14 November 2013

WAWILI WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA BAADA YA KUKUTWA NA HATIA KWENYE KESI YA MAUAJI MBEYA.....

WATUHUMIWA wawili kati ya wanne wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya. Hukumu hiyo ilitolewa jana katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya iliyokuwa ikiendesha vikao vyake katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe chini ya Jaji Samweli Karua, baada ya kuahirishwa kutolewa kwa hukumu hiyo kwa zaidi ya mara tatu na kuzua hali ya sintofahamu kwa ndugu wa washtakiwa na wafuatiliaji wa kesi hiyo.
Watuhumiwa wawili wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, Kelvin Myovela(kushoto), aliyehukumiwa kifungo cha miaka saba jela na David Mwasipasa(Kulia) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya.
Mhukumiwa namba moja wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Hakimu Mwakalinga(kushoto) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa na mwenyeshati la Bluu ni Obote Mwanyingili amehukumiwa miaka saba jela kwa kumhifadhi mtuhumiwa.(Picha na Ezekiel Kamanga, Mbeya)


Awali kabla ya kusoma kwa hukumu hiyo Mwendesha mashtaka wa Serikali., Archiles Mulisa, aliwataja watuhumiwa wote wanne kuwa ni Hakimu Mwakalinga, Daudi Mwasipasa, Obote Mwanyingili na Kelvin Myovela wanaokabiliwa na tuhuma za kumuua kwa maksudi aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe John Mwankenja.


Alisema watuhumiwa hao wenye kesi namba 131/2012 walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.

Mulisa aliyekuwa akisaidiwa na Wakili wa Serikali Lugano Mwakilasa kwa upande wa mashtaka huku  Watuhumiwa wakitetewa na Mawakili wawili ambao ni Victor Mkumbe na Simon Mwakolo. 

Mulisa alidai mahakamani hapo kuwa kesi inayowakabili  watuhumiwa hao walilitenda Mei 19,2011 kwa kumuua kwa maksudi John Mwankenja kinyume na kifungu cha 196 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Karua ambaye alianza majira ya saa 14:37 mchana na kukamilisha saa 15:37 alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka na utetezi haubishaniwi kuhusu kifo cha marehemu.

Aliongeza kuwa pande hizo mbili pia hazibishaniwi kuhusu ripoti za kitaalamu na dhamira za mauaji hayo bali kinachobishaniwa ni uhusika wa watuhumiwa hao dhidi ya mauaji hayo.

Alisema katika kutetea hoja zao upande wa mashtaka ulileta mashahidi 11 ambao wote kwa pamoja  wakiongozwa na shahidi namba moja waliwatuhumu washtakiwa kuhusika na tukio hilo.

Shahidi huyo namba moja Weston Jacob(17) mkazi wa Kiwira Mwanafunzi kidato cha Tatu katika shule ya Sekondari Kipoke ambaye pia ni Mjomba wa marehemu ambaye aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio akiwa nyumbani akijisomea majira ya 2: 30 usiku ambapo marehemu alifika nyumbani na kupiga honi ya gari akitaka afunguliwe mlango.
Mbali na ushahidi huo Jaji Karua alisema pamoja na ushauri wa wazee wa baraza la mahakama ambao pia wanawatuhumu washtakiwa hao kuhusika na tukio hilo nae anakubaliana nao lakini siyo kwa watuhumiwa wote.

Kutokana na ushahidi huo alisema Mshtakiwa namba moja na namba mbili ambao ni Hakimu Mwakalinga na Daudi Mwasipasa wanatiwa hatiani kuhusika moja kwa moja na mauaji kutokana na ukiri wao kwa mlinzi wa amani, Mchukua maelezo na  vipimo vya vinasaba.

Alisema Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili yeye anatiwa hatiani kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji hivyo yeye hausiki moja kwa moja na kosa hilo.

Jaji karua alisema kwa upande wa mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela anatiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika nkatika mauaji hayo ingawa hakusika na kitendo hicho moja kwa moja.

Aliongeza kuwa kutokana na kifungu cha sheria cha mwenendo wa makosa ya jinai kifungu namba 300 na 217 washtakiwa namba tatu na namba nne wanatiwa hatiani na mahakama.

Mwendesha mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa, aliiambia mahakama hiyo kwamba itoe adhabu kali kutokana na kitendo alichofanyiwa marehemu na iwe fundisho kwa watu wengine.

Kwa upande wa utetezi ambao siku ya hukumu uliwakilishwa na Wakili Merick Luvinga alisema mahakama iwanee huruma washtakiwa kwa kuwa wote umri wao ni mdogo wanaweza kujifunza na kurudi kuungana na jamii pia ni kosa lao la kwanza hivyo wasipewe adhabu kali.

Kutokana na utetezi huo, Jaji Karua alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuthibitisha kuhusika pasipo shaka kwa washtakiwa namba moja na namba mbili hivyo adhabu yao ni kunyongwa hadi kufa.

Aliongeza kuwa Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili anayehusika kumhifadhi mtuhumiwa wa kwanza ataenda jela miaka saba kwa kosa hilo sambamba na mshtakiwa namba nne  Kelvin Myovela aliyehifadhi silaha iliyotumika kwenye mauaji.

Alisema kutokana kosa hilo mtuhumiwa huyo atatumikia kifungo jela miaka saba ingawa pia tayari alikuwa amehukumiwa kifungo jela cha miaka 20 kwa kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria

No comments:

Post a Comment

Comments system

Disqus Shortname