MASKINI! Stori zilizozagaa mitaani kuhusu mali za aliyekuwa mkali wa
sinema za Kibongo, marehemu Steven Kanumba zinasema kuwa, zimeuzwa na
kampuni aliyoiacha, Kanumba The Great Film imefilisika, Ijumaa Wikienda
linakupa ripoti iliyoshiba.
Habari zinadai kuwa baada ya kifo cha Kanumba Aprili 7, 2012, mali
alizoziacha zinafujwa, hakuna utaratibu mzuri wa kusimamia mamb
na kwamba, uzalishaji wa sinema katika kampuni yake ni mdogo tofauti na enzi za uhai wake.
Chanzo
chetu cha habari ambacho ni mmoja wa wasanii wa filamu Bongo aliye na
ukaribu na familia hiyo, alisema ni kweli kuna tatizo la usimamizi na
uendelezaji wa mali za marehemu lakini akasema ni jambo la kawaida kwa
sababu marehemu ameondoka na mbinu zake.
“Kila mtu ana nyota yake kaka, asikudanganye mtu, lakini pia kila
mmoja ana namna anavyojua kuendesha biashara zake, sasa Kanumba alikuwa
na mikakati yake, hawa walioachiwa nao wana mikakati yao. Mfano,
hawataweza kutoa sinema nyingi kwa sababu soko la waliobaki si kubwa
kama ilivyokuwa kwa Kanumba.
“Angalia hata ushindani... hivi kweli Seth (Bosco, ‘mdogo wa
Kanumba’) anaweza kupambana na magwiji kama JB (Jacob Steven) au Ray
(Vincent Kigosi) sokoni? Watu waache lawama,” alisema msanii huyo ambaye
aliomba hifadhi ya jina.
MDOGO WAKE ABANWA
Waandishi wa habari hizi
walifunga safari hadi Sinza–Mori, Dar zilipo Ofisi za Kanumba The Great
Film na kuzungumza na mdogo wa marehemu Kanumba, Seth Bosco ambaye
alisisitiza kampuni ya marehemu kaka yake haijafilisika kama maneno
yalivyozagaa mitaani.
“Hao wanaosema eti kampuni ya Kanumba imefilisika wanakurupuka tu,
hawana cha kufanya lakini nataka kuwahakikishia kuwa, hatujayumba ila
tunakabiliwa na changamoto za kawaida tu kama inavyokuwa kwa kampuni
nyingine,” alisema Seth.
HIACE, TOYOTA GX 110
WIKIENDA: Lakini Seth kuna
maneno kuwa lile gari aina ya Toyota GX 110 na Toyota Hiace lilikokuwa
likitumika kwenye kurekodi sinema yameuzwa, ni kweli?
SETH: Ni kweli
Hiace tumeiuza lakini tumenunua Noah kwa kazi hiyohiyo ya ‘location’,
kuhusu GX 110 halijauzwa, lipo nyumbani hata sasa hivi ukienda
utalikuta.
KUHUSU LEXUS
WIKIENDA:Tulisikia gari alilokuwa akitembelea marehemu Kanumba, Toyota Lexus limeuzwa. Ni kwa nini na liliuzwa kwa bei gani?
SETH:
Kama familia tuliamua kuliuza kwa sababu ya gharama za uendeshaji. Lile
gari linatumia mafuta mengi sana na matengenezo yake ni makubwa na
hatukuona sababu za kuingia kwenye gharama kubwa za namna hiyo.
Kuhusu bei lililouziwa, kwa kweli sifahamu. Kama unavyojua baada ya
mtu kufariki dunia, huwa kuna msimamizi wa mirathi, yeye ndiye anayejua
kuhusu hilo.
UZALISHAJI
WIKIENDA: Kipindi cha Kanumba, alikuwa
akitoa sinema nyingi sana, nadhani kama sikosei ilikuwa moja kila baada
ya miezi miwili wakati mwingine kila mwezi sinema moja lakini baada ya
yeye kuondoka, uzalishaji hakuna tena.
Mfano mpaka sasa kuna sinema mbili tu sokoni tangu alipokufa ambapo inakaribia miaka miwili sasa. Tatizo ni nini?
SETH: Ni kweli, lakini si kwa sababu ya tatizo la fedha – ni uhitaji.
Unajua kuna changamoto nyingi sana kwenye tasnia yetu. Ni kweli mpaka
sasa tumetoa sinema mbili; Malaika na Wonderful Girl ambayo tayari iko
kwa msambazaji lakini bado haijaingia mitaani.
Mwaka huu ndiyo tumeanza, kuna kazi moja tunaifanya sasa hivi, ingawa
si ya kwetu, sisi tunasimamia kwenye production (kuizalisha) lakini
mipango ya mwaka huu ni mikubwa, mapema sana, tutaanza kurekodi kazi
yetu nyingine, kwa sasa siwezi kusema jina lake ila inakuja.
OFISI VIPI?
WIKIENDA: Kwa nini muda mwingi ofisi inakuwa imefungwa tofauti na ilivyokuwa kwa marehemu Kanumba?
SETH:
Kaka hii ni kampuni, sisi tunafanya biashara na mteja wangu hahitaji
kunifuata. Mimi mteja wangu ni Steps, ambaye namtayarishia kazi kisha
nampelekea.
Milango inaweza kuwa imefungwa lakini kazi za ‘editing’ zikawa
zinaendelea ndani au tukafunga ofisi lakini tukawa location tunarekodi,
kuna tatizo gani hapo?
WIKIENDA: Lakini marehemu alikuwa anauza hadi filamu hapa ofisini? Imekuwaje siku hizi?
SETH: Hatujawahi kuuza sinema hapa ofisini ila tulikuwa tunaweka kama
mfano wa kazi zilizowahi kufanywa na marehemu – si za watu wala kampuni
nyingine. Lengo lilikuwa kuwapa watu wanaotutembelea (bure), si kwa
kuwauzia.
Bila shaka maelezo hayo ya Seth yatakuwa yamejibu maneno yote yanayosemwa mitaani
No comments:
Post a Comment