19 February 2014

LULU AANIKA UKWELI JUU YA KIFO CHA MAREHEMU KANUMBA

MWANGA umeanza kuonekana juu ya kesi inayomkabili staa wa filamu za Bongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ ya kumuua bila kukusudia staa mwenzake wa muvi, Steven Charles Meshack Kusekwa Kanumba ambapo safari hii aliamua kukiri vipengele kibao, Risasi Mchanganyiko lina habari yote.
Elizabeth Michael 'Lulu' aliyeambatana na Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ wakiwa eneo la mahakama.
Akikiri mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania juzi (Jumatatu) wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa, nyota huyo aliweka wazi mambo ambayo hapo awali hakuwahi kuyakubali kortini jambo lililovuta hisia za wasikilizaji waliokuwa wamefurika ndani ya chombo hicho cha kutoa haki kujua kinachoendelea.
Mwendesha mashitaka wa upande wa serikali, Monica Mbogo alivitaja vipengele kadhaa ambavyo Lulu alitakiwa kuvikana au kuvikubali.
Katika kesi hiyo iliyoendeshwa kwa ustadi mkubwa wa wanasheria kuoneshana ujuzi wa kusoma na ‘kubugia’ vipengele vigumu vya sheria, Lulu alipata wakati mgumu wa mambo kiasi cha kumwita wakili wake, Peter Kibatala mara kwa mara.
MADAI YA KUMUUA KANUMBA BILA KUKUSUDIA
Lulu alikiri kwamba, mashitaka yake mahakamani hapo yalikuwa ya kumuua bila kukusudia, marehemu Steven Kanumba Aprili 7, mwaka 2012.

KUWEPO ENEO LA TUKIO NA KUTOKEA KWA UGOMVI
Katika maelezo yake, Lulu aliweka bayana kuwa siku ya tukio alifika nyumbani kwa marehemu maeneo ya Sinza ya Vatican jijini Dar saa 6 usiku na kuingia moja kwa moja chumbani.
Alizidi ‘kuchezesha taya’ kuwa, kulitokea ugomvi kati yake na marehemu licha ya kutotaja chanzo cha ugomvi huo.

Aliongeza kwamba, Kanumba alimvuta mkono na kumrudisha ndani wakati alipokuwa akijaribu kukimbia na kuufunga mlango, mwishowe alifanikiwa kutoka na kukimbia kusikojulikana.
KUKAMATWA KWAKE BAMAGA
Lulu aliweka wazi kuwa, siku ya tukio, saa 11alfajiri alikamatwa maeneo ya Bamaga- Mwenge jijini Dar es Salaam alipokuwa akijaribu kutorokea kusikojulikana.

KUHUSU UHUSIANO
Bila kupepesa macho wala kuchezesha kope, Lulu alikubali kuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu Kanumba kwa muda ambao hakuutaja hali ambayo baadhi ya watu walionesha kuwa ‘sapraizidi’.

AMWAGA MACHOZI KORTINI
Awali, Lulu alipofika mahakamani hapo akiwa ameongozana na mama yake mzazi, Lucresia Karugila na staa wa muvi za Kibongo, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ alionekana kuwa na amani.

Msanii huyo alimudu kusoma Gazeti la Ijumaa Wikienda ambalo liliingia mtaani siku hiyo. Lakini baada ya kuanza kwa kesi, ilifika mahali alidondosha machozi hali iliyomlazimu kujifuta uso kwa kitambaa.
Baadhi ya watu walinong’ona kuwa, mrembo huyo alikuwa analizwa na kumbukumbu za tukio la kifo cha Kanumba na kwa sababu ya kuogopa kesi.

MAMA KANUMBA ASUSA
Habari nyingine zilidai kuwa, mama wa marehemu Kanumba, Flora Mtegoa hakutokea mahakamani hapo licha ya umoja na udugu alionao kwa sasa na familia ya  Lulu.

Ilidaiwa kuwa sababu kubwa ya kushindwa kufika kortini ni kukosa uamuzi wa upande gani angekaa kati ya mshtakiwa (Lulu) na mshitaki (Jamhuri) kwa vile kote kuna muhusu kwa sasa.
“Unajua mama Kanumba alipogundua kwamba anayetakiwa kujibu madai ni Lulu ambaye baada ya kutoka mahabusu alimtangaza ni mwanaye na anayelalamika ni serikali, alishindwa kujua akija leo (juzi) angekaa upande gani? Akaamua kutokufika kabisa,” kilisema chanzo chetu.
Risasi Mchanganyiko lilimsaka kwa simu mama huyo lakini bila mafanikio kufuatia simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila kupokelewa.
TUJIKUMBUSHE KIDOGO
Lulu alikamatwa kwa kosa la kumuua bila kukusudia aliyekuwa galacha wa filamu za Kibongo, marehemu Steven Kanumba mnamo Aprili 7, 2012 nyumbani kwake, Sinza Vatican jijini Dar.

Baada ya kukamatwa na kuswekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar, Lulu alipandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo hakutakiwa kujibu ndiyo au hapana.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa mahakama hiyo haikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi ya madai hayo.
Aliachiwa kwa dhamana Januari 29, 2013 na kuambiwa kwamba kesi yake itakaporudi, itakuwa chini ya mahakama kuu. Juzi ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname