Wanamgambo wa Al Shabaab wenye uhusiano na Al-Qaeda,
wamesema kuwa wamepiga marufuku raia wanaoishi katika maeneo
wanayodhibiti kutumia internet.
Wapiganaji hao wametoa onyo kwa kampuni zote zinazotoa huduma ya internet siku 15 kufunga biashara zao.Wanamgambo hao hutumia sheria kali za kiisilamu katika maeneo wanayotawala na kuwakamata watu mara kwa mara kwa tuhuma za kufanya ujasusi.
Internet hutumiwa sana nchini Somalia, taifa ambalo limekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miongo miwili, huku kundi hilo likionekana kuwa kikwazo kikubwa kwa amani.
Kundi la Shebab zamani lilikuwa likitawala katika sehemu kubwa za Kusini mwa Somalia na Kati, lakini likaondoa wapiganaji wake baada ya kushindwa na wanajeshi wa Muungano wa Afrika wanaopambana nao.
Majeshi ya Afrika ikiwemo wanajeshi kutoka Uganda, Burundi na Kenya, tangu hapo wamedhibiti sehemu kadhaa kutoka kwa wapiganaji hao.
Lakini mashambulizi ya kuvizia yanayofanywa na kundi hilo dhidi ya maslahi ya majeshi ya serikali na yale ya kigeni, yameondoa matumaini ya kunusuru taifa hilo kutokana na vita vya miaka mingi.
No comments:
Post a Comment