wenyeji hao hawatafungua,” kilisema chanzo.Mwimba Injili mahiri nchini, Flora Mbasha akiwa na mumewe, Emanuel Mbasha,
Chanzo kikazidi kudai kwamba, ilibidi Flora apige simu polisi ili wafike kumuokoa yeye na familia yake.
“Polisi wawili walifika haraka sana wakiwa na bunduki na kukuta wale watu wamekimbia maana walimsikia Flora akiongea na polisi kuomba msaada.

“Lakini polisi wenyewe ilibidi watumie nguvu kubwa kugonga geti na kujitambulisha ndipo akatokea Flora na kuchungulia nje kupitia dirisha dogo. Alipowaona polisi akafungua mlango,” kilisema chanzo hicho.
Akihojiwa na polisi hao, Flora alisema watu hao walikimbia na hakuwajua kwa sura wala hawakujitambulisha ni akina nani.

Alizungumza na gazeti hili baada ya tukio, Flora alisema: “Unajua kwa sasa nina hofu sana na nilihisi wale watu walikuwa wakinifuatilia kwa karibu kila sehemu, sasa naogopa kuendelea kuishi hapa, wanaweza kurudi na sijui lengo lao.”
Hata hivyo, baada ya askari hao kuondoka katika eneo hilo, Flora naye aliingia kwenye  gari lake akiwa na mdogo wake na kuondoka.
Mume wa Flora, Mbasha naye yupo mafichoni baada ya kudaiwa kumbaka binti wa miaka 17 ndani ya nyumba yao huku utata ukitawala kuhusu ukweli wa tukio hilo ambalo limeigawa jamii.

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname