Mwanafunzi
ambaye anataka kupata alama za juu katika mtihani wake lazima awe mtu
wa kujiandaa kila siku kwa kutumia dondoo zifuatazo ili kujihakikishia
uwezo wa kufaulu na kuepukana na dhana ya kuishi kwa kutegemea bahati.
KWANZA: Kama
nilivyosema hapo juu jambo la kwanza ni kuzingatia muda, si vema
kukurupuka na kukimbizana nao na kujinyima usingizi wakati ratiba ya
mtihani ilikuwa inafahamika na muhusika alikuwa na uwezo wa kujiandaa
taratibu kuelekea kwenye siku ya kutahiniwa kwake.
PILI: Jindae
mwenyewe kwa kutafuta na kufanya mitihani iliyopita, huku ukinakili
maswali ambayo watunzi wamekuwa wakiyarudia rudia kila mwaka.
Njia
hii itakuwezesha kujiandaa kwa kuzingatia shabaha na mahitaji halisi ya
maswali yatokayo mara nyingi kwenye mitihani. Hakikisha unapata
mitihani ya nyuma ya ngazi uliyopo isiyopungua kumi au zaidi na uifanye
huku ukihakikisha hakuna swali hata moja ambalo linakushinda.
Pamoja
na ukweli kwamba ubahatishaji wa vitu si njia sahihi sana, lakini
umeonekana kuwasaidia wale ambao ubahatishaji wao huambatana na umakini,
hivyo mwanafunzi anatakiwa kuwa na tabia ya kubahatisha maswali ambayo
anadhani mwalimu wake anaweza kuyatoa kutoka kwenye daftari lake na
hivyo kujiandaa.
Ubaharishaji
huu, lazima uambane na kile nilichosema awali, yaani kuwa na
kumbukumbu ya mitihani iliyopita. Wanasema watalaamu kuwa ulimwengu una
tabia ya kurudia matukio, hivyo hata kwenye maswali kuna tabia hii ya
kujirudia rudia.
TATU: Orodhesha
maeneo yote ambayo huyaelewi kwenye mtihani hiyo ya nyuma na uyafanyie
mazoezi kwa kupata ushauri kwa waalimu wako. Kama kuna mada ambazo
hujazielewa kwenye daftari lako hakikisha muda uliojiwekea utatosha
kuzielewa.
NNE: Hakikisha
unajizoeza kufanya mitihani ya majaribio mara kwa mara, ambayo
utaifanya kwa kuzingatia muda na masharti yote ambayo hutolewa siku ya
kufanya mtihani halisi. Haifai mwanafunzi kukimbia majaribio
yanayotolewa darasani na mwalimu wake, kwani hayo ndiyo yatamuwezesha
kufahamu kama amekamilika kwa kutahiniwa au bado kuna eneo linamtatiza.
TANO: Hakikisha
kuwa kumbukumbu zako kichwani zinaongezeka kadiri unavyojifunza, usiwe
mtu wa kusahau sahau uliyojifunza na ikiwezekana eneo ambalo unaonekana
kulisahau ndilo ulipe kipaumbele cha kujikumbusha, ikibidi hata kila
siku.
SITA: Angalia
kwa makini alama zako za mitihani ya majaribio, ikiwa unapata alama za
chini ujue kuna mahali panahitaji nguvu za ziada, shauriana na mwalimu
wako maeneo yote unayokosa au yanayokusumbua kabla ya siku ya mtihani.
SABA: Ili
mwanafunzi awe na uhakika wa kufanya vema mtihani wake anatakiwa
kuzingatia dondoo zote zilizotolewa kwenye kipengele cha kuimarisha
kumbukumbu kichwani, ambazo zimo ndani ya kitabu hiki.
NANE: Wakati
mwingine ni vema ukausikiliza mwili, si vema kuulazimisha kusoma hata
kama unaona kuna udhaifu, baadhi ya wanafunzi hukesha wiki mbili
mfululizo wakisoma, matokeo yake mwili na akili huchoka na kushindwa
kupokea masomo vizuri. Muda wa kupumzika unahitajika.
TISA: Kabla
mwanafunzi hajaingia katika chumba cha mtihani anatakiwa kujiamini kwa
kushinda hofu. Eneo hili ni muhimu sana kwani kuna wanafunzi hufeli si
kwa sababu hawakujiandaa, bali hukumbwa na hofu muda mfupi kabla ya
kuanza mtihani. Hivyo ni muhimu mwanafunzi akaandaliwa kisaikolojia na
waalimu pamoja na wazazi wake jinsi atakavyoweza kufanya mtihani bila
hofu.
KUMI: Imani
ni hitimisho la mafanikio ya mwanafunzi, haifai kuingia katika chumba
cha mtihani ukiwa na mawazo hasi. Kinachotakiwa ni ari ya ushindi au kwa
lugha nyingine ni mawazo chanya. “LAZIMA NIFAULU MTIHANI HUU” Imani hii
inaweza kujengwa na mtu kupitia kujiamini mwenyewe au kuamini kwa
msaada wa nguvu za imani yake ya dini.
No comments:
Post a Comment