13 November 2013
UNATARAJIA KUINGIA KWENYE NDOA AU NDOANO
WENGI wanapenda sana ndoa, wanatamani kuoa au kuolewa. Ni jambo zuri, la heri na lenye heshima kubwa sana. Hata hivyo, ukiingia kwenye maisha ya muunganikio usiyo sahihi, maisha yako yanaweza kubadilika na kuwa machungu. Utaishi maisha ya kilio kila siku, hutakuwa na amani wala furaha kwa sababu utakuwa umeingia kwenye ndoa ambayo waswahili wanasema ni ndoano. Ni vizuri vijana wakatafakari hili kwa makini kabla ya kuingia kwenye muunganiko huo. Sikia nikuambie...ukifanya makosa leo mara moja tu, unakuwa umeyagharimu maisha yako yote. Najua vijana wengi (hasa wasichana) wanapata wakati mgumu sana unapofikia wakati ambao
wanadhani umri wao unawapasa kuingia kwenye ndoa bila mafanikio.
Zipo dhana nyingine ambazo si sahihi. Msichana akiwa na zaidi ya miaka 27 bado hajaolewa, anajiona ana nuksi na amekosa bahati ya kupata mume wake wa ndoa. Eti ndoa ni bahati! Si kweli. Si suala la bahati...huja kwa wakati unaostahili! Utakuja kumsikia mwingine anasema: “Ni bora niolewe na yeyote atakayekuja mbele yangu, maana nahisi nina nuksi. Hakuna anayetaka kunioa, kama ni kupenda nitajifunzia huko huko.” Huu si mtazamo sahihi marafiki zangu. Suala la ndoa si la kubahatisha. Ujue kwamba ukiingia kwenye ndoa kwa lengo la kuondoa nuksi, kweli itakuwa hivyo...maana utaolewa ili uonekane halafu siku mbili tatu, unaachika! JIULIZE MASWALI HAYA YA MSINGI Kabla ya kuamua kuingia kwenye uhusiano (hasa ndoa) na mwenzi uliyempenda, yapo mambo ya msingi sana ambayo ni vyema kama ungeyapa kipaumbele kichwani mwako. Huna sababu ya kuingia kwenye ndoa kama majibu ya maswali yako uliyojiuliza si mazuri. Yana viashirio vibaya. Lazima kwanza majibu yako yawe mazuri yenye kukupa matumaini mapya katika maisha yako ya ndoa. Twende tukaone hayo maswali. NI MWEZI WA NDOTO ZAKO? Jambo la kwanza kabisa kujiuliza kichwani mwako ni kwamba, kabla ya kukutana na huyo ambaye unatarajia kuingia naye kwenye ndoa, awali uliota kuwa na nani? Lazima kichwani mwako ulikuwa na mtu uliyekuwa unawaza kuwa naye. Zipo sifa za kawaida ambazo mtu anaweza kuvutiwa nazo kabla ya kukutana na mtu ambaye anadhani anaweza kuwa wake kwenye ndoa. Itakuwa vichekesho mwanaume kukubali kuingia kwenye ndoa na mwanamke mwembamba sana, wakati kichwani mwake alikuwa akivutiwa zaidi na wanawake wenye maumbo makubwa! Ndugu zangu, ingawa wengi wanakwepa ukweli huu lakini ni kweli kabisa kuwa, kila mmoja huwa na chaguo lake kichwani kabla ya kukutana na mhusika wake. Uliwaza nini kabla? Kuwa na mwanaume mweusi au mweupe? Acha kubahatisha, hakikisha unayekuwa naye ni yule ambaye ulitamani kabla ya kukutana naye. Ukilazimisha kuwa na mtu ambaye unajua wazi kwamba moyo wako haujaridhika ni tatizo kubwa sana hapo baadaye. Lazima awe na vigezo vile muhimu ambavyo kweli unavihitaji kutoka kwa mwenzi wa maisha yako. Kumbuka kwamba, ukishangia kwenye ndoa si rahisi kutoka. Utakuwa naye siku zote za maisha yako. Je, itakuwaje utakapoanza kuhisi upungufu wake au kutamani wengine nje ya ndoa yako, wakati tayari umeshaingia ndani? Tafakari hili kwa makini. CHAGUO HALISI LA MOYO Siri ya pendo la dhati lipo ndani ya moyo wa mhusika. Lazima moyo wako ukiri kwamba aliye mbele yako unavutiwa naye kwa kila kitu. Hutakiwi kuwa na ukakasi wowote moyoni mwako. Maana kuna mwingine utamsikia akisema: “Ni mzuri lakini siyo sana...sijapenda kabisa matege yake, lakini si vibaya maana ana macho mazuri, sema hana shepu kali sana...nitaoa hivyo hivyo, marafiki zangu wote wameshaoa nimebaki mimi. Huu ni mtazamo hasi rafiki zangu. Kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa, lazima moyo wako uridhie na ukupe kibali rasmi kwamba, sasa nenda kwake, maana huyo ndiye niliyempenda! Hapo sasa unaweza kupiga hatua moja mbele na kuamua bila kuwa na shaka yoyote kwamba huyo ndiye. KASORO ZAKE? Hakuna aliyekamilika chini ya jua, lakini kuna wengine kasoro zao zinavuka mipaka. Ni kweli ni vyema kujifunza kusamehe lakini kuna maeneo mengine ni magumu zaidi kuweza kusameheka kwa urahisi. Mfano umemfumania mpenzi wako zaidi ya mara tatu, hutakiwi kuendelea kung’ang’ania kwamba unampenda na unataka kuingia naye kwenye ndoa. Uchumba tu umemfumania mara tatu, mkioana si ndiyo ataingia na mpenzi wake hadi chumbani kabisa? Hakuna sababu ya kukimbilia ndoa marafiki zangu, lakini jambo la msingi ni kujua unakwenda kwenye ndoa na nani. Naamini kuna vitu umejifunza. Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment