25 February 2014

HARARE, Zimbabwe: Mugabe awataka viongozi wa Africa wamheshimu Nyerere

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe. 
RAIS wa Zimbabwe Robert Mugabe aliwalaumu viongozi wa Kiafrika kwa kutomheshimu aliyekuwa rais wa Tanzania marehemu Julius Nyerere kwa mchango wake katika ukombozi wa bara hili.
Kiongozi huyo wa miaka 90 alikuwa akiongea wakati wa sherehe ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwake, iliyoandaliwa na wafanyakazi wa afisi yake baada ya kurejea kutoka Singapore mnamo Jumamosi, alikokuwa ameenda kufanyiwa upasuaji wa jicho.
Alisema kuwa viongozi hao wanapaswa kujitahidi katika utambuzi wa mchango wa kiongozi huyo, ambaye aliwapa hifadhi wahanaharaki wengi wa vita vya ukombozi katika nchi yake.
Marehemu Nyerere anaaminika kuchangia pakubwa katika kuhakikisha kuwa Bw Mugabe alitwaa mamlaka.
Aliripotiwa kumpemdelea dhidi ya mpinzani wake mkuu marehemu Dkt Joshua Nkomo, ambaye anachukuliwa na wengi kama mwanzilishi wa uanaharakati wa kitaifa nchini humo.
Watoto wengi wa shule walikuwa miongoni mwa umati uliokuwa ukipeperusha bendera, ukimrimbikizia sifa kiongozi huyo mkongwe.
Kulikuwa na maonyesho ya keki kubwa zilizokuwa zimewekwa kati mwa uwanja wa Marondera, ulio kilomita 80 kutoka Harare. Umati huo ulikuwa umevaa mavazi mekundu, kama ilivyo desturi wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa rais.
Katika hotuba iliyodumu kwa zaidi ya saa moja, alisema kuwa Wazimbabwe hawaichukii Uingereza, iliyoitawala, lakini wanaipenda nchi yao sana.
Pia, aliwalaumu mashoga kwa kuendesha kile alichotaja kama 'vitendo visivyo vya kibinadamu.’
Gharama ya maadhimisho hayo ilikisiwa kuwa zaidi ya Sh85 milioni, na imepelekea baadhi ya wakosoaji wake kutoa hisia kali kuhusu kiwango hicho, walichotaja kama ubadhirifu katika nchi inayokabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi.
“Ningependa kusema kuwa wakati heshima zinatolewa kwa viongozi waliotetea na kupigania ukombozi wa Afrika, Mwalimu Julius Nyerere ndiye amekuwa akisahaulika sana,” akasema Rais Mugabe mnamo Jumamosi.
“Ni Tanzania iliyowasaidia wanaharakati wengi kwa makao na hata kifedha. Lakini hakuna lolote ambalo limetajwa kuhusu kiongozi huyo na nchi yake na uliokuwa Muungano wa Nchi za Kiafrika (OAU). Kwameh Nkrumah wa Ghana alipewa heshima zake. Lakini Nyerere na Tanzania hawakupata utambuzi wowote,” akasema rais huyo.
Deni
Rais huyo ambaye ndiye naibu mwenyekiti wa Muungano wa Afrika (AU) alisema kuwa bara hili linapaswa kufahamishwa deni ililo nalo kwa Dkt Nyerere.
“Ningetaka sisi kama Wazimbabwe kumtambua Dkt Nyerere. Bara la Afrika linapaswa kukumbushwa wajibu aliotekeleza kiongozi huyo katika ukombozi wake. Nchi yake ndiyo ilikuwa makao ya utoaji mafunzo kwa wanaharakati walioshiriki katika harakati za ukombozi,” akasema.
“Ni mzigo ambao haukuwa wa kisiasa tu. Tanzania inapaswa kutambuliwa kwa mchango iliyotekeleza,” akaongeza.

Rais Mugabe ni mojawapo ya viongozi walioshiriki katika ukombozi wa nchi zao ambaye anazidi kushikilia uongozi.

Chanzo: swahilihub.com

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname